Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Ni miezi kadhaa sasa gazeti hili limekuwa likiwahoji baadhi ya wajasiriamali wadogo na kuchapisha habari zao katika jarida la uchumi kila Alhamisi.
Katika kipindi chote hicho, idadi kubwa ya wajasiriamali wamekuwa wakimtaja mfanyabiashara mahiri nchini, Said Salim Bakhresa kuwa mtu wanayevutiwa naye na kutamani kufuata nyayo zake.
Mwingine aliyewahi kutajwa ni mwenyekiti wa kampuni za IPP, Reginald Mengi. Inatia moyo kuwa wajasiriamali wengi wana watu wanaowachukulia kama kioo, tena wakiwa ni wazawa. Wajasiriamali wengi wana ndoto ya kuwa kama wao ili nao siku moja waje kuwa na mafanikio makubwa kibiashara.
Wajasiriamali wa Tanzania na wananchi wengine kwa jumla, wanatamani kujua safari ya mafanikio ya mashujaa wao mbalimbali wakiwamo wafanyabiashara, lakini kwa mazingira yalivyo nchini kujua hayo ni suala gumu.
Hii ni kwa sababu ya pengine utamaduni, mazoea au sababu binafsi kuwa baadhi ya watu waliofanikiwa, aghalabu hawako tayari kuelezea simulizi za safari ya mafanikio yao au kwa Kiingereza success stories.
Hii ni tofauti na ilivyo kwa wenzetu, hasa wa nchi za Ulaya na Marekani. Katika nchi hizo, watu wengi wanaofanikiwa katika nyanja mbalimbali, hawaoni shida kutoka mbele ya watu na kuelezea baadhi ya mambo yaliyochangia mafanikio yao. Wapo wanaojitokeza na kuzungumza katika mikutano maalumu ya hadhara kwa lengo la kuwapa hamasa wengine, lakini pia wapo wanaoandika machapisho, hususan vitabu.
Mtu kama Robert Kiyosaki ni mjasiriamali aliyefanikiwa nchini Marekani na hatimaye akageuka kuwa mwalimu na mtunzi wa kuhamasisha jamii kujihusisha na shughuli za ujasiriamali.
Maisha yake tangu akiwa mdogo, mitazamo na falsafa zake kuhusu maisha, biashara na uwekezaji kwa jumla, ameviweka katika machapisho yake na kuwa chachu kwa wasomaji wengi wanaotamani kubadili maisha yao.
Hapa kwetu wajasiriamali kama hawa wanaojitokeza katika gazeti na wengineo, wanahitaji kuelimishwa, kupewa hamasa ili hatimaye ndoto zao ziwe kweli. Vitabu vya ujasiriamali vinavyotungwa na waandishi, vingi vimejaa nadharia, havina ‘success stories’ ya kuwavutia watu wakahamasika katika shughuli za ujasiriamali.
Natoa rai kwa wafanyabiashara wakubwa hapa nchini na hata watu wengine katika kada tofauti waliofanikiwa kuzungumza, kuandika au hata kuwa tayari kuhojiwa kwa lengo la kuhamasisha jamii.
Asiye na kipaji cha kuandika, azungumze katika mikutano au majukwaa maalumu. Asiyeweza kuzungumza mbele ya kadamnasi,walau atafute mtu washirikiane kuandika wasifu (biography) au tawasifu ( autobiography).
Kwa mfano, wajasiriamali tunaozungumza nao kila siku na kumtaja mzee Bakhresa wangetamani kumsoma au kumsikiliza akisimulia safari yake kutoka kumiliki mgahawa mdogo hadi kuwa na himaya kubwa ya biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki, Kati na Kusini. Pia Watanzania wangependa kujua safari ya Mengi kuanzia alipotoka hadi kujenga mtandao mkubwa wa vyombo vya habari Afrika Mashariki.
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment