Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MVUTANO mpya unarajiwa kuibuka katika ugawaji wa majimbo mapya kati ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Hatua hiyo inatokana na uamuzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutangaza ugawaji wa majimbo ya uchaguzi huku mapya yakitarajiwa kuongezeka.
Mchakato huo wa kugawa majimbo ya uchaguzi unatarajiwa kuanza leo kwa kutoa tangazo katika Gazeti la Serikali kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi.
Akitangaza uamuzi huo Dar es Salaam jana mbele ya viongozi wa vyama vya siasa, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Mstaafu Damian Lubuva, alisema mgawanyo huo wa majimbo mapya ya uchaguzi utazingatia vigezo 13 ikiwa ni pamoja na jimbo kuwa ndani ya halmashauri au wilaya mbili hali inayomfanya mbunge mmoja kutumika katika sehemu hizo mbili.
Jaji Lubuva alitaja taratibu zinatarajiwa kutumika kuwa ni pamoja na mgawanyo wa wastani wa idadi ya watu ambayo itapatikana kwa kuzingatia idadi ya watu wote nchini, wa mijini na vijijini.
Alisema kigezo kingine kitakachotazamwa ni idadi ya watu itakayotokana na makisio ya ongezeko la watu hadi kufikia Julai mwaka huu na kwa kuzingatia Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012.
“Pia kigezo chetu kingine ni upatikanaji wa mawasiliano yanayomuwezesha mwakilishi kuwafikia kwa urahisi wananchi kwa njia ya simu, barabara, vyombo vya habari.
“Pia tutaangalia jografia kwa kuangalia mahali iwapo jimbo litakuwa milimani, visiwani au mabondeni ili kujua namna bora ya uwasilishwaji wake,” alisema Jaji Lubuva.
Alisema katika ugawaji wa majimbo mpya pia itaangaliwa hali ya uchumi ikiwa na dhamira ya kukwepa maeneo yenye uchumi mkubwa kumeza katika uwakilishi maeneo yaliyo chini katika uchumi.
“Takwimu zitakazotumiwa ni za ukusanyaji wa mapato zilizopatikana kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na asilimia ya watu walio chini ya kiwango cha umasikini kilichopatikana katika Ofisi ya Makamu wa Rais(OMR),” alisema.
Alisema ukubwa wa jimbo husika na taarifa zake zitakazopatikana katika OMR na NEC, ni miongoni mwa vigezo vitakavyotumika katika kupata majimbo mapya ya uchaguzi.
“Mipaka ya utawala na pale ambako itabadilika kabla ya kufanya ugawaji wa majimbo, NEC itazingatia mabadiliko hayo. Uwepo wa kata moja kutokuwa katika majimbo mawili na kuangalia mpangilio wa maeneo ya makazi ya watu yaliyopo, ikiwamo mazingira ya muungano.
“Tanzania ni muungano wa nchi mbili hivyo ugawaji wa majimbo utazingatia upekee wa mazingira ya Muungano,” alisema.
Jaji Lubuva alisema kigezo kingine kitakachoangaliwa ni uwezo wa ukubwa wa Bunge kuepuka kuzidisha idadi tofauti na inayostahili.
Vigezo viti maalumu
Mwenyekiti huyo NEC alisema kigezo kingine ni kuhusu viti maalum vya wanawake ambako kwa mujibu wa Katiba imetengwa asilimia 30 ni kwa ajili ya wajumbe wanawake ili kuweka usawa wa jinsia.
“Kutokana na ukweli kwamba idadi ya wanawake wa viti maalumu imekuwa ikiongezeka kila mwaka wa uchaguzi, hivyo kama mwaka huu itaongezeka, NEC itabidi izingatie ongezeko hilo,” alisema.
KURA YA MAONI
Jaji Lubuva, alisema ucheleweshwaji wa uandikishaji wa Kura ya Maoni ulichangiwa na ukosefu wa fedha lakini sasa limetatuliwa hivyo wanatarajia kumaliza hatua ya uandikishwaji kabla ya Oktoba mwaka huu.
“Tulianza na vifaa 250 katika majaribio, baadaye tukaongeza zikawa 248, Aprili 17 tukapata nyingine 1600, Aprili 25 tukaingiza vifaa 1572.
“Mei 20 tunatarajia kuingiza vifaa vingine 1600 na itakapofika Mei 29 serikali itaingiza vifaa vingine 1500, ambavyo naamini vitawezesha kumaliza zoezi hilo kabla ya Oktoba,” alisema Jaji Lubuva.
Profesa Lipumba
Akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba aliitaka tume kutanguliza uwazi katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu na iepuke kurudia yaliyofanyika katika kura ya maoni.
Alisema wamekuwa wakipokea taarifa kutoka kwa watu walio ndani ya serikali kwamba tayari NEC imeshagawa baadhi ya majimbo taarifa ambazo zimekuwa zikiwatia hofu.
“Nimetembelea baadhi ya maeneo ya Kusini hususan Mkoa wa Mtwara, nimepata taarifa kutoka kwa watu walio ndani ya Serikali wakisema jimbo la Masasi pamoja na lile la Mtwara limegawanywa, leo mnatuambia bado hamjagawanya huku ni kutufanyia ‘danganya toto’,” alisema Lipumba.
Alisema katika mkoa huo kuna baadhi ya maeneo ambayo idadi kubwa ya watu hawajaandikishwa katika uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura.
Nape
Naye Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye alisema ni vizuri tume ikaweka wazi ratiba nzima ya uchaguzi kuwaondoa hofu baadhi ya wanasiasa hasa wale wa upinzani wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) akiwamo Profesa Lipumba.
“Mimi nafikiri hofu kubwa ya wenzetu (UKAWA) inatokana na wao kuwa tayari wameshagawana majimbo ya uchaguzi, sasa leo mnapotueleza kwamba huenda yakagawanywa kulingana na vigezo 13 mlivyotueleza inawashtua.
“Itabidi NEC muweke ratiba nje kuwatoa hofu UKAWA ili wakajipange upya,” alisema na kuwaacha watu hoi kwa vicheko akiwamo Lipumba.
Mziray
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa na Rais Mtendaji wa Chama cha APPT-Maendeleo, Peter Mziray alitaka kujua kutoka kwa Tume iwapo kura ya maoni itafanyika au haitafanyika.
“Toeni ratiba nzima mkifanya hivyo hatutakuwa na ugomvi nanyi na hata kwa hatua ya kura ya maoni binafsi naona haiwezekani nendeni tu mkamshauri Rais Kikwete kwamba aiache.
“Lakini sijui nani anaweza kulisemea hilo labda tupeleke sheria ndani ya Bunge la Bajeti litakaloanza kwamba suala la Katiba liachwe hadi Rais mwingine ajaye na huyo tumlazimishe kuandika Katiba,” alisema.
Akijibu hofu hiyo ya kura ya maoni, Jaji Lubuva alisema kwa sasa wanasiasa wanatakiwa kujikita zaidi katika daftari la wapiga kura.
“Suala la Kura ya Maoni mimi nafikiri lingeachwa kwanza hadi tutakapomaliza uandikishaji wa daftari ndipo tunaweza kutangaza tarehe rasmi ya kufanyika kwa kura hiyo,” alisema.
Majimbo mapya
Kutokana na hali hiyo baadhi ya majimbo ambayo yanaweza kugawanywa ni pamoja na jimbo la Kahama Mjini ambalo lipo katika halmashauri mbili za Ushetu na Kahama, hali inayomfanya mbunge wa sasa kuhudhuria vikao katika maeneo yote mawili.
Majimbo ya Kondoa Kusini na Kaskazini nayo yanatarajiwa kuingia katika kugawanywa baada ya Wilaya ya Kondoa kugawanywa na kuzaliwa wilaya mpya ya Chemba.
Pia majimbo ya Mbinga Mashariki na Magharibi nayo huenda yakaingia katika vigezo vya NEC baada ya kuanzishwa kwa Wilaya mpya ya Nyasa.
Majimbo ya mwaka 2010
Mwaka 2010, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) iligawa majimbo mapya ambayo ni Tunduru (Ruvuma) yalizaliwa majimbo ya Tunduru Kaskazini na Kusini, Nkasi (Rukwa) yalianzishwa majimbo ya Nkasi Kusini na Kaskazini, Maswa (Simiyu) Maswa Magharibi na Mashariki, Bukombe (Shinyanga), Singida Kusini (Singida), Kasulu Mjini na Vijijnini (Kigoma) na Ukonga na Segerea (Dar es Salaam).
Uamuzi kuhusu mapendekezo ya kugawa majimbo ya uchaguzi ulifikiwa na NEC baada ya kufanya uchambuzi.
Mapendekezo hayo yaliwasilishwa NEC na Kamati za Ushauri wa Mkoa (RCC) baada ya halmashauri 45 kupeleka maombi 47 zikitaka kugawanywa majimbo yao.
Hofu kwa wabunge
Kutokana na taarifa za ugawaji wa majimbo hivi sasa idadi kubwa ya wabunge wamejichimbia majimboni kwao kusubiri hatima yao.
chanzo:Mtanzania
0 comments:
Post a Comment