Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Didas Masaburi.
Msemaji wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Gaston Makwembe,
aliwahi kunukuliwa na vyombo vya habari (siyo gazeti hili), kuwa ujenzi
wa kituo hicho unatarajiwa kuanza mwezi ujao na kwamba maandalizi
yalikuwa yanaendelea.
Stendi hiyo ambayo imekuwapo eneo la Ubungo tangu miaka ya katikati
ya tisini inalazimika kuhamishwa kwa kuwa sehemu kubwa ya eneo lake
imemegwa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya mabasi yaendayo haraka
(Dart), hivyo kubakiwa na eneo dogo lisilokidhi mahitaji.
NIPASHE lilitembelea eneo hilo ambalo stendi inatarajiwa
kuhamishiwa na kukuta halijafanyiwa maandalizi yoyote huku likiwa na
milima, mabonde na vichaka vinavyohatarisha usalama wa wakazi waliopo
jirani na eneo hilo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wakazi hao walisema eneo hilo kwa
sasa ni hatarishi kutokana na vibaka kujificha na kufanya uhalifu
nyakati za usiku ikiwamo ubakaji.
Aldo Mkande maarufu kama Mnyal’ alisema eneo hilo limekaa wazi kwa
muda mrefu na serikali hadi sasa haijamaliza kuwalipa fidia wakazi wa
eneo hilo.
“Mimi eneo langu sijalipwa bado na serikali haijanifuata wala
sijapewa barua ninasikia tu kutoka kwa watu kuwa serikali inahitaji
kuhamishia stendi ya mabasi katika eneo hili,” alisema Mkande.
Naye Khadija Salum, alisema mwaka jana serikali iliweka nguzo
zinazoonyesha mpaka wa eneo hilo lakini kwa hivi sasa nguzo hizo hazipo
baada ya kuibwa na vibaka.
Baadhi ya wakazi ambao hawakutaka kutaja majina yao walieleza kuwa
serikali haikuwa makini na ujenzi wa kituo hicho bali kunaufisadi
unaendelea wa ‘kutafuna’ fedha za Watanzania.
NIPASHE lilipofika eneo hilo liliwakuta vijana wakicheza mpira wa
miguu, pamoja na biashara ya ununuzi wa chupa za plastiki ukiendelea.
Eneo hilo limekuwa kwenye mgogoro kwa muda mrefu kati ya wakazi wa
eneo hilo na serikali, baada ya wakazi hao kufungua kesi mahakamani
kupinga fidia ndogo waliyokuwa wanalipwa.
Wakazi hao walipata nguvu kubwa zaidi mwaka juzi baada ya kushinda
kwa kishindo kesi yao namba 80 ya mwaka 2005 iliyowasilishwa Mahakama
Kuu ya Ardhi Jijini Dar es Salaam.
Kwenye kesi hiyo iliyofunguliwa Mahakama Kuu, Kitengo cha Ardhi na
Proches Eleza Tarimo na wenzake 72, dhidi ya Katibu Mkuu wa Wizara ya
Ujenzi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, mahakama ilitambua kuwa
wanamiliki maeneo yao kihalali.
Pamoja na mambo mengine, hukumu hiyo inaitaka serikali kulipa fidia
kwa wenye maeneo hayo kama inataka kuyatwaa kulingana na sheria ya
ardhi ya vijiji ya mwaka 1999
Wakati hukumu ikisema hivyo, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Didas
Masaburi, aliwahi kunukuliwa na gazeti hili kuwa Halmashauri ya jiji la
Dar es Salaam ndiyo mmiliki halali wa maeneo hayo na kwamba wanaendelea
na mchakato wa kuandaa michoro kwa ajili ya ujenzi wa stendi hiyo
ikikadiriwa kugharimu Sh. bilioni sita katika hatua za awali.
CHANZO:
NIPASHE
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment