Home » » WENYEVITI WAAPISHWA KWA MABOMU DAR

WENYEVITI WAAPISHWA KWA MABOMU DAR

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura
 
Hafla ya a kuapisha wenyeviti wateule wa serikali za mitaa wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, jana ilitawaliwa na mapambano na kulilazimisha Jeshi la Polisi kuingilia kati kwa kutumia mabomu kurejesha amani huku likiwatia mbaroni watu saba.
Hafla hiyo iliingia dosari baada ya wananchi kuvamia eneo la uapishaji na kuanza kutembeza mkong’oto na kuwajeruhi  wanachama wawili wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa madai hawakushinda katika mitaa yao, lakini walikwenda kuapishwa.

Vurugu hizo ambazo ziliwalazimu polisi kupiga mabomu kuwaokoa wanachama wa CCM waliokuwa wakipewa kichapo, zilitokea kati ya saa 3:00 na 4:00 asubuhi katika eneo la hoteli la Land Mark Ubungo ambako hafla hiyo ilikuwa ikifanyika.

Wanachama wa vyama vya CCM, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama cha Wananchi (CUF), walianza kujikusanya eneo hilo na ghafla walijitokeza wanachama wawili wa CCM ambao nao walikwenda kuingia ukumbini kuapishwa hivyo kupewa kichapo.

Waliopewa kichapo ni Juma Mbena kutoka mtaa wa Msisili ‘A’ na Semtani Jeta wa mtaa wa Mkwamani Kata ya Kawe ambao walifika eneo hilo kwa lengo la kuapishwa.

Hata hivyo, kabla hawajaingia ukumbini, wananchi walianza kuwashambulia kwa kipigo huku wakihoji inakuwaje  wanachama hao wa CCM wakaapishwe wakati hawakushinda uchaguzi katika mitaa yao uliofanyika kati ya Desemba 14 na 21 mwaka jana.

“CCM wanataka kufanya hujuma hawa tunawafahamu hawakushinda uchaguzi kwenye mitaa yao, sasa inakuwaje ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni iwape barua za kuitwa kuapishwa huku walioshinda wakinyimwa kupewa barua za kuitwa,” walisikika wananchi hao wakihoji.

Wakati vurugu hizo zikiendelea, mawili ya polisi yenye namba za PT 1896, T 848 AGJ yakiwa na askari zaidi ya 13 wakiwa na mabomu na silaha za moto yalifika na kuanza kupiga mabomu ovyo kutawanya wananchi.

Wanachama hao wa CCM waliokuwa wakipigwa baadaye waliokolewa na polisi hao na kuchukuliwa kwa gari yenye namba za usajili PT 1896 na kuondolewa eneo hilo.

Kufuatia hali hiyo, wananchi wakiwamo wasafiri waliokuwa wakienda katika kituo cha mabasi yaendayo mikoani na nje ya nchi cha Ubungo (UBT) walipata wakati mgumu kutokana na mabomu hayo na huku wengine wakilazimika  kurudi nyuma na kupita sehemu nyingine.

Vurugu katika eneo hilo zilidumu kwa takribani nusu saa huku polisi wakiimarisha ulinzi katika ukumbi ambao shughuli hiyo ilikuwa ikifanyika na magari ya polisi yakiwa yameegeshwa kwenye lango la kuingilia na askari wenye silaha wakiwa eneo hilo.

Aidha, baadhi ya wanachama wa Chadema walilalamika kwamba baadhi ya maeneo walishida wanachama wao, lakini wakatangazwa wa CCM.

Mwenyekiti wa mtaa wa King’ongo (CUF), Abubakar Said Nyamguma, akizungumza na NIPASHE nje ya ukumbi, alisema yeye ni miongoni mwa walishindi ambao wamefanyiwa hujuma kwa kutopewa barua ya kuitwa kwa ajili ya kuapishwa.

“Mimi nilishinda katika mtaa wangu kwa kura 461 nikamshinda mgombea wa CCM, Dematius Mapensi, ambaye cha kushangaza amepewa barua ya kwenda kuapishwa,” alisema.

Nyamguma alisema kufuatia hali hiyo, amewasiliana kwa simu na Ofisa Mtendaji wa Kata ya Salanga kumuuliza kwanini hajampa barua ya kuitwa kuapishwa, lakini hakumpa ushirikiano.

Hata hivyo, Ofisa Mtendaji wa Kata hiyo, Zuhra Almas, alisema mgombea wa CCM, Mapensi ndiye aliyeshida uchaguzi kwa kupata kura 463 dhidi yamgombea wa CUF aliyepata kura 461.

Zuhra alisema baada ya kutangazwa matokeo mgombe wa CUF aliandika barua kuyapinga ambayo ilipelekwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, lakini bahati mbaya hadi sasa majibu hayajatoka manispaa.

MAJIBU YA MKURUGENZI
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Injinia Mussa Natty, akizungumzia vurugu hizo, alisema anasikitishwa na hali hiyo iliyojitokeza na kwamba waliokuwa wakilalamikia matokeo walipashwa kwenda mahakamani.

“Nchi hii tulipofikia siyo pazuri, inajulikana wazi uchaguzi ukiisha, aliyetangazwa ndiye mshindi na kama mtu hujaridhika unakwenda mahakamani,” alisema.

Natty alipoulizwa kwamba inakuwaje baadhi ya wenyeviti ambao uchaguzi katika mitaa yao ulikuwa na utata na suala hilo limefikishwe kwenye vyombo vya sheria, lakini wamekwenda kuapishwa.

Alisema kiutaratibu mahakama itakavyoamua kama mlalamikaji ameshinda atarudishiwa nafasi yake ya uenyekiti na kama ameshindwa, mlalamikiwa atabaki kuwa mwenyekiti wa mtaa husika.

Mkurugenzi huyo kabla ya hafla ya kuapisha kuanza, aliwaeleza wenyeviti wa serikali za mitaa kuwa uongozi wa mtaa ni kiungo kikubwa kati ya wananchi na manispaa, hivyo watoe ushirikiano kwa halmashauri  ili kuwaletea maendeleo wananchi.

“Majukumu ya mwenyekiti wa mtaa ni makubwa na kazi hii sehemu kubwa ni ya kujitolea, bila ninyi manispaa yetu haiwezi kuwa na maendeleo, wekeni itikadi za vyama vyenu pembeni katika suala la utekelezaji wa maendeleo kwa wananchi,” alisema.

Kabla ya kuapishwa, wenyeviti hao walipewa mafunzo na mada zilizotolewa ni pamoja na upangaji wa mipango, majukumu ya mwenyekiti wa mtaa, majukumu ya kamati mtaa na mkutano mkuu wa mtaa, wajibu wa wenyeviti wa mitaa katika suala la usafi na kukusanya mapato.
Jumla ya wenyeviti 197 waliapishwa.

KAULI YA POLISI
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura, aliliambia NIPASHE jana jioni kuwa katika vurugu hizo, polisi waliwatia mbaroni watu saba.

Kamanda Wambura aliongeza kwamba uchunguzi unaendelea na baada ya kukamilika, watuhumiwa watafikishwa mahakamani.

Kumekuwapo na matukio ya vurugu katika maeneo kadhaa ikiwamo wilaya ya Tarime, mkoani Mara wakati wa kuapisha viongozi waliochaguliwa kuongoza mitaa, vitongoji na vijiji.
 
SOURCE: NIPASHE
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa