Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com
Home » » UGONJWA WA EBOLA NA JITIHADA ZA SERIKALI KATIKA KUPAMBANA NAO.

UGONJWA WA EBOLA NA JITIHADA ZA SERIKALI KATIKA KUPAMBANA NAO.



Na Benedict Liwenga, Maelezo-DSM.

 
Ebola ni ugonjwa unaosababishwa na virusi vya homa ya hemoraji ikimaanisha ugonjwa wa kumwagika damu bila kuganda (Viral Haemorrhagic Fevers).
 
Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali, ugonjwa huu ni hatari na unasababishwa na kirusi kiitwacho ebola kwani kirusi hicho ni moja kati ya familia ya virusi watatu toka katika familia ya filoviridiae.
 
Kuna aina tano za kirusi cha ebola ambao ni bundibugyo ebolavirus (BDBV), Zaire Ebolavirus (EBOV), Reston Ebolavirus (RESTV), Sudan Ebolavirus (SUDV) na Tai Forest Ebolavirus (TAFV).
 
Ni ugongwa unaoua kwa kasi na tafiti zinaonyesha kwamba katika orodha ya watu 10 walioambukizwa na virusi vya ugonjwa huo, basi wastani kati ya watano au tisa hufariki.
 
Aina hizo tatu za virusi, yaani BDBV, EBOV na RESTV, ndiyo inayongoza kwa kusababisha mlipuko wa ugonjwa huo Barani Afrika wakati aina nyingine za virusi hao wanapatikana katika nchi za Asia, yaani Ufilipino na Thailand.
 
Taarifa mbalimbali zinaonyesha kuwa kwa mara ya kwanza ugonjwa huu uliripotiwa kutokea mnamo mwaka 1976 katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na taarifa zinaeleza kuwa hatari ya mgojwa kupoteza maisha ni asilimia 90.
 
Tafiti zinaonyesha kuwa, kuwa Popo wanaopenda kula matunda wanaeneza ugonjwa huo bila wao kuaathirika na katika jamii yetu ugonjwa huo huweza kuambukizwa kutoka mtu mmoja mwenye maambukizi kwenda kwa mwingine baada ya kugusana na damu au maji maji kupitia michubuko au majeraha yaliyopo juu ya ngozi.
 
Pia watu ambao wako katika hatari ya kupata ugonjwa huo ni jamii inayoishi karibu na jamii ya wanyama ambao mara nyingi ni Nyani, Sokwe, Tumbili pamoja na Popo.
 
Licha ya watu walio na maambukizi ya ugonjwa huo kapata nafuu, lakini bado wanaweza kuwaambukiza wengine kwa njia mbalimbali, mfano kwa njia ya kujamiana.
 
Wataalam wanaamini kuwa virusi vya ugonjwa huo huwa havienei kwa njia ya hewa bali kwa mtu kugusana na majimaji ya mwili, kama vile matapishi, mate, jasho, machozi, ama manii au shahawa ya mtu aliyeathirika na ugonjwa huo.
 
Kwa upande mwingine hata Madaktari na wauguzi, wanaowatunza wagonjwa wa ebola, watu wenye uhusiano wa karibu na mtu aliyeambukizwa, watu wanaogusa maiti ya mtu mwenye virusi hivyo wapo katika hatari ya kuambukizwa virusi vya Ebola.
 
Ishara na dalili muhimu ya ugonjwa huu ni hali ya kutokwa na damu katika sehemu tofauti za mwili kama vile katika ufizi, pua, katika njia ya haja, lakini kabla mgonjwa hajafikia daraja hilo, kwanza mtu huwa na homa kali, viwango vya joto vya mwili hupanda sana, kisha anaweza kuwa anajisikia kutapika, na hata kutapika kwenyewe, kuharisha, na pia kuwa mnyonge huku viungo vyake vikiwa na maumivu.
 
Ili kuweza kutambua mtu ama mgonjwa ameambukizwa na ugonjwa huo, njia ya pekee ya kuthibitisha hilo ni kupitia vipimo vya maabara.
 
Huduma ya kwanza ambayo mgonjwa wa Ebola anaweza kupewa kwanza kabisa ni vema kumfikisha mgonjwa huyo katika Kituo cha Afya haraka kwa haraka kwani kuvigundua virusi vya ebola kunahitaji maabara ambayo ina uwezo wa kutosha.
 
Katika kuzingatia matibabu ya mgonjwa wa Ebola jambo la kwanza ni kuchunguza na kuhakikisha kwamba mtu ana virusi hivyo, pili ni kumtenga na watu wengine ili yeye mwenyewe asidhurike zaidi na asiwadhuru wengine na katika kufanya hivyo haimaanishi kwamba mgonjwa huyo anatengwa kwa kunyanyapaliwa, lengo ni kuepusha maambukizi yasiendelee kwa watu wengine ambao hawana ugonjwa huo.
 
Taarifa nyingi kuhusiana na ugonjwa huu zinasema kuwa mpaka sasa hakuna dawa maalumu ambayo inatumika kuwatibu wale walio na virusi vya ugonjwa huo kwani dawa zilizoko sasa ni zile ambazo ziko ngazi ya majaribio ili kuweza kuona namna gani zinaweza kukabiliana na ugonjwa huo.
Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitoa kauli ya kwamba hatari ya kuambukizwa kwa ugonjwa huo kwa njia ya safari za ndege ni chini sana, hata hivyo, watu hushauriwa kuwa waangalifu kuhusiana na hali yao na afya na ile ya wasafiri wengine.
 
Tahadhari ni bora kuliko kinga, ili kujihadhari na ugonjwa huo endapo utakuwa umeonekana kuingia nchini mwetu hatunabudi kujiepusha kugusana na majimaji yote yanayotoka kwenye mwili wa mtu ambaye atakuwa ameathirika na ugonjwa huo, na pia ni vema tukatumia dawa za kuuwa vijidudu katika choo, katika matapishi, katika mate na majimaji yoyote ya mgonjwa.
 
Bila shaka ugonjwa wa Ebola unaweza kuzuilika endapo tu sote tutachukua hatua, hivyo ni muhimu kwa kila mmoja kuwajibika katika hili na kutoa taarifa mapema kwa Viongozi wa Serikali na wa huduma za Afya katika ngazi zote pale anapotokea mtu mwenye dalili za ugonjwa huo.
 
Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizochukua tahadhadhari kubwa na mapema ingawa hakuna kesi yoyote iliyoripotiwa juu ya uwepo wa ugonjwa huo hapa nchini.
 
Kwa kuanzisha mafunzo maalum kwa Kikosi Kazi yenye lengo la kudhibiti ugonjwa wa Ebola, Serikali imetoa mafunzo kwa mamia ya Watumishi wa Afya watakaokwenda kuhudumia abiria wanaoingia na kutoka nje ya nchi.
 
Sambamba na hilo, Serikali imeweza kufanikisha kuingiza nchini sehemu ya vifaa vya kubaini hatua za awali za ugonjwa wa Ebola kwa kupima hali ya joto la mwili kwa wasafiri kutoka nje nchi wanaotumia viwanja vya ndege  vilivyokuwa vimeagizwa na Serikali vilikwisha wasili jijini Dar es salaam.
 
Vifaa hivyo vinavyohusisha kamera zenye uwezo wa kubaini joto la mwili wa msafiri kwa umbali wa mita 100 bila  kumgusa muhusika ambayo viliagizwa kutoka nchini Afrika ya Kusini.
 
Wakati wa siku ya kukabidhi vifaa hivyo kwa Wataalam wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Kebwe Steven Kebwe alisema kuwa kuwasili kwa vifaa hivyo ni moja ya juhudi za Serikali za kuhakikisha kuwa wananchi wanakuwa salama kwa kuuzuia ugonjwa huo kuingia nchini.
 
Aidha alisema kuwa vifaa hivyo vitapelekwa katika maeneo ya Viwanja vya ndege na maeneo yanayotumiwa na raia wa kigeni kuingia nchini vikiwemo vya Dar es salaam, Zanzibar, Kilimanjaro,Mbeya na Mwanza.
 
Licha ya kuwepo kwa juhudi hizo, bado Serikali inaendelea na mpango wa kuagiza vifaa zaidi vya kuwezesha shughuli ya upimaji wa afya kwa wasafiri wanaotembea yaani vifaa vya(Scanners) vitakavyowezesha kubaini afya za wasafiri wengi zaidi kwa wakati mmoja.
 
Aidha, aliwataka wataalam wa afya kufanya kazi zao kwa weledi mkubwa kwa kuhakikisha wanawapima abiria wote wanaotoka nje ya nchi bila kujali hadhi walizonazo ili kuweza kubaini kama wana maabukizi au dalili zozote za ugonjwa wa Ebola.
 
“Nataka mfanye kazi yenu kwa kuzingatia weledi wa taaluma yenu na kwa kuzingatia yale mliyojifunza, mvitumie vifaa hivi kupima kila abiria ili kubaini joto lake bila kujali cheo wala hadhi yake maana janga hili ni kubwa” Alisema Dkt. Kebwe.
 
Akizungumzia kuhusu matunzo ya vifaa hivyo, aliwataka wataalam hao kuhakikisha wanavitunza vifaa hivyo ili viweze kudumu na kutimiza malengo yaliyokusudiwa ya kuwasaidia wananchi kutokana na vifaa hivyo kugharimu fedha nyingi.
 
Katika hatua nyingine Mh. Kebwe alifafanua kuwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inaendelea na shughuli ya utoaji wa Elimu ya Afya kuhusu ugonjwa wa huo ili kuwawezesha wananchi kuchukua tahadhari na kuzielewa dalili za ugonjwa huo na namna ya kujingika endapo utagundulika nchini.
 
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Bohari ya Dawa nchini (MSD), Bw. Cosmas Mwaifwani ambaye Ofisi yake ilihusika katika uagizaji wa vifaa hivyo alisema kuwa mahitaji ya vifaa hivyo kwa sasa yameongezeka kutokana na umuhimu wake na jinsi vinavyofanya kazi kwa ufanisi mkubwa.
 
Alisema kuwa upimaji kwa kutumia vifaa hivyo unatumia teknolojia ya kubaini mionzi ya joto kutoka katika mwili wa binadamu pindi vinapoelekezwa katika maeneo ya macho na masikio ya mwili wa binadamu.
 
“Vifaa hivi vinauwezo wa kutunza picha na kumbukumbu za msafiri, muda, joto la msafiri na tarehe aliyoingia nchini na vifaa hivi vina uwezo wa kupata takwimu kutoka kwenye hali ya majimaji au jasho la Binadamu pindi kinapoelekezwa kwake”, alisema Mwaifwani.
 
Mwaifwani aliongeza kuwa MSD inaendelea kuimarisha uwezo wake kwa kuongeza vifaa zaidi kutoka nchi za Ubelgiji na China huku akisisitiza kuwa Bohari hiyo imejiandaa kukabiliana na ugonjwa wa Ebola kwa kujenga uwezo wa kuwa na dawa za kutibu hali ya magonjwa yanayoambatana na homa hiyo.
 
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Viwanja vya Ndege nchini, Bw. Moses Malaki akizungumza kwa niaba ya Viwanja vya ndege nchini alielezea hali hiyo ya upatikanaji wa vifaa  katika maeneo hayo kuwa itaongeza ufanisi wa uchunguzi wa afya kwa wasafiri na kuondoa usumbufu kutokana na uwezo wa vifaa hivyo kumpima msafiri akiwa mbali.
 
Pamoja na juhudi za serikali katika kuzuia usiingie nchini ugonjwa huo na hali ya kukaa kwa tahadhari, jamii nchini hainabudi kuzingatia elimu itolewayo na wataalam wa afya juu ya namna ya kujikinga ili kuweza kuudhibiti vema ugonjwa huo kwani mpaka hivi sasa tayari Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa zaidi ya watu 560 wamepoteza maisha nchini Sierra Leone na wengine zaidi 2,600 wamefariki dunia huko Afrika ya Magharibi.
 
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa