SHIRIKA la Nyumba la
Taifa (NHC) limesema kuwa, tuhuma zinazotolewa kwa Mkurugenzi Mkuu wa
shirika hilo, Nehemia Mchechu kuwa ameundiwa zengwe na bodi ya
wakurugenzi ya NHC kwa nia ya kuhakikisha kuwa harejeshwi tena katika
wadhifa huo baada ya kumaliza muda wake hazina ukweli wowote.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NHC, David Shambwe aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Alisema, taarifa
zilizotolewa na gazeti moja la kila siku (si Majira) zilidai kuwa,
Mkurugenzi huyo ameundiwa zengwe na bodi ya wakurugenzi kuhakikisha
harejeshwi tena katika wadhifa huo, baada ya kumaliza muda wake.
Pia gazeti hilo
lilieleza kuwa, mizengwe hiyo inaungwa mkono na vigogo wa serikali
wakiwemo wabunge ambao kuwepo kwa Mchechu katika shirika hilo
kumewanyima ulaji ikiwemo kupangishwa nyumba za shirika.
Kaimu huyo alifafanua
kuwa katika taarifa hiyo ilieleza pia, Mchechu amewekewa masharti magumu
na bodi hiyo ya kumtaka apunguze idadi ya wakurugenzi wa menejimenti ya
sasa ya shirika hilo.
Shambwe alisema kuwa,
Bodi ya Wakurugenzi ya NHC ina miezi miwili tu, tangu iteuliwe na
mamlaka husika na haijawahi kukaa katika kikao chochote kujadili suala
la kumuondoa Mkurugenzi Mkuu na kupunguza menejimenti ya shirika iliyopo
sasa.
Alisema, Mkurugenzi
Mkuu na menejimenti ya shirika bado wana mikataba halali ambayo
haijamaliza muda wake, hivyo hoja ya kuwa Mchechu na menejimenti yake
wanaundiwa zengwe baada ya kumaliza muda wao haina ukweli wowote.
"Kutokuwepo kwa
Mkurugenzi Mkuu kwenye ufunguzi wa miradi hakutokani na kuwepo mizengwe
kama ilivyoandikwa na gazeti hilo, kwani alikuwa katika likizo yake ya
mwaka iliyoanza Juni 30, mwaka huu hadi Julai 18,"alisema Shambwe.
Aliongeza kuwa, likizo
hiyo ilikuwa stahiki halali kama walivyo watumishi wengine wa umma na
hakuchukua likizo kutokana na kuwepo mizengwe ya kumuondoa kama
ilivyoandikwa na gazeti hilo.
Hata hivyo alisema, NHC
itaendelea kuwa mstari wa mbele kutoa habari makini kwa chombo chochote
cha habari bila kuficha jambo lolote hivyo ni vyema kuhakikisha habari
zinazoandikwa zinakuwa na maelezo kutoka pande zote.
Pia alisema, Watanzania
wanatakiwa kufahamu kuwa hakuna mtafaruku wowote uliopo ndani ya
shirika na wataendelea kutoa huduma bora katika sekta ya nyumba kama
taifa lilivyowaamini.
Chanzo:Majira
0 comments:
Post a Comment