Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Tuliwahi kusema katika safu hii kuwa, iwapo Watanzania
wangetakiwa kutoa maoni kuhusu taasisi ya umma ambayo wanadhani iliundwa
kulinda masilahi ya viongozi badala ya wananchi, bila shaka wengi
wangeinyooshea vidole Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi. Taasisi hiyo
imekuwapo kwa zaidi ya miongo mitatu sasa na kadiri siku zinavyopita,
ndivyo Watanzania wengi wanavyozidi kujiuliza maswali kuhusu nini hasa
nafasi ya sekretarieti hiyo katika mfumo wa utawala bora katika nchi
yetu.
Maswali ambayo yamekuwa yakiulizwa kuhusu taasisi
hiyo yanalenga kuhoji utendaji na ufanisi wa kazi zake tangu ilipoundwa
kisheria kwa lengo la kupiga vita ufisadi na kusimamia uadilifu miongoni
mwa viongozi wetu kama ilivyofafanuliwa katika Azimio la Arusha. Ni
vyema ikumbukwe kwamba sababu za wananchi kuhoji uhalali wa kuwapo
chombo hicho ni baada ya viongozi wa umma kujichimbia katika uozo na
ufisadi na kutupilia mbali maadili ya uongozi, huku viongozi wa
sekretarieti hiyo wakishuhudia pasipo kuchukua hatua. Sekretarieti hiyo
imekuwa ikionekana kama kiinimacho, kwani sheria iliyoiunda inaipa nguvu
kwa mkono wa kulia na wakati huohuo kuinyang’anya nguvu hizo kwa mkono
wa kushoto.
Ni kichekesho kwamba sheria inatoa uhuru kwa kila
mtu kwenda katika ofisi za sekretarieti hiyo kulipa ada kabla ya kukagua
nyaraka za viongozi waliotangaza mali zao ili kubaini kasoro, ukweli au
uongo uliomo.
Lakini sheria hiyo inamkataza mtu yeyote
aliyekagua nyaraka hizo kutoa kwa mtu yeyote taarifa kuhusu kitu
chochote alichokiona katika nyaraka hizo. Tafsiri pekee ya maelekezo
hayo ni kwamba wananchi wanakatazwa kujua mali walizochuma viongozi wao
kabla na baada ya kupewa uongozi. Vyombo vya habari ambavyo vinawajibika
kuufahamisha umma kuhusu mali walizonazo viongozi wao vimekuwa
vikikwazwa na “Sheria ya Maadili ya Viongozi”.
Sheria hiyo ndiyo imewapa kiburi viongozi kiasi
cha kukataa kutaja mali wanazomiliki. Pamoja na viongozi wengi
kuthibitika kutotangaza mali zao, Sekretarieti hiyo imekuwa kimya siyo
tu kwa kuona inasimamia sheria butu, bali pia kwa sababu baadhi ya
viongozi wa kitaifa pia wameshindwa au wamekataa kufanya hivyo. Baadhi
yao walitaja mali zao wakati wakiingia madarakani, lakini walishindwa au
walikataa kufanya hivyo walipomaliza muda wao wa uongozi.
Kwa kuwa huo ndiyo umekuwa utamaduni wa viongozi
wetu unaolindwa na sheria, Sekretarieti hiyo miaka yote imekuwa kama
“chui wa karatasi” au mbwa asiye na meno. Tumekuwa tukisema kwamba
Sekretarieti hiyo pia imechangia hali hiyo kwa kushindwa kuhakikisha
kwamba sheria iliyopo inarekebishwa, kwani kwa kukaa kimya imetoa mwanya
kwa wananchi kuendelea kuhoji uhalali wake.
Ndiyo maana tumetiwa moyo na hatua ya Sekretarieti
hiyo ya kuandaa warsha jijini Dar es Salaam juzi kupokea maoni ya
wananchi kuhusu sheria inayotarajiwa kutungwa kudhibiti mgongano wa
kimasilahi kwa viongozi na watumishi wa umma. Sheria hiyo imechelewa,
lakini italeta uwajibikaji na uzingatiaji wa maadili ya viongozi. Ni
matarajio yetu kwamba Sekretarieti itabadilishwa kimuundo ili iwe huru
na yenye madaraka kamili ya kufanya uamuzi pasipo kuingiliwa.
Ni matarajio yetu pia kwamba sheria hiyo itaweka
misingi na mifumo itakayowezesha kuwapo uwazi katika utendaji wa
Sekretarieti hiyo, ikiwa ni pamoja na kudhibiti viongozi wanaotumia
vibaya rasilimali na madaraka waliyopewa na umma.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment