Home » » IKULU YAELEZA HATMA KIPORO CHA MUHONGO

IKULU YAELEZA HATMA KIPORO CHA MUHONGO

Yasema JK atatimiza ahadi hivi karibuni
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Salvatory Rweyemamu.
 
Wakati makundi mbalimbali katika jamii yakishinikiza Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo, awajibishwe, kutokana na kuhusishwa na kashfa ya kampuni ya IPTL ya uchotwaji wa zaidi ya Sh. bilioni 300 kifisadi katika akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Ikulu imesema Rais Jakaya Kikwete atatoa maamuzi kuhusu waziri huyo hivi karibuni.
Maamuzi ya Rais Kikwete yanatarajiwa kutolewa kufuatia uchunguzi uliofanywa na vyombo mbalimbali, ikiwamo Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru) dhidi ya Prof. Muhongo, ili kujiridhisha kama anahusika katika kashfa hiyo au la, kabla ya kuchukuliwa hatua zinazostahiki.

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Salvatory Rweyemamu, alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa maamuzi juu ya kuhusu Prof. Muhongo kuhusiana na uchunguzi unaofanywa dhidi yake, ni ahadi iliyotolewa Rais Kikwete, ambayo kama ilivyo kawaida yake, lazima ataitimiza.

Alisema Rais Kikwete alipotamka kwamba, amemuweka kiporo Prof. Muhongo kwa siku mbili hadi tatu kwa kuwa kuna uchunguzi dhidi yake alioagiza ufanyike, alimaanisha kuwa atatoa maamuzi hayo hivi karibuni.

“Kwa hiyo, Mheshimiwa Rais atatoa maamuzi (kuhusu Prof. Muhongo) hivi karibuni. Anachoahidi Rais atatimiza,” alisema Rweyemamu alipokuwa akijibu maswali ya waandishi wa habari, ofisini kwake, Ikulu, jijini Dar es Salaam jana.

Akijibu swali sababu za Prof. Muhongo kutowekwa kando kama ilivyofanyika kwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Eliakim Maswi, ili kupisha uchunguzi unaofanyika dhidi yake, Rweyemamu alisema Prof. Muhongo bado ni waziri wa serikali na kuhoji: “Tatizo ni nini?”.

“Bwana Maswi yeye ni mtumishi wa umma, mtumishi wa serikali, civil savant. Kuna sheria tofauti za civil savant na wanasiasa. Huyu mmoja ni mwanasiasa, ni kiongozi wa umma, huyu mwingine ni kama mimi. Mimi ni mtumishi wa serikali. Taratibu zangu za kuniwajibisha zitakuwa tofauti na za waziri,” alisema Rweyemamu.

Aliongeza: “Na mimi ningeomba kitu kimoja hivi. Kwanini mnafikiri suala la Prof. Muhongo ni suala la kufa na kupona? Kuingia kwenye shughuli za watu wengine mtakwenda mbali sana.”

Aidha, Rweyemamu alitaka aelezwe na waandishi namna Prof. Muhongo anavyohusika katika kashfa hiyo na kuelezwa kuwa kunatokana na maazimio nane yaliyopitishwa na Bunge, Novemba 29, mwaka jana.

Maswali hayo yaliulizwa na waandishi kufuatia siku tatu zilizoahidiwa na Rais Kikwete za kumuweka kiporo Prof. Muhongo, ili kuruhusu uchunguzi dhidi yake ufanyike, kabla ya kuchukuliwa hatua, kupita ambazo kufikia leo zimefika siku 29, huku kinachoendelea kuhusiana na suala hilo kikibaki kuwa kitendawili.

Kuhusika kwa Prof. Muhongo katika kashfa hiyo, kulibainishwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kupitia taarifa yake iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe, bungeni Novemba 26, mwaka jana.

Kufuatia taarifa hiyo ya PAC, Bunge kwa kauli moja lilipitisha maazimio nane, moja likiitaka mamlaka ya uteuzi kutengua uteuzi wa viongozi kadhaa wa serikali, akiwamo Prof. Muhongo.

Wengine, ambao Bunge liliazimia wawajibishwe kutokana na kuhusishwa katika kashfa hiyo, ni Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Maswi na aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka.

Wamo pia wenyeviti wa kamati tatu za Bunge; Victor Mwambalaswa (Nishati na Madini), William Ngeleja (Katiba, Sheria na Utawala) na Andrew Chenge (Bajeti).

Katika maazimio hayo, Bunge lilishauri hatua za haraka zichukuliwe na kamati husika za Bunge kabla ya kuanza kwa mkutano wa 18 wa Bunge unaotarajiwa kuanza Januari 27, mwaka huu.

Hata hivyo, Desemba 22, mwaka huu, Rais Kikwete akilihutubia taifa kupitia wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam alisema amemuweka kiporo Prof. Muhongo kwa siku mbili hadi tatu kwa kuwa kuna uchunguzi dhidi yake alioagiza ufanyike.

Rais Kikwete alisema iwapo angepata majibu ndani ya siku hizo, angefanya uamuzi dhidi ya Prof. Muhongo.

Alisema miongoni mwa vyombo vya serikali, ambavyo wakati huo vilikuwa vikiendelea na uchunguzi dhidi ya Prof. Muhongo, ni pamoja na tume hiyo kwa ajili ya kupata maamuzi kwa misingi ya haki.

Hata hivyo, tangu wakati huo, kufikia leo zimekwishapita siku 29 bila Rais Kikwete kutangaza hatma ya Prof. Muhongo kama anatimuliwa au kubaki katika nafasi yake serikalini, huku giza nene likiwa linaendelea kugubika suala hilo.

Hali hiyo ilichangiwa pia na ukimya na kigugumizi kizito cha kushindwa kuzungumzia suala hilo kilichokuwa kimeisibu Ikulu, tangu siku zilizoahidiwa na Rais Kikwete kulishughulikia kupita na kuzidi kuongezeka.

Katika hotuba yake kupitia wazee, Rais Kikwete aliagiza kuchukuliwa hatua kwa Maswi ili kupisha uchunguzi wa tuhuma kuhusu ushiriki wake kwenye kashfa hiyo.

Siku iliyofuata, Balozi Sefue alimweka ‘kando’ Maswi na kumteua Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Ngosi Mwihava, kukaimu nafasi hiyo hadi uchunguzi utakapokamilika.

Kutokana na kuchelewa kutekelezwa kwa maazimio ya Bunge yaliyotaka viongozi hao kuwajibishwa, Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), umeahidi kuwasilisha hoja bungeni ya kupiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu na kufanya maandamano nchi nzima.

Mpaka sasa, viongozi watatu wamekumbwa na dhoruba inayotokana na kashfa hiyo baada ya kujiuzulu kwa aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema, kung’olewa kwa Prof. Tibaijuka na kuwekwa kando kwa Maswi.

Makundi mbalimbali katika jamii, wakiwamo wanasiasa, wabunge, asasi zisizokuwa za kiserikali, viongozi wa dini, wamekuwa wakishinikiza kutaka Prof. Muhongo awajibishwe..

Mbunge wa Kahama (CCM), James Lembeli, jana alikaririwa akisema kuendelea kwa Prof. Muhongo kuachwa kwenye wadhifa huo kunachochea hasira za wananchi.

Aidha, hadi sasa watumishi watano wa serikali, ambao Lembeli na Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR), David Kafulila alieyeibuka kasfha hiyo Bungeni, wamewaita kuwa ni “vidagaa”, wamefikishwa kizimbani kwa tuhuma za kupokea mgawo wa fedha za Escrow.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia kamati kuu yake (CC) kimeagiza watu wote waliohusika na kashfa ya Tegeta Escrow kuchukuliwa hatua.



KAFULILA ALONGA
Akizungumzia kauli hiyo ya Ikulu jana, Kafulila, alisema Prof. Muhongo alishindwa kutekeleza sheria ya fedha ya mwaka 2012 inayomtaka athibitishe uhamishaji wa hisa.

Alisema hali hiyo ilisababisha mmiliki wa kampuni ya PAP, Singh Seth kuinunua IPTL kwa kutumia nyaraka za kughushi, kama ilivyoeleza ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kutumia uhalali huo wa kughushi kupora mabilioni ya fedha za Tegeta Escrow kwa ushirika wake na vigogo wa serikali.

“Sasa Ikulu kuendelea kumlinda yeye na wenzake ni sawa na kusema Ikulu hii siyo ya umma na inaweza kusababisha uasi wa kijamii. Muhongo alifanya makosa ya kifisadi kama alivyofanya Mramba ambaye sasa yupo mahakamani kwa kusababisha hasara ya bilioni 11. muhongo na wenzake wamesababisha hasara ya zaidi ya bilioni 300,” alisema Kafulila.

Aliongeza: “Ikulu kutochukua hatua inaonyesha wazi imepoteza imani ya umma na inaendesha nchi kimabavu wananchi wapende wasipende. Hii ndiyo jeuri halisi ya kifisadi serikali kuongozwa na mawaziri viporo.”

WAITUMIA IKULU KUTAPELI
Awali, Rweyemamu alizungumzia utapeli unaofanywa na baadhi ya watu, ambao wamekuwa wakijipatia mamilioni ya shilingi kwa kutumia jina la Ikulu.
Alisema watu hao wamekuwa wakidanganya kuwa ili kupata kazi Ikulu unatakiwa utoe Sh. milioni 17.

Kutokana na hali hiyo, aliutaka umma kujua kwamba, nafasi za kazi au vyeo vya Ikulu na serikalini kwa jumla havitolewi kwa fedha.

JK HAJAVUNJA SHERIA KURA MAONI
Pia alisema madai yaliyotolewa na baadhi ya watu kwamba, alivunja sheria hiyo, ambayo inataka katika muda wa wiki mbili baada ya Bunge Maalumu la Katiba (BMK) kuvunjwa, atoe maelekezo ya kufanyika kura ya maoni hayana ukweli wowote.

Alisema baada ya BMK kuvunjwa, Rais Kikwete alitoa maelekezo kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) kufanya maandalizi ya kura ya maoni na kwa hiyo, alitimiza matakwa yote ya sheria ya kura ya maoni.

MISAMAHA YA KODI
Pia alisema madai ya kuituhumu serikali kwamba, inapendelea kuwapo misamaha ya kodi, ambayo yamekuwa yakitolewa yakitolewa na baadhi ya wabunge na kuripotiwa na baadhi ya wavyombo vya habari, hayana ukweli.

Alisema daima serikali haiwezi kupendelea kuona misamaha ya kodi inakuwapo na kwamba, kama ni lawama zinapaswa kuelekezwa kwa wabunge, kwani katika mikutano ya 16 na 17 ya Bunge, serikali iliwahi kupeleka bungeni muswada uliotaka misamaha ya kodi ifutwe, lakini wabunge wakakataa kuupitisha.

Pia alisema muda ukifika nakala za rasimu ya katiba inayopendekezwa zitapatikana ili kuwapa wananchi fursa ya kuisoma na kuielewa kabla ya kupigia kura ya ama kuikubali au kuikataa.

KUHUSU KAULI YA WARIOBA
Kuhusu kauli ya aliyekuwa Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, inayotabiri kukwama kwa kura ya maoni kufanyika Aprili, mwaka huu, kutokana na maandalizi hafifu, Rweyemamu alisema serikali haiwezi kumzuia mtu yeyote kusema analotaka.

Alisema mchakato wa kufanyika kura ya maoni unakwenda kwa hatua na kwamba, hakuna wasiwasi wowote juu ya kufanyika katika muda uliopangwa na serikali.
CHANZO: NIPASHE
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa