Na
Saidi Mkabakuli
Waziri
wa nchi (Ofisi ya Rais) Mahusiano na Uratibu, Mhe. Dkt. Mary Nagu amefanya
ziara ya kujitambulisha kwa Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango ambayo ni moja
taasisi anazoziratibu.
Akizungumza
wakati wa ziara hiyo Dkt. Nagu alitoa wito kwa Tume ya Mipango ijielekeze
katika kujibu changamoto kuu za kiuchumi zinazowakabili watanzania kwa sasa
ikiwemo umaskini miongoni kwa Watanzania walioko vijijini, ukosefu wa wa
viwanda vya kuongeza thamani mazao hasa kipindi hiki Tanzania inapoelekea kwenye
uchumi wa gesi.
Dkt. Nagu aliasa Tume ya Mipango kufanya tafiti
mbalimbali za kiuchumi na kijamii zitakazotoa majibu ya changamoto hizo.
“Kwa kuwa moja
ya majukumu ya Tume ya Mipango ni kuandaa mipango ya maendeleo ya muda mrefu,
kati na ile ya kila mwaka na pia kufanya tafiti mbalimbali za kiuchumi na
kijamii, napenda kusisitiza kuwa mipango inayoandaliwa ijielekeze katika kujibu
changamoto hizo kubwa zinazowakabili wananchi wetu ili kuhakikisha kuwa
tunafikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025,” alisema Dkt. Nagu.
Kwa mujibu wa malengo makuu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo
2025, serikali imejipanga kuhakikisha maisha bora na mazuri kwa kila mtanzania,
utawala bora unaozingatia sheria, na kujenga uchumi imara, wa kisasa na
ushindani.
Akizungumza wakati wa kumkaribisha Dkt. Nagu, Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Dkt. Philip
Mpango alisema kuwa majukumu ya msingi ya Tume ya Mipango ni kutoa dira na mwongozo wa uchumi
wa Taifa pamoja na kubuni sera za uchumi na mikakati ya mipango ya maendeleo ya
Taifa; usimamizi wa uchumi na kufanya utafiti katika nyanja za uchumi na
maendeleo ya jamii.
Dkt. Mpango aliongeza kuwa kwa sasa Tume ya Mipango inafanya kazi ya kuratibu utekelezaji wa Mpango wa
Maendeleo wa Taifa 2014/15 pamoja na uandaaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa
2015/16 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2016/17.
“Vilevile, Tume
ya Mipango tumejidhatiti katika kuandaa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano
2016/17 – 2020/21 ambao utajikita katika kuifikisha tanzania kuwa ni nchi ya
viwanda,” alisema Dkt. Mpango.
Kwa mujibu wa Dkt. Mpango, tangu kuundwa upya kwa Tume ya
Mipango mwaka 2008, imefanikiwa kukamilisha kazi kubwa za kitaifa ikiwemo
kufanya mapitio ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, kuandaa Mpango Elekezi wa
Miaka 15 (2011/12 – 2025/26 pamoja na kuandaa Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa
Miaka Mitano (2011/12 – 2015/16) na kuratibu utekelezaji wa Sera ya Taifa ya
Idadi ya Watu 2006.
Kazi nyingine ni pamoja na kuandaa Mipango ya Maendeleo
ya Taifa kila Mwaka, kuandaa mfumo wa ufuatiliaji na utekelezaji wa miradi ya
Matokeo Makubwa Sasa na kuratibu uanzishwaji wa President Delivery Bureau
(PDB), Kuandaa Mwongozo wa Usimamizi wa Uwekezaji katika Sekta ya Umma (Public
Investiment Management - Operational Manual – PIM-OM), na kufanya tafiti
mbalimbali za kiuchumi na kijamii.
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment