Home » » BABA WA DOMASHO AFUNGUKA

BABA WA DOMASHO AFUNGUKA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
  

Raymond Domayo, baba mzazi wa kiungo mkabaji Frank Domayo, amesema fedha nono ndiyo zilizomshawishi mwanaye atimkie Azam FC, hivyo amewataka viongozi na mashabiki wa Yanga wasimchukie badala yake wamuunge mkono.
Domayo, ambaye alikuwa kiungo tegemeo wa Yanga msimu uliopita, hivi karibuni alimwaga wino wa kuichezea Azam FC kwa mkataba wa miaka miwili na kuvuna kitita cha Sh70 milioni.
Pia, kiungo huyo ambaye mkataba wake na Yanga unatarajiwa kumalizika mwanzoni mwa Juni, atazoa Sh3 milioni kama mshahara wake wa kila mwezi baada ya kujiunga na Azam.
Kwa upande mwingine, uamuzi huo wa Domayo kutimkia Azam uliwakasirisha mashabiki wa Yanga, ambao wamekuwa wakiwashutumu viongozi wao kwa kufanya uzembe uliosababisha kiungo huyo kuwakimbia.
Akizungumza na gazeti hili nyumbani kwake Tabata Kisiwani jana, Mzee Domayo aliwataka viongozi na mashabiki wa Yanga kutambua kwamba soka ni ajira kama zilivyo ajira nyingine, hivyo uamuzi wa mwanaye umetokana na kupata masilahi mazuri na siyo kitu kingine.
“Nawaomba mashabiki wa Yanga wasimchukie mwanangu kwani Azam amekwenda kwa sababu amepata masilahi mazuri zaidi ingawa alikuwa anaipenda klabu ya Yanga.
“Ukweli ni kwamba soka ni kazi kama zilivyo kazi nyingine. Leo hii unaweza kuwa hapa kesho ukahamia kwingine ambako wanakupa masilahi mazuri,” alisema Mzee Domayo. Aliongeza: “Hata hao mashabiki, ikitokea timu inawahitaji wakaishabikie leo hii halafu watalipwa, unafikiri hawataenda? Ni wazi watakwenda kwa sababu ya fedha hata kama wanaipenda klabu yao.
“Isitoshe mimi baba yake sina kazi kwa sasa, hivyo namtegemea yeye na nina watoto wengine bado wanasoma,” alisema Mzee Domayo, ambaye alidai ana taaluma ya udereva. Katibu mkuu wa Yanga, Beno Njovu, akizungumzia kauli ya mzee huyo, alisema: “Hatuna tatizo na Domayo kwa vile amehama Yanga na kwenda Azam kwa mapenzi yake, kwa sasa tunajipanga.”
Chanzo:Mwananchi

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa