Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Uuzwaji wa hisa za Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) jana
uliibuka upya bungeni baada ya Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema)
kuhoji sababu za Serikali kufuta kesi kuhusu utata wa mauzo hayo.
Suali la UDA limeibuka katika kipindi ambacho
ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)
imebainisha ukiukwaji mkubwa wa taratibu katika mauzo ya hisa za shirika
hilo ambazo zilipaswa kuuzwa na Shirika Hodhi la Mali za Serikali
(CHC), badala ya bodi ya shirika.
CAG Ludovick Utouh anasema katika taarifa yake
kuwa, baada ya kugundua ukiukwaji huo wa sheria aliishauri Bodi ya UDA
kutouza hisa hizo, lakini alipuuzwa.
“Bodi ya wakurugenzi wa UDA iliendelea na uuzaji
wa hisa bila kupata kibali cha Serikali na hata CHC,” inasema sehemu ya
ripoti hiyo.
Swali hilo lilijibiwa na Naibu Waziri wa Fedha,
Adamu Malima lakini majibu yake yalionekana wazi kutowaridhisha wabunge
hao. Malima alisema Oktoba 2000, Serikali iliamua kuipa UDA hisa
3,631,045 kati ya 7,119,697 ambazo ni sawa na asilimia 51, hivyo
kubakiza hisa 3,488,651 sawa na asilimia 49 zilizogawiwa na hadi sasa
hazijauzwa.
Kwa mujibu wa Malima, UDA ilianzishwa Mei 1974 kwa
mtaji wa Sh1.5 bilioni sawa na hisa 15,000,000 kwa bei ya Sh100 kwa
kila hisa. Kati ya hizo, hisa 7,119,697 ziligawiwa na kulipiwa, hisa
7,880,303 zilizobaki hazikugawiwa.
Katika swali la nyongeza, Mnyika alihoji kuwa,
pamoja na CAG kubaini kuna ufisadi katika kuuza hisa za UDA, iweje hadi
sasa umiliki wa kampuni hiyo uko chini ya kampuni ya Simon Group na kwa
nini DPP aliondoa kesi ya uuzaji huo mahakamani.
“Ni kwa nini watuhumiwa wameachiwa? Mheshimiwa
Spika, haya yasipojibiwa tutaamini kuwa jambo hili linawahusu vigogo wa
CCM na mnawalinda katika ufisadi huu,” alisema Mnyika.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Fedha, Adam
Malima alikiri kwamba suala la UDA lina mazingira yenye utata mkubwa na
kuwa DPP baada ya kubaini utata huo, aliiondoa kesi hiyo na Takukuru na
vyombo vingine vya uchunguzi vinaendelea na uchunguzi.
Baadaye, akichangia mjadala wa Wizara ya Katiba na
Sheria, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema alisema
faili hilo lilirudishwa kwa Takukuru likafanyiwa kazi na jana ndio
lilirejeshwa kwa DPP kwa ajili ya uamuzi.
“Ninamshauri DPP wakati anatoa uamuzi asizingatie
mambo yaliyojadiliwa bungeni, bali afuate fikra na taratibu za
kisheria,” alisema.
Hisa za Serikali
Malima alisema mwenye mamlaka ya kuuza hisa za Serikali
hajaziuza na mmiliki halali wa UDA ni Halmashauri ya Jiji la Dar es
Salaam lenye hisa asilimia 51 na Serikali asilimia 49.
Alisema mwaka 2006 Serikali iliamua kuuza hisa
zake kwa lengo la kupata mwekezaji mahiri na mwenye uwezo wa kuboresha
huduma za usafiri Dar es Salaam, lakini haikufanikiwa.
Alisema Januari 2010, Bodi ya UDA iliiarifu
Serikali kwamba amepatikana mwekezaji, Simon Group, ambaye angeuziwa
hisa za Serikali pamoja na hisa 7,880,303 ambazo hazikugawiwa mwaka
1971.
Baada ya kupokea pendekezo hilo, Serikali
iliiagiza Bodi ya UDA kutoendelea na kusitisha mchakato huo, hivyo hisa
za Serikali ndani ya UDA bado hazijauzwa na mgawanyo wa hisa unabaki
vilevile kwa Halmashauri ya Jiji kumiliki asilimia 51 na Serikali,
kupitia Msajili wa Hazina asilimia 49.
Hoja hiyo ilipingwa na Mkurugenzi wa Simon Group,
Robert Kisena akisema kampuni yake ilinunua hisa zaidi ya milioni tatu
za Jiji kwa kufuata sheria na taratibu zote za ununuzi wa hisa.
“Tunamiliki UDA kwa asilimia 76 na Serikali
asilimia 24. Tulinunua hisa hizi kwa taratibu zilizobarikiwa na kamati
ya Bunge. Tena tulilipa kwa bei ya juu baada ya kufanyiwa uthamini
upya,” alisema Kisena.
Ripoti ya CAG inaonyesha thamani ya hisa hizo
wakati zinatolewa ilikuwa ni Sh744.79 kwa kila moja lakini mpaka
zinauzwa thamani yake ilishushwa kwa asilimia 60 na kuuzwa kwa Sh298,
jambo ambalo baadhi ya wabunge wanalielezea kuwa na mwanya wa rushwa.
Mdee na DPP
Katika mchango wake kwenye mjadala wa Bajeti ya
Sheria na Katiba, mbunge wa Kawe, Halima Mdee alimlipua DPP kwa kile
alichodai kukumbatia majalada ya rushwa kubwa kwa maslahi yake binafsi.
Ingawa Mdee hakumtaja DPP kwa jina, lakini
anayeshikiliwa wadhifa huo kwa sasa ni Eliezer Feleshi na mbunge huyo
alitumia fursa hiyo kuhoji kuachiwa kwa mshtakiwa wa kesi ya ufisadi wa
Sh2.4 bilioni za UDA.
Mdee alisema DPP amekuwa akilalamikiwa na
mkurugenzi mkuu wa Takukuru, Dk Edward Hosea kwamba amekuwa kikwazo
katika kushughulikia kesi kubwa za rushwa.
“(Dk Hosea) Akitaka kufungua shauri la rushwa
kubwa, mpaka akaombe kibali kwa DPP… analalamika DPP amekuwa akibania
vibali vya kufungua kesi kwa maslahi yake binafsi,” aliongeza Mdee.
Mdee alimtaka Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Migiro na AG, Jaji Fredrick Werema kulieleza Bunge ni lini watapeleka bungeni sheria ya Takukuru ya mwaka 2007 ili ifaniywe marekebisho.
Chanzo:Mwananchi
Mdee alimtaka Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Migiro na AG, Jaji Fredrick Werema kulieleza Bunge ni lini watapeleka bungeni sheria ya Takukuru ya mwaka 2007 ili ifaniywe marekebisho.
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment