Home » » MUHIMBILI YAKAUKIWA DAMU KWA WAGONJWA.

MUHIMBILI YAKAUKIWA DAMU KWA WAGONJWA.

aWaziri wa Afya na Ustawi, Dk. Seif Rashid.

 Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), inakabiliwa na uhaba wa damu kwa kiasi kikubwa, hali inayosababisha kitengo cha damu kuhudumia wagonjwa wa dharura zaidi, kuliko walio na magonjwa sugu. 
 
Kitengo cha damu hospitalini hapo, kimekuwa kikipokea maombi yapatayo 100 kwa siku, na uwezo wake ni kutoa chupa 50 hadi 65, sawa na asilimia 60.
 
 Maombi hayo ya damu ni kutoka idara ya dharura, kwa ajili ya akina mama wajawazito, watoto waliopo kwenye matibabu ya saratani, pamoja na vyumba vya upasuaji. 
 
Akizungumza na NIPASHE, mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma na Huduma kwa Wateja, Aminiel Aligaesha, alisema hali hiyo inatokana na mahitaji makubwa na ukusanyaji mdogo wa damu, ikiwamo mwamko mdogo wa jamii wa kuchangia damu.
 
"Hatuna damu ya kutosheleza kwa asilimia 100, hospitali hii ni ya Taifa, tunapokea wagonjwa wengi na mahitaji ni makubwa zaidi na tofauti na benki ya damu iliyopo," alisema Aligaesha.
 
Alisema kati ya maombi yote kwa siku, MNH hutoa chupa 50 za damu, kupitia kitengo cha ukusanyaji damu hospitalini hapo.
 
 Pia, alisisitiza kuwa damu haiuzwi kwa wagonjwa bali hutolewa bure na aliwasihi ndugu wa wagonjwa kutokutoa hela ili wahudumiwe.
 
"Tunaendelea kuwasihi watu kuchangia damu ili kuweza kuokoa maisha ya wagonjwa wa dharura, ajali na wengineo, tunapendekeza kuwa turuhusiwe kwenda kufanya kampeni nje ya hospitali tuweze kuwasaidia wagonjwa zaidi na si kutegemea sana Mpango wa Taifa wa Damu Salama (NBTS)," aliongeza.
 
Naye Meneja wa Mpango wa Taifa wa Damu Salama Kanda ya Mashariki, Aveline Mgasa, alisema taasisi hiyo inakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa damu salama, ili kukidhi mahitaji. 
 
Alisema uwezo wa kukusanya damu salama ni chupa 160,000 wakati mahitaji ni chupa 450,000.
 
Waziri wa Afya na Ustawi, Dk. Seif Rashid alipotafutwa ili kuzungumzia hali hiyo hakupatikana na msemaji wa wizara, Nshachris Mwamwaja, alisema yupo kwenye kikao.
 
CHANZO: NIPASHE
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa