Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
WAKALA
wa Usajili, Ufilisi na Udhamini Tanzania (RITA) ameanzisha mpango wa
uandikishaji na utoaji vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wanaoanzia umri wa
miaka sita hadi 18 katika shule zote za msingi na sekondari nchini.
Hatua hiyo inatokana na kubaini kuwa ni asilimia 23 tu ya Watanzania
nchini ndio waliosajiliwa na kupewa vyeti vya kuzaliwa.
Akizungumza
wakati wa uzinduzi wa Mpango huo kwa Manispaa ya Ilala Dar es Salaam
jana, Meya wa Manispaa hiyo, Jerry Silaa, alisema utasaidia kuongeza
idadi ya Watanzania wenye vyeti vya kuzaliwa ambavyo ni tiketi ya kupata
mahitaji muhimu na kutambulika kama wazawa wa nchi.
“Asilimia
23 ni ndogo sana, hasa ikizingatiwa kuwa vyeti vya kuzaliwa ni nyaraka
muhimu kwa raia yeyote, ili apate mahitaji muhimu nchini mwake kama vile
hati ya kusafiria, kusoma, kitambulisho cha uraia na hata haki ya
kupiga kura,” alisema Silaa.
Alisema
mpango huo ambao unaanzia Ilala utaanza na shule za msingi za Serikali
ambapo watoto wasiokuwa na vyeti hivyo, kupitia walimu waliopewa mafunzo
maalumu ya usajili na utoaji vyeti hivyo, watasajiliwa na kuvipata
ndani ya wiki moja.
Hata
hivyo, alionya walimu waliochaguliwa kushughulikia usajili huo,
kuhakikisha kuwa wanatanguliza uzalendo na kusajili na kutoa vyeti kwa
watoto ambao wamehakikiwa na kuthibitika kuwa ni Watanzania na si
vinginevyo.
“Napenda
kueleza, kwamba kumekuwa na changamoto ya kukosa uaminifu kwa watendaji
wengi wa Serikali, ambao wanaaminiwa kukusanya fedha. Nasisitiza kwamba
fedha ya Serikali ni lazima iwasilishwe inakotakiwa kwa njia sahihi.
“Naamini
walimu mtakuwa waaminifu na atayefanya kinyume, sheria itachukua mkondo
wake. Naamini walimu wa Manispaa yangu hamtaniangusha katika hili,”
alisisitiza.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Rita, Philipo Saliboko, alisema katika
kutekeleza mpango huo, Wakala huyo ameamua kushirikisha walimu na
waratibu katika usajili na uhakiki wa watoto hao ambapo hatua ya mwisho
itafanywa na watendaji wa Rita kwa kuhakiki taarifa za watoto hao na
kutoa vyeti.
“Awamu
ya kwanza ya mpango huu, tumeamua kuanzia Dar es Salaam, katika
manispaa ya Ilala, na itafutiwa na Kinondoni na kumalizikia Temeke.
Katika mikoa mingine bado mchakato wa kifedha unaendelea ili kuendelea
na mpango huu,” alisema Saliboko.
Alisema
Ilala jumla ya walimu 105 na waratibu 28 ndio watashiriki kusajili
watoto hao kwa kuzungumza na wazazi wao na kuhakiki taarifa zao kabla ya
kuziwasilisha Rita kwa uhakiki zaidi na kuchapishwa kwa vyeti hivyo.
Akizungumzia
shule za msingi na sekondari binafsi, Saliboko alisema watatumia walimu
waliopewa mafunzo, lakini pia watashirikisha taasisi muhimu kama
Uhamiaji ili kutotoa vyeti kwa watoto wasio wazawa wa Tanzania.
Chanzo;Habari Leo
0 comments:
Post a Comment