Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam
Saidi Mecki Sadiki akifuangua kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Dar
es salaam (RCC) leo jijini Dar es salaam.Kushoto ni Katibu Tawala wa mkoa wa Dar es salaam Bi. Theresia Mmbando.
============== ======== =========
Aron Msigwa –MAELEZO.
Jiji la Dar es salaam linaangalia upya utaratibu wa kuwaondoa ombaomba na wafanyabiashara ndogondogo(wamachinga) katika maeneo yasiyoruhusiwa katika jiji la
Dar es salaam kufuatia sheria na hatua zinazochukuliwa ikiwemo kuwarudisha ombaomba hao
katika mikoa wanayotoka kutokuzaa matunda na kuwa endelevu kufuatia wengi wao kurudi katika maeneo ya awali kila wanapoondolewa.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Said Mecki Sadiki
wakati akifungua kikao cha wajumbe wa Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Dar es
salaam (RCC) kilichofanyika leo jijini Dar es salaam kujadili masuala
mbalimbali ya mendeleo katika jiji la Dar es salaam.
Amesema kuwa kuendelea kuwepo
kwa wafanyabiashara hao katika maeneo yasiyo rasmi ni moja ya changamoto
inayolikabili jiji la Dar es salaam kutokana na biashara wanazozifanya
kuchangia kuzuia maeneo ya barabara ya waenda kwa miguu, kusababisha uchafuzi
wa mazingira,kusabisha msongamano wa magari kwa baadhi yao kuweka bidhaa barabarani.
Amesema kutokana na hali hiyo baadhi ya wafanyabiashara walio na
biashara rasmi ambao hulipa kodi za
Serikali wamekuwa wakilamikia hali ya ukwepaji
wa kodi inayofanywa na wafanyabiashara hao.
Bw. Sadiki amesema mpango wa mkoa wa sasa ni kuendelea kuwatumia
wafanyabiashara hao kama fursa ya mtaji
wa rasilimali watu ambayo itatumika kama chanzo cha mapato katika kuleta
maendeleo ya mkoa.
Amesema watendaji na viongozi wa halmashauri za mkoa wa Dar es salaam
wanalojukumu la kuweka mazingira mazuri ya kufanya shughuli zao na kuwatumia
katika shughuli za uzalishaji kwa utaratibu mzuri utakaowekwa ili waendelee
kunufaika na shughuli wanazofanya.
Akizungumzia kuhusu uboreshaji wa huduma za jamii zikiwemo za Maji,
Elimu na Afya katika jiji la Dar es salaam amesema kuwa Serikali inaendelea kuzijengea
uwezo shule kwa kuongeza majengo ya madarasa, maabara na kuhakikisha kuwa
wanafunzi wote wanaofaulu elimu ya msingi wanapata fursa ya kuendelea na masomo
ya Sekondari.
Kuhusu huduma za afya amesema kuwa mkoa unaendelea na maandalizi ya
ujenzi wa jengo la ghorofa nane, eneo la Magomeni katika manispaa ya Ilala
litakalotumika kutolea huduma ya Afya ya Mama na Mtoto na kuwa na uwezo wa
kulaza wagonjwa 500.
“ Sasa tuko kwenye maandalizi ya
ujenzi wa jengo maalum la kutolea huduma ya Afya ya Mama na Mtoto katika jiji
la Dar es salaam litakalogharimu zaidi ya shilingi bilioni ishirini na moja,
tayari benki ya Tanzania Investment Bank imeshakubali kutoa mkopo kwa ajili ya
jengo hilo” Amesisitiza.
Aidha, katika hatua nyingine Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam ametoa
ufafanuzi kuhusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika nchi nzima Desemba 14 mwaka huu na kueleza kuwa baadhi
ya maeneo ya jiji la Dar es salaam ambayo uchaguzi huo uliahirishwa kutokana na
sababu mbalimbali zikiwemo vurugu, uchaguzi huo utarudiwa ndani ya siku saba.
Ameeleza kuwa katika mkoa wa Dar es salaam uchaguzi huo ulitarajiwa
kufanyika kwenye mitaa 561 lakini kutokana na changamoto mbalimbali ulifanyika
kwenye mitaa 491 na kuahirishwa kwenye kata 70.
Amelitaka jeshi la Polisi kuhakikisha kuwa linaimarisha ulinzi na
usalama wakati wa marudio ya uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika ndani ya siku
7 katika mitaa yote ambayo uchaguzi uliahirishwa .
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment