Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com
Home » » JK KUKUTANA NA VIONGOZI WA VYAMA VYA SIASA KESHO

JK KUKUTANA NA VIONGOZI WA VYAMA VYA SIASA KESHO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Rais Jakaya Kikwete
Wenyeviti na Makatibu Wakuu wa vyama vya siasa vilivyopo katika Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), wamewasili mjini hapa kwa ajili ya kukutana na Rais Jakaya Kikwete kuzungumzia mustakabali wa mchakato wa Katiba mpya.
Kabla ya kukutana na Rais Kikwete Jumatatu ijayo, viongozi hao wa TCD leo watakutana kwa faragha ili kupata taarifa ya kamati waliyounda ambayo ilipewa jukumu la kuchambua na kutoa ushauri juu ya masuala watakayokwenda nayo katika kikao hicho na Rais.

Kamati iliyopewa jukumu hilo inaongozwa na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, huku wajumbe wakiwa ni Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba, Katibu Mkuu wa CCM, Abdurhaman Kinana na Katibu Mkuu wa Chadema, Wilbrod Slaa.

Mmoja wa viongozi wa vyama hivyo, aliliambia NIPASHE mjini hapa jana kwamba, kikao hicho cha viongozi wa TCD kina lengo la kuweka msimamo wa pamoja kabla ya kumkabili Rais Kikwete.

Kikao hicho cha TCD na Rais Kikwete kinafuatia kikao kama hicho kilichofanyika wiki mbili zilizopita mjini hapa, ambacho hata hivyo kilitawaliwa na usiri mkubwa.
Hata hivyo, baada ya kikao hicho, Mwenyekiti wa TCD, John Cheyo, alisema walizungumzia masuala makuu mawili, mchakato wa Katiba mpya na uchaguzi mkuu wa mwakani.

Cheyo alikataa kuingia kwa undani juu ya masuala hayo waliyojadili, lakini alisema baada ya mazungumzo walikubaliana kila upande ukatafakari waliyozungumza ili watakapokutana kwa mara ya pili waweze kutoka na maamuzi.

Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanaeleza kuwa kikao hicho huenda kikatoa muelekeo Juu ya Bunge Maalum la Katiba kama litasitishwa au litaendelea.

Bunge hilo lipo katika mkanganyiko kufuatia wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kususia, huku kukiwa na miito ya makundi mbalimbali ya jamii yakitoa wito wa kusitishwa kwa Bunge hilo.

Viongozi wengi wa TCD watakaokutana na Rais Kikwete ukiacha Cheyo, Lipumba, Kinana, Mbati na Slaaa ni Mwenyekiti wa TLP, Agostine Mrema, Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Philip Mangula, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu na Mwenyekiti wa UPDP, Fahami Dovutwa anayewakilishwa vyama visivyo na wabunge.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa