Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Kasi ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kupunguza msongamano
wa magari jijini Dar es Salaam inaonekana si ya kuridhisha licha ya
ukubwa wa tatizo lenyewe.
Miradi hiyo ilitangazwa bungeni na Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli katika hotuba yake ya Bajeti ya Mwaka 2013/2014.
Baadhi ya miradi iliyotangazwa na waziri ni pamoja na ujenzi wa barabara za juu kwenye makutano ya barabara (flyover).
Mradi huu bado haujaanza kutekelezwa licha ya Dk.
Magufuli kulieleza Bunge kuwa wakati ule walikuwa katika mchakato wa
kumpata mkandarasi.
Mradi mwingine ni ujenzi wa kivuko au boti kutoka Dar es Salaam mpaka Bagamoyo chenye uwezo wa kubeba watu 300.
Mradi huu pia ungesaidia kwa kiasi kikubwa
kupunguza msongamano kwani baadhi ya watu wangesafiri kwa kutumia kivuko
au boti maalumu mpaka Bagamoyo.
Dk. Magufuli alisema katika hotuba yake kuwa
mkandarasi wa mradi huo alikuwa amepatikana na usanifu wa maegesho
matatu ulikuwa unaendelea.
Mpaka sasa hamna shughuli zozote zinazohusu mradi huo zinazoendelea, licha ya tamko hilo kutolewa na waziri mwenyewe.
Meneja wa Tanroads Mkoa wa Dar es Salaam, Julius
Ndyamkama alisema ujenzi wa kivuko unaendelea mjini Bangladesh, India na
mwezi wa tano kivuko hicho kitawasili nchini.
Ndyamkama alisema Tanroads wameanza maandalizi ya
ujenzi wa Flyover maeneo ya Tazara na mpaka sasa wameondoa mabango ya
matangazo, mabomba na nguzo za umeme eneo ambako litajengwa daraja la
juu.
“Kuhusu barabara alizozisema waziri, tayari
makandarasi wameshapatikana na mikataba yote tuliyoingia ipo kwa
Mwanasheria Mkuu. Utekelezaji utaanza baada ya Mwanasheria Mkuu kupitia
mikataba hiyo,” alisema Ndyamkama.
Tatizo la msongamano wa magari Dar es Salaam
limeongezeka zaidi kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo ujenzi wa
mradi mwingine wa barabara za Mabasi Yaendayo Kasi (Dart).
Suluhisho la kudumu la tatizo hili lingekuwa kufungua barabara
nyingine ambazo pia zipo katika miradi ya wizara hiyo, ili kutoa nafasi
ya kuendelea na ujenzi, wakati huohuo kupunguza foleni.
Ujenzi na upanuzi wa Barabara ya Morogoro (Mbezi) –
Malamba Mawili – Kinyerezi – Banana bado unasuasua. Barabara hiyo ni
mbaya, haijajengwa kwa kiwango cha lami.
Umuhimu wa barabara hii ni kupunguza msongamano wa magari katika Barabara za Mandela na Morogoro.
Barabara nyingine zilizo kwenye miradi ya wizara
katika kupunguza msongamano Dar es Salaam ni ile ya kilomita 20 kutoka
Tegeta–Kibaoni–Wazo– Goba – hadi Mbezi Mwisho.
Nyingine ni Kimara Baruti – Msewe - Changanyikeni, Tangi Bovu – Goba na Kimara – Kilungule – External (Mandela Road).
Katika barabara zote hizi, Dk. Magufuli alisema usanifu wake ulikuwa umekamilika.
Msemaji wa Wizara ya Ujenzi, Martin Ntemo alisema
ujenzi wa barabara hizo ulichelewa kwa sababu mchakato wa kuwapata
makandarasi unafanywa na wadhamini wenyewe ambao ni Wajapani.
Ntemo aliongeza kuwa ujenzi wa awamu ya pili wa barabara hizo utaanza muda wowote kwani makandarasi wameshapatikana.
“Tunatarajia kupokea kivuko kipya Mei mwaka huu.
Kivuko hiki hakijachelewa, kimefuata taratibu zote kama ilivyotakiwa,”
alisisitiza Ntemo.
Hata hivyo, kasi ya utekelezaji wa miradi hii
haiendani na ukubwa tatizo. Wengi wanatarajia kuwa barabara za mzunguko
(ring roads) ambazo ni za muda mfupi zingejengwa haraka ili kusaidia
wakati wa ujenzi wa miradi mikubwa ya muda mrefu.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment