Home » » Wajumbe CCM watetea serikali mbili

Wajumbe CCM watetea serikali mbili

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Mjumbe wa Bunge maalum la Katiba,Abbas Mtemvu.
 
Watanzania  wametakiwa kujiandaa kisaikolojia kupokea serikali mbili zenye kutatua changamoto za Muungano.

Kauli hiyo ilitolewa na wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambapo pia walisema mchakato wa Katiba mpya unaoendelea sasa utamalizika vizuri na kwa amani na utulivu hadi hatua ya kupiga kura ya maoni kuamua aina ya muundano wa Serikali utakaokuwa umeridhiwa na Bunge Maalumu la Katiba.

Abbas Mtemvu alisema tangu ulipoanza mchakato wa Katiba mpya kumekuwa na kila aina ya maneno ambayo yamekuwa yakiwachanganya wananchi na kwamba CCM bado inaamini katika muundo wa Serikali mbili pamoja na rasimu ya Katiba kutaja muundo wa Serikali tatu.

 “Chama kilipendekeza serikali mbili na wala siyo tatu wala moja. ..kwa hali hii tunawaomba Watanzania wawe watulivu katika kipindi hiki ambacho Bunge Maalum la Katiba likiwa katika mchakato wa kupata kanuni za kuendesha Bunge hilo,” alisema.

Mtemvu  alisema serikali mbili zitatoa jibu la kutatua na hata kuimarisha muungano katika Tanzania Bara na Zanzibar.

Naye mbunge wa Kibaha Vijijini, Hamoud Jumaa, alisema hakuna dhambi kubwa aliyotenda kama kuruhusu Zanzibar kuvunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano.

Alisema matatizo yote yanayoibuka sasa kuhusu muundo wa Serikali, yanatokana na marekebisho ya Katiba ya Zanzibar ambayo ilivunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Alisema marekebisho ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 2010 ndiyo yaliyosababisha Zanzibar kutambuliwa kama nchi ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Kwa hali hiyo tunaamini sisi kama wajumbe wa Bunge hili tutakuwa imara na mara baada ya kumaliza uundwaji wa Katiba hii, tutakuwa na Muungano imara ambao utafurahiwa na kila mwananchi, kubwa wawe na utulivu,” alisema Jumaa.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa