Na. Aron Msigwa –
MAELEZO.
SERIKALI imewataka
wamiliki wa viwanda kuwapa ushirikiano wadadisi wa Sensa ya Viwanda watakaopita
katika maeneo yao kwa lengo la kukusanya takwimu sahihi za viwanda vilivyopo nchini na mchango vinaotoa katika
maendeleo ya taifa.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es salaam na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Maria Bilia
wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku 14 ya wadadisi wa Sensa ya Viwanda yanayoendelea katika chuo
cha Takwimu cha Mashariki mwa Afrika kilichopo eneo la Changanyikeni jijini Dar
es salaam.
Amesema
kuwa mafanikio ya Sensa hiyo yatatokana na wamiliki wa viwanda
kuthamini
na kutambua umuhimu za Sensa hiyo kwa kutoa ushirikiano kwa wadadisi
watakaopita katika maeneo yao kupata taarifa zinazohusu masuala
mbalimbali ikiwemo uzalishaji wa bidhaa na masuala ya ajira;
Amesema upatikanaji wa
takwimu sahihi kuhusu Sekta ya Viwanda nchini Tanzania utaiwezesha Serikali
kuweka Sera na mipango endelevu ya maendeleo itakayoisaidia sekta hiyo kupiga
hatua kimaendeleo.
“Sensa hii ya viwanda
ni muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu, na mafanikio yake yatatokana na wenye
viwanda kutupa ushirikiano maana bila wao
kutoa takwimu sahihi mipango ya maendeleo kuhusu viwanda haitatekelezeka kwa
sababu ya kukosa takwimu sahihi” Amesema Bilia.
Kuhusu sampuli ya
viwanda vitakayoguswa na Sensa hiyo
amesema ni pamoja na maeneo ya viwanda
yaliyoajiri watu wengi na yanayohusisha uzalishaji
mkubwa wa bidhaa za viwandani ,maeneo ya uzalishaji wa bidhaa za kokoto, bidhaa
za vyakula na maeneo yaliyoajiri mtu zaidi ya mmoja.
Kwa upande wake
Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Dkt. Albina Chuwa akizungumza
wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo amesema kuwa Sensa hiyo ya viwanda itakayohusisha
viwanda vyote nchini inafanywa kwa ushirikiano wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu na
Wizara ya Viwanda na Biashara.
Amesema kukamilika kwa
Sensa hiyo kutaliwezesha taifa kuwa na takwimu sahihi za viwanda na kutambua
mchango wa Sekta ya viwanda katika uchumi wa taifa na mchango wa ajira kwa
wananchi.
Kuhusu mafunzo hayo ya
siku 14 kwa wadadisi 200 watakaoendesha zoezi hilo amesema Ofisi ya Taifa ya
Takwimu kupitia Chuo cha Takwimu cha Mashariki mwa Afrika inaendesha mafunzo
hayo kwa vitendo na nadharia ili kuwawezesha na kuwajengea uwezo wadadisi hao
kukusanya takwimu bora.
“Lengo la kuendesha
Sensa hii ni kuhakikisha kuwa nchi yetu
inapiga hatua na kuwa nchi yenye maendeleo ya kati kwa kuwa na matumizi sahihi
ya takwimu ztu”
Kaimu Mkurugenzi wa
Shirikisho la wenye Viwanda nchini Bw.Hussein Kamote akizungumza wakati wa
ufunguzi wa mafunzo hayo kwa niaba ya wamiliki wa Viwanda nchini amesema kuwa
Sensa ya viwanda itakayofanyika nchini mwezi huu italiwezesha taifa kuwa na takwimu sahihi zinazohusu sekta ya
viwanda.
“Sensa hii ya viwanda
ni muhimu sana kwa maendeleo ya taifa nawaomba wenye viwanda watoe ushirikiano
wa kutosha maana bila wao zoezi hili litakuwa gumu”
Ameongeza kuwa Sensa ya
viwanda ni muhimu kutokana na mchango wake katika nchi nyingi za Asia ambazo
zimefanikiwa na kupiga hatua kimaendeleo kwa sababu ya kuwa Sensa endelevu na
takwimu sahihi za sekta ya viwanda na mchango wake katika pato la taifa.
MWISHO.
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment