Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
ameshtushwa na kusononeshwa sana na taarifa za kifo cha Rais wa Jamhuri
ya Zambia, Mheshimiwa Michael Chilufya Sata (pichani) ambacho
kimetokea jana, Jumanne, Oktoba 28, 2014 kwenye Hospitali ya King
Edward VII, London, Uingereza, ambako alikuwa anatibiwa akiwa na umri wa
miaka 77.
Katika
salamu ambazo amempelekea Makamu wa Rais wa Zambia, Mheshimiwa Dkt. Guy
Scott kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Rais
Kikwete amesema:
“Nimepokea
kwa mshtuko mkubwa na huzuni nyingi, habari za kusikitisha za kifo cha
Mheshimiwa Michael Chilufya Sata, Rais wa Jamhuri ya Zambia. Kwa niaba
ya Serikali na Wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na hakika,
kwa niaba yangu mwenyewe, napenda kukutumia wewe Mheshimiwa salamu za
rambirambi za dhati ya moyo wangu, na kupitia kwako familia ya wafiwa na
ndugu wa Hayati Rais Sata pamoja na Serikali na ndugu zetu wananchi
wote wa Zambia kufuatia msiba huu wa ghafla.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Hayati
Sata atakumbukwa daima kama mmoja wa viongozi wa mfano wa kuigwa katika
Afrika. Katika kipindi chake kifupi cha uongozi wa juu wa Zambia,
alifanikiwa kuleta mageuzi makubwa katika maisha ya wananchi wengi wa
Zambia. Atakumbukwa pia kwa imani yake isiyoyumba ya kupigania uhuru,
haki na usawa, sifa ambazo zilimfanya kiongozi mpendwa ndani na nje ya
mipaka ya Jamhuri ya Zambia.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Hivyo,
huyu ni kiongozi ambaye siyo tu atakumbwa na wananchi wa Zambia lakini
atakumbukwa na sisi sote wenzake na watoto wote wa Afrika.”
“Katika
kipindi hiki kigumu cha majonzi na huzuni, tunaungana nanyi kuomboleza
na kumwomba Mwenyezi Mungu awape nguvu na subira wana familia ya wafiwa,
jamaa na ndugu zetu wote wa Zambia ili waweze kuhimili machungu ya
kipindi hiki cha msiba mkubwa. Aidha, tuko pamoja nanyi katika kumwomba
Mwenyezi Mungu aiweke pema roho ya Marehemu Michael Chilufya Sata.”
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
29 Oktoba,2014.
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment