Home » » WAFUASI ‘WAFUNIKA’ JANGWANI

WAFUASI ‘WAFUNIKA’ JANGWANI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

Maelfu ya wanachama na mashabiki wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), jana walifurika kushuhudia tukio la kihistoria la kusainiwa kwa makubaliano ya kushirikiana kwenye Viwanja vya Jangwani.
Wakiwa wamevalia nguo zenye rangi mbalimbali zinazosadifu alama na utambulisho wa vyama vyao, wafuasi wa vyama vya CUF, Chadema, NLD na NCCR-Mageuzi walijumuika katika viwanja hivyo pasipo kujali jua kali lililokuwa likiwaka wakati wa mchana.
Tofauti na mikutano mikubwa ya siasa ambayo wengi walizoea kuona bendera za chama husika pekee, katika mkutano huo, bendera za vyama hivyo zilitawala kuonyesha kuzaliwa kwa kitu kipya.
Hata hivyo, bendera za Chadema ndizo zilizotawala katika mkutano huo zikifuatiwa na zile za CUF na NCCR huku NLD kikiwa na bendera chache zaidi.
Vikundi mbalimbali vilianza kuingia uwanjani saa 7.45 mchana kwa njia mbalimbali ikiwamo malori na maandamano madogomadogo kutokea Kariakoo na Kigogo.
Msafara wa viongozi
Ilipofika saa tisa alasiri, msafara wa viongozi wa Ukawa ulianza kuingia uwanjani ukitokea katika Barabara ya Morogoro ukiongozwa na king’ora kilichofuatiwa na gari la usalama la Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad. Msururu huo wa magari ulifuatiwa wa viongozi wa Chadema, Freeman Mbowe, NCCR-Mageuzi, James Mbatia na viongozi wengine.
Wakati wanaingia, wafuasi walikuwa wamejipanga mistari wakiwapungia mikono bila kuchoka na viongozi hao kuitikia. Msafara huo pia uliambatana na mbwembwe za walinzi kuning’inia katika gari la Mbowe.
Mbwa kunusa viti vya Jukwaa Kuu
Katika kile kilichoonekana kama ni kuhakikisha usalama, kitengo cha ulinzi cha Ukawa kilikuwa na mbwa wawili waliotumika ‘kukagua’ viti vya viongozi wakuu. Baada ya kumaliza kazi yao, mbwa hao walioonekana kufunzwa vizuri, walirudishwa katika gari dogo. Pia ulinzi uliimarishwa katika sehemu kubwa ya viwanja hivyo kwani pia walikuwapo polisi pamoja na walinzi wa vyama husika ambao asilimia kubwa walivalia mavazi meusi.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu ndiye aliyeanza kuzungumza katika hadhira hiyo baada ya kupanda jukwaa kuu na kuuliza ngapi? Alijibiwa na umati huo... “tatuuuuu”. Pia aliendelea kuhamasisha watu kwa kaulimbiu ya “Ukawa?” na wafuasi wakijibu “Tumaini letu”.
Mwalimu aliendelea hivyo hivyo kwa salamu za vyama vyote akianza na ile ya CUF ya “Haki” huku wananchi wakijibu kwa sauti kubwa ya “sawa kwa wote.” Aliendelea hivyo kwa Chadema kwa salamu ya “People’s….” na wananchi wakijibu “Power” kwa sauti kubwa.
Chanzo;Mwananchi

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa