Home » » MTUHUMIWA SUGU UTAPELI WA VIWANJA DAR MBARONI.

MTUHUMIWA SUGU UTAPELI WA VIWANJA DAR MBARONI.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Alphayo Kidata.

Mtu mmoja ambaye anadaiwa kuwa kinara wa utapeli wa viwanja jijini Dar es Salaam (jina linahifadhiwa kwa sasa), leo anatarajiwa kupandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, kujibu tuhuma zinazomkabili.
 
Mtuhumiwa huyo ambaye aliwahi kufanyakazi katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, anadaiwa kutapeli zaidi ya viwanja 30, kikiwamo cha familia ya Mwalimu Julius Nyerere na cha Katibu Mkuu wa Wizara Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, pamoja na cha mwanamke mmoja ambaye alikuwa akifanya kazi Umoja wa Mataifa (UN). Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura, amethibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo.
 
Habari za ndani ambazo NIPASHE ilikuwa ikizifuatilia kuhusiana na mtuhumiwa huyo, zinaeleza kuwa, amekuwa akitapeli viwanja mbalimbali katika maeneo nyeti ya Mikocheni, Mbezi Beach na Oysterbay, jijini Dar es Salaam.
 
Akizungumza na gazeti hili kwa masharti ya jina lake lisiandikwe gazetini, wakili mmoja alisema kuna baadhi ya vigogo ambao wanamlinda na jambo la kushangaza amekuwa akipata hati kutoka Wizara ya Ardhi wakati siyo mmiliki halali wa viwanja hivyo.
 
 “Kuna kiwanja amekidhulumu cha Mbezi Beach mmiliki kaenda kufungua kesi lakini akamtishia kumuua, yaani mwenye kiwanja hana amani na maisha yake na huyo mtu huwa anashirikiana na polisi,” alisema na kuongeza:
 
 “Jambo jingine la kushangaza hata Katibu Mkuu wa Ardhi amemdhulumu kiwanja chake na hata kesi ilivyofunguliwa, jalada la kesi lilipotea katika mazingira ya kutatanisha.”
 
Alisema anashangazwa ni kwa nini mtuhumiwa huyo hachukuliwi hatua wakati watu wanapoteza haki zao za msingi, huku baadhi ya watu wakimlinda.
 
Akizungumza na NIPASHE jana, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Alphayo Kidata, alisema ni kweli mtuhumiwa huyo amekuwa akidhulumu viwanja vya watu na kwamba walikuwa wanakusanya taarifa zake kwa umakini ili kumfikisha kwenye vyombo vya dola.
 
Alisema mtuhumiwa huyo aliwahi kufanyakazi wizarani hapo na kwamba alikamatwa Jumamosi katika kesi ya kudhulumu viwanja viwili vilivyopo Mikocheni vyenye namba 507/2/1 na 507/2/2, Block C ambacho kimojawapo ni cha familia ya Mwalimu Nyerere.
 
Alisema atafikishwa mahakamani kwa ajili ya viwanja hivyo viwili kwanza na kwamba vingine vitafuata ambavyo amevidhulumu.
 
Kidata alisema yupo tayari kwa lolote katika kuhakikisha viwanja hivyo vinarudishwa kwa wananchi na kwamba hayupo tayari kuona haki ya mtu inapotea.
 
"Wapo wengi ambao amewadhulumu viwanja sasa nimeanza na viwanja hivi viwili, vingine vitafuata nyuma na nipo tayari kwa lolote lakini haki itendeke na siyo watu kuumia huku haki zao zikipotea, huwa naumia sana ninapoona mtu anadhulumiwa haki yake," alisema.
Katibu huyo alisema wote ambao wametapeliwa viwanja vyao wajiandae kuyapokea maeneo yao.
 
Kidata alipoulizwa kama ni kweli na yeye ni miongoni mwa watu waliotapeliwa viwanja na mtuhumiwa huyo, hakutaka kulizungumzia suala hilo na kusema yapo mengi lakini atayaelezea baadaye. Alipoulizwa kuhusiana na mtuhumiwa huyo kudaiwa kufanyakazi wizarani hapo, katibu mkuu huyo alithibitisha kuwa ni kweli alishawahi kufanyakazi Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
 
Alisema kijana huyo ana tuhuma nyingi na wizara inaendelea kumfuatilia pamoja na wengine ambao wanamfuata nyuma ili wachukuliwe hatua na iwe fundisho kwa wengine kuacha michezo hiyo michafu.
CHANZO: NIPASHE
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa