Home » » UKOMBOZI DAR WAJA

UKOMBOZI DAR WAJA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Waziri Mkuu,Mizengo Pinda.
 
Wakazi  wa jiji la Dar es Salaam watapata nafuu ya maisha kwa mwaka wa fedha ujao kufuatia maamuzi ya serikali ya kujenga barabara sita mpya kwa kiwango cha lami hivyo kupunguza msongamano ambao umekuwa sugu katika jiji hilo.
Akiwasilisha hotuba ya mapitio na mwekekeo wa kazi za serikali na makadirio ya matumizi ya fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka wa fedha wa 2014/15 mjini Dodoma jana, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alitaja barabara hizo kuwa ni pamoja na Tabata Dampo - Kigogo (km 1.6); Kifuru - Kinyerezi (km 4) na  Goba - Mbezi Mwisho (km 7).

Nyingine ni Tangi Bovu (Samaki) - Goba (km 9); Kimara Baruti - Msewe (km 2.6) na Kimara - daraja la Maji Chumvi External (km 3).

Alisema kuwa tayari Serikali imesaini mikataba na wakandarasi kwa ajili ya ujenzi wa barabara hizo ambazo zinatarajiwa kukamilika kati ya miezi 8 hadi 18.

Pia alisema kuwa katika mwaka wa fedha unaomalizika Serikali imekamilisha ujenzi wa barabara za lami za Ubungo Bus Terminal - Kigogo - Kawawa yenye urefu wa kilometa 6.4; barabara ya Jet Corner –Vituka - Davis Corner yenye urefu wa kilometa 10.3 na barabara ya Ubungo Maziwa - Mabibo External yenye urefu wa kilometa 2.25 pamoja na daraja la External.

Ujenzi wa barabara ya Mzunguko wa Kigogo - Jangwani yenye kilometa 2.72 na zile zitakazotumika kwa Mabasi yaendayo haraka unaendelea.

USAFIRI WA ANGA
Kuhusu usafiri wa anga, alisema serikali itaboresha miundominu ya viwanja vya ndege na kuviwezesha kutoa huduma kwa kuzingatia sheria na kanuni za uendeshaji za kimataifa.

Pinda alisema mwaka 2013/14 viwanja vya ndege 13 vikiwemo vya Mwanza, Musoma, Bukoba, Kigoma, Tabora, Arusha, Tanga, Lindi, Mtwara, Iringa,Songea, Nachigwea na Kila Masoko vilifanyiwa ukaguzi na kupata leseni ya uendeshaji.

”Aidha serikali imeanza mradi wa ujenzi wa jengo jipya la tatu la abiria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere utakaogharimu Shilingi bilioni 518,” alisema.

Aliongeza kuwa mradi huo unatarajiwa kukamilika Oktoba mwakani na jengo hilo litakuwa na ukubwa wa mita za mraba 70,000, ambao ni zaidi ya mara nne ya jengo lililopo sasa lenye ukubwa wa mita za mraba 15,000.

Alisema baada ya kukamilika kwa jengo hilo na muindombinu yake litakuwa na uwezo wa kuegesha ndege kubwa za abiria na kuhudumia abiria milioni 6 kwa mwaka ikilinganishwa na la sasa lenye uwezo wa kuhudumia abiria milioni 2.5.

VITAMBULISHO VYA TAIFA
kuhusu vitambulisho vya Taifa, alisema serikali imekamilisha usajili na utambuzi wa watu kwa upande wa Zanzibar, watumishi wa umma na vyombo vya ulinzi na usalama na wakazi wa mkoa wa Dar es Salaam.

Alisema kwa mwaka 2014/5 zoezi la utambuzi na usajili wa Watanzania litaendelea katika mikoa mingine ili kwa pamoja wanufaike na Vitambulisho vya Taifa katika nyanja za kijamii, kiuchumi na kiusalama.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa