Home » » SERIKALI YAICHUNGUZA HOTELI WALIKOFIA WATOTO

SERIKALI YAICHUNGUZA HOTELI WALIKOFIA WATOTO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Kamanda wa Polisi mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura.
Wakala wa Usalama  wa Afya Mahali pa Kazi (Osha), umetuma timu ya wakaguzi kukagua mabwawa ya kuogelea ya hoteli ya Landmark Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam kama yako salama na vigezo vyote vinazingatiwa katika kuyaendesha.
Osha imesema kuwa lengo la kutuma timu ya wakaguzi katika bwawa hilo ni kuangalia usalama wa wafanyakazi wao.

Hatua hiyo inafuatia kufariki dunia kwa watoto watatu Aprili 27, mwaka huu wakati wakiogelea katika bwawa la watu wazima.

Watoto hao walikwenda katika hoteli hiyo kwa ajili ya sherehe ya siku ya kuzaliwa mwenzao.

Osha imesema kwamba kama watoto wadogo walizama na kupoteza maisha bila msaada, hali hiyo pia ni hatari kwa wafanyakazi wa hoteli hiyo.

Mtendaji Mkuu wa Osha, Dk. Akwilina Kayumba, alisema baada ya ukaguzi huo wataandika ripoti kuhusu watakachokibaini.

Alifafanua kuwa kama wakibaini mabwawa hayo hayana vigezo vinavyotakiwa, watayafungia na kuiandikia barua Wizara ya Maliasili na Utalii ili ifanye ukaguzi kuhakikisha yanakidhi vigezo vyote vinavyotakiwa kwa usalama wa wafanyakazi.

“Naomba nieleweke kuwa Osha tuko kwa ajili ya kuangalia usalama wa afya mahali pa kazi kwa wafanyakazi, tunaenda kukagua si kwa kuwa watoto wamezama na kufariki dunia, ni kwa ajili pia  ya usalama wa wafanyakazi wa hoteli hiyo,” alisema Dk. Kayumba na kuongeza:

“Kama majanga yametokea kwa watoto hata kwa wafanyakazi yanaweza kutokea na kusababisha vifo.”

Watoto waliozama na kufariki dunia wakati wakiogelea ni Ndimbuni Bahati (09), Eva Nicholous (09) na Janeth Zacharia (10).

Watoto hao walikuwa wanaogelea katika bwawa la watoto, lakini kutokana na kuwa wengi, baadhi yao walitoroka na kwenda kuogelea katika bwawa la wakubwa lenye kina kirefu cha maji.

Wiki iliyopita, Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia maofisa wa Kitengo cha Leseni (Tala), ilisema  kitendo cha watoto watatu kufariki dunia wakati  wakiogelea katika bwawa la hoteli  hiyo ni uzembe.

Maofisa hao walisema kitendo cha kuwaacha watoto wadogo kuogelea bila uangalizi ni kinyume cha biashara ya uendeshaji hoteli kwa mujibu ya Sheria ya Usajili wa Biashara ya Utalii ya mwaka 2008.

Walisema kwa mujibu wa kanuni za uendeshaji wa huduma za hoteli za kitalii, ni lazima kuwa na wataalamu wanaosimamia shughuli na utoaji huduma mbalimbali katika hoteli.

Walisema kuwa hata kama msimamizi anatakiwa kuundoka mara moja, ni lazima awapo mtu mbadala wa kusimamia watu wanaoogelea bila kujali umri.

Aidha, walisema katika eneo la bwawa, lazima kuwa na waokoaji ambao wanatakiwa kuwapo muda wote kuanzia mmoja hadi watano kutegemea na kina cha maji, kuwapo na maboya na kamba kwa ajili ya kuwasaidia wateja ikiwa litatokea tatizo.

Waliongeza kuwa lazima kuwapo na tahadhari kwa watu waliolewa kutoruhusiwa kuogelea pamoja na kuwazuia watoto wadogo kuogelea katika kina kirefu cha maji.

Walisema Wizara haihusiki katika kuchukua hatua bali vyombo vingine likiwamo Jeshi la Polisi ikiwa itathibitika kuwapo kwa uzembe. Hata hivyo, mwangalizi wa bwawa hilo, Chriss Patrick, alisema watoto hao walikuwa wanakula chakula  jirani ya bwawa hilo, lakini  ghafla walianza  kukimbizana na kurukia katika bwawa  la wakubwa wakati yeye akiwa kwenye bwawa la watoto.

Alisema siku hiyo alikuwa zamu peke yake kutokana na mwenzake aliyetakiwa kuwa naye zamu kupata udhuru wa kuumwa.

Patrick alisema kutokana na kuwa peke yake, alizidiwa majukumu na kushindwa kuwaokoa watoto hao.

Meneja Mkuu wa hoteli hiyo, Wallace Chege, alisema watoto hao walikwenda katika hoteli hiyo kwa ajili ya kupata huduma ya chakula bila kulipia gharama za huduma ya kuogelea.

Chege alisema wakati mwangalizi akiwa anaangalia upande wa bwawa la watoto ndipo watoto hao walianza kukimbizana na kurukia kwenye bwawa la wakubwa kitu kilichopelekea vifo hivyo.

Mjomba wa Janet, John Mbugi, alisema juzi kuwa walisafirisha mwili wa marehemu kwenda Iringa kwa ajili ya mazishi na kwamba mwili wa Ndimbuni ulipelekwa Mbeya.

Mwili wa  Eva Mwakatobe, ulizikwa jana  katika makaburi ya Sinza, jijini Dar es Salaam ambamo Baba yake mzazi akizungumza katika mazishi hayo alisema familia imekaa na kuzungumza na  watu wa hoteli hiyo na wameamua kusamehe na wameshirikiana nao kwa mambo mbalimbali ikiwa kujitolea gari ya kupeleka watu makaburini.
Jeshi la Polisi hadi sasa halijatoa taarifa kuhusiana na hatua lilizozichukua ikiwamo kuwahoji wahusika.

Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova,  Jumanne iliyopita alisema suala hilo ameliacha kwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura.

Hata hivyo, Kamanda Wambura tangu wiki iliyopita amekuwa akitafutwa na kusema yuko kwenye vikao na wakati mwingine simu yake inaita bila majibu.

Jana alipotafutwa simu yake ilikuwa inaita bila majibu. Alipotumiwa ujumbe mfupi (sms), hakujibu na baadaye kuzima simu.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa