Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Wiki ya Machi 18 - 22, 2014, mwenyekiti Tume ya Mabadiliko ya
Katiba, Jaji Joseph Warioba aliwasilisha Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kwenye Bunge la Katiba.
Wiki hiyo iliishia siku ya Ijumaa ambayo Rais wa
Jamhuri ya Muungano, Jakaya Mrisho Kikwete alitoa hotuba kwa Bunge hilo
Maalumu.
Hotuba zote zilipokelewa kwa hisia tofauti
kulingana na msimamo wa kila mtu kuhusu hoja inayoonekana ni kubwa
kuliko zote katika Mchakato wa Kuandika Katiba Mpya, hususan suala la
Muundo wa Muungano.
Wale wanaoshabikia muundo wa serikali tatu,
walifurahishwa mno na hotuba ya Jaji Warioba na wanaoshabikia muundo wa
serikali mbili, walifurahishwa mno na hotuba ya Rais Kikwete. Mimi
Sikufurahishwa na hotuba zote mbili kwa sababu zifuatazo;
Hotuba hazikunifurahisha
Moja, hotuba zote mbili zilichukua muda mrefu
zaidi kuelezea sura moja tu ya Rasimu ya Katiba nayo ni sura ya Sita
inayohusu muundo wa Jamhuri ya Muungano kana kwamba Katiba hii inahusu
suala hilo pekee.
Ni dhahiri kwamba suala hili ni kubwa na muhimu,
kwani linahusu uhai wa dola yenyewe na siwezi kubeza. Hata hivyo,
masuala kama Haki za Raia ni muhimu zaidi kwani hata uwe na muundo wa
namna gani wa Muungano au hata Muungano wenyewe kuvunjika, bila ya kuwa
na haki za msingi za raia, katiba hiyo itakataliwa na wananchi.
Huu mtindo unaozuka wa kudhani muundo wa Muungano
ndio mwarobaini wa matatizo ya ufisadi, matumizi mabaya ya madaraka,
ubadhirifu, umasikini, elimu ya hovyo, afya dhaifu, utatufikisha pabaya
na hata kurudi tena kuandika katiba kwa lengo la kudai haki hizo. Jaji
Warioba na Rais Kikwete wameshindwa kuruka kiunzi hicho na kutambua kuwa
Katiba ni zaidi ya Muungano.
Pili, Rais Kikwete na Jaji Warioba wamejenga hoja
zao kuhusu miundo ya Muungano wanayopendekeza au kuunga mkono kutokana
na misingi ama ya ‘malalamiko’ au ‘hofu’.
Jaji Warioba aliorodhesha malalamiko 11 ya upande
wa Zanzibar dhidi ya Muungano na malalamiko kumi ya upande wa Bara.
Kimsingi malalamiko yote ya upande wa bara yanazaliwa na vitendo vya
upande wa Zanzibar, isipokuwa lalamiko namba ‘vii’ linalohusu kupotea
kwa utambulisho wa Tanganyika katika Muundo wa Muungano.
Jaji Warioba anajenga msingi wa pendekezo la tume
yake kutokana na kujibu malalamiko au maarufu kama kero za Muungano na
anasema “Muundo wa serikali mbili hauwezi kubaki kwa hali ya sasa.
Muungano wa serikali mbili waliotuachia waasisi siyo uliopo sasa...
waasisi walituachia Muungano wa nchi moja yenye serikali mbili, na siyo
nchi mbili zenye Serikali Mbili”. Nukuu hii niliipenda kuliko zote
katika Hotuba ya Mzee wangu Warioba.
Rais Kikwete alijenga msingi wa maoni yake kwenye
hofu za kuwa na serikali tatu. Hofu hizo ni pamoja na gharama za
kuendesha Muungano, kuzuka kwa hisia za utaifa wa Utanganyika na
Uzanzibari, uwezekano wa Muungano kuvunjika kwa kushindwa kuhudumia
majeshi na hata Jeshi kuchukua nchi ikibidi na kutupilia mbali katiba na
Serikali ya Muungano kutokuwa na Rasilimali zake
Rais alisema ‘Serikali ya Muungano ni egemezi na tegemezi’ nukuu
ambayo niliipenda kuliko zote katika Hotuba ya mzee wangu Kikwete.
Lakini Rais hakuniridhisha kabisa namna ya
kumaliza kero za Muungano kwa muundo wa sasa kwani umeshindwa kuzimaliza
kwa takribani miaka 50 tangu Muungano uundwe.
Haiwezekani muundo uliozalisha kero lukuki ndio
utarajiwe kuzimaliza kero hizo. Kwa vyovyote vile ni lazima kuwa na
muundo mpya, lakini kiukweli ni lazima muundo huo mpya ujibu hofu
alizoeleza Rais maana ni hofu za kweli.
Naye Jaji Warioba hakuniridhisha na namna suala la
Uraia litakavyotatuliwa kwani kutoa jibu la kubakia na ‘kukubali’ nchi
mbili halafu uraia mmoja kunatia shaka kubwa. Kama tunataka kuwa na
Uraia mmoja ni lazima tuwe nchi moja, hatuwezi kuwa na nchi mbili uraia
mmoja.
Pia vyanzo vya mapato ya Muungano ni vidogo mno
kuendesha dola. Hivyo rasimu iliyopo ina mapungufu makubwa japo imetoa
mapendekezo yatakayomaliza malalamiko.
Kazi ya Bunge sasa ni kuboresha rasimu ili kumaliza kero za Muungano na kuziondoa za hofu za muundo mpya.
Kama kweli tunataka kusikia Watanzania wanataka
nini kwenye muundo wa Muungano, tusimamishe Bunge na twende tukawaulize
kwa kura ya maoni.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment