WAKATI mgomo wa wafanyakazi wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) ukiingia katika siku ya tano leo, menejimenti ya mamlaka hiyo imewashitaki Mahakama ya Kazi wafanyakazi wote waliogoma, kushinikiza kulipwa mishahara yao ya miezi mitano.
Mamlaka hiyo imewashitaki wafanyakazi hao kwa madai kuwa mgomo huo ni batili.
Wafanyakazi hao, wamegoma ili kushinikiza malipo yao hayo, pamoja na kusikilizwa madai yao mengine, ikiwa ni pamoja na kujua hatma ya uendeshwaji wa mamlaka hiyo.
Akizungumza na HabariLeo jana, Kaimu Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli nchini (TRAWU), Yassin Mleke alisema wamepewa hati ya kuitwa mahakamani kutokana na kufanya mgomo unaodaiwa ni batili.
Alisema menejimenti hiyo inadai mgomo huo si wa kisheria , hivyo inaomba Mahakama kutoa amri kwa wafanyakazi hao kurudi kazini.
Hata hivyo, alisema mgomo huo ni halali, kutokana na wao kudai haki ya msingi na kufuata taratibu zote, hivyo si kweli kuwa mgomo huo ni batili.
Hii ni mara ya pili kwa wafanyakazi wa Tazara kupelekwa mahakamani, ambapo pia Mei mwaka jana menejimenti hiyo iliwaburuza wafanyakazi wake katika Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, kwa madai ya kufanya mgomo kinyume cha sheria.
Aidha, Agosti, mwaka juzi Mkurugenzi Mtendaji wa Tazara, alitangaza kuwafukuza kazi wafanyakazi 1,076 wa mamlaka hiyo upande wa Tanzania, kutokana na kufanya mgomo usio wa halali na kusababisha hasara ya dola za Marekani 600,000 (Sh milioni 972 kwa mwaka huo).
Awali wafanyakazi hao kupitia chama chao na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta), walitoa siku saba kwa mamlaka hiyo kuhakikisha inawalipa mishahara yote ya miezi mitano.
Chanzo:Habari leo
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment