Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Senso
Habari hiyo ilichapishwa na gazeti la NIPASHE ukurasa wa kwanza katika toleo lake la jana.Pongezi hizo zimekuwa zikitolewa na wananchi hao kwa ama kwa kupiga simu au kwa kutuma ujumbe mfupi wa simu ya mkononi (sms) kwenye chumba cha habari cha magazeti ya The Guardian Limited, jijini Dar es Salaam kwa nyakati tofauti jana.
Wote wametaja majina na namba zao za simu, lakini kwa sababu za kiusalama haziwezi kutajwa gazetini.“Asanteni NIPASHE kwa kuliona tatizo la ‘Tigo’,” alisema mmoja wa wananchi hao kupitia sms.
Mwananchi mwingine alisema habari iliyochapishwa na NIPASHE ni ukweli mtupu kwa kuwa yeye ni shuhuda mmojawapo, ambaye amekuwa akiwashuhudia askari hao wakiendesha vitendo hivyo katika maeneo mbalimbali nchini.
“Juzi (eneo la) Goba tu wamechukua laki sita asubuhi. Wamekuwa kero,” alisema mwananchi huyo.
Mwananchi mwingine alisema baadhi ya askari hao, ambao anawafahamu, wengi wao ‘mradi’ huo haramu umewawezesha kujenga nyumba na wengine kumiliki magari kwa kipindi kifupi.
Mkazi wa Mbezi Kimara, jijini Dar es Salaam, mbali na kulipongeza NIPASHE, alisema limesaidia sana kuweka bayana kero kubwa ya askari wa ‘Tigo’.
Alisema askari hao wamekuwa wakipokea rushwa wazi na kwamba kwa mwenendo huo ni lazima kuna watu ndani ya Jeshi la Polisi wanawalinda.
Aliomba kuwapo na mdahalo nchini kote kujadili kero hiyo ili ukweli ujulikane.
Mwananchi mwingine alisema picha ya askari wa ‘Tigo’ iliyochapishwa katika ukurasa wa mbele wa toleo la jana la NIPASHE anamfahamu vyema kwa majina na matendo, ambayo amekuwa akiyafanya kwa kutumia pikipiki.
Alisema askari huyo hivi karibuni amenunua gari jipya na anajulikana kwa vitendo vyake viovu.
“Hayo mliyoyaandika ni punje ya vitendo vya dhuluma vinavyofanywa na Polisi Tigo dhidi ya raia,” alisema mwananchi mwingine.
Askari hao wanalalamikiwa kwa kukamata malori ya mizigo, zikiwamo Fuso na Pick Up, pamoja na kukamata magari mengine yanayokiuka sheria za usalama barabarani wakati ni jukumu la askari wa usalama barabarani.
Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Senso, alisema wananchi wanapaswa kuwapongeza badala ya kuwalalamikia kwa sababu askari hao hawawezi kuona uhalifu halafu wasichukue hatua.
Lakini Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga aliwaonya askari hao kuwa jukumu lao ni kudhibiti ujambazi na siyo kuwavizia madereva wa bodaboda na bajaj barabarani.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment