Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
HAIJAPATA kutokea, ndivyo unavyoweza kusema kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha jijini Dar es Salaam kwa siku tatu mfululizo kuanzia juzi na kusababisha maafa makubwa.
Mvua hizo mbali ya kusababisha foleni za magari na shida ya usafiri kwa abiria wanaotumia mabasi ya umma, pia imesababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu ya barabara, madaraja, reli ambapo baadhi ya nyumba za wakazi wa jiji hilo zimejaa maji hivyo wamelazimika kuyahama makazi yao kwa muda.
Baadhi ya maeneo yaliyoathirika sana na mvua hizo ni Tandale, Buguruni kwa Mnyamani, Msimbazi, Tabata, Kigogo, Jangwani, Sinza, Mtoni, Mbagala, Kariakoo, Msasani, Mabibo, Kawe, Mikocheni, Gongolamboto, Ulongoni, Vingunguti.
Maeneo mengi ya jiji hilo hayapitiki kirahisi kutokana na mafuriko yaliyosababisha barabara na mitaro kujaa maji hivyo kusababisha usumbufu kwa madereva wa magari pamoja na watembea kwa miguu.
Waandishi wetu waliofika eneo la Jangwani, walishuhudia maji yamejaa juu ya daraja ambalo ujenzi wake umekamilika hivi karibuni ambapo baadhi ya nyumba nazo zilifunikwa kwa maji hivyo kuhatarisha usalama wa wananchi.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, baadhi ya wakazi waishio Jangwani, walisema mvua hiyo imewaathiri kwa kiasi kikubwa kutokana na maji kujaa hadi barabarani.
Walisema wamelazimika kuyahama makazi yao na kuhamia kwenye vituo vya mabasi yaendayo kasi ili kuokoa maisha yao pamoja na vitu vyao mbalimbali kama magodoro, vitanda, viti, meza, televisheni, redio na nguo.
Kwa upande wao, baadhi ya wakazi wa Kigogo Mwisho, walisema mvua hiyo imesababisha Mto msimbazi kujaa maji ambayo yamehamia kwenye makazi ya watu.
Mkazi wa Tabata, Bi. Anna John, alisema Watanzania wengi wamekuwa wakipuuza taarifa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA), juu ya athari za mvua na kuendelea kukaa mabondeni badala ya kuhamia maeneo salama.
Alisema ni vyema watu waishio mabondeni wakazingatia ushauri wa TMA ili waepukane na adha wanayoipata hasa yanapotokea mafurikio ambayo yanaweza kupoteza uhai
wao na kuharibu mali walizozitafuta kwa jasho jingi.
Katika Manispaa ya Kinondoni, Barabara ya Sinza Uzuri, Tandale kwa Tumbo na Mtogole, wananchi wengi wamezikimbia nyumba zao kutokana na maji kujaa ndani.
"Juzi na leo (jana), hatukulala ndani tukihofia usalama wetu, tumelazimika kulala kwenye mabaraza ya watu...kimsingi hali ni mbaya sana," alisema Asha Saidi, mkazi wa Tandale.
Polisi wafunga barabara
Kutokana na hali hiyo, Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, kimelazimika kuzifunga baadhi ya barabara ikiwemo ya Jangwani na Kigogo ambazo zilikuwa zimejaa maji hivyo kutopitika kirahisi ili kuepusha madhara yanayoweza kutokea.
Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, lilitoa wito kwa waajiri kuwaruhusu wafanyakazi wao mapema ili waweze kuanza safari ya kurudi nyumbani kutokana na barabara hizo kufungwa ili kuepusha usumbufu.
TMA wazungumza
Taarifa iliyotolewa na TMA, ilisema mvua hizo zitaanza kupungua kuanzi leo na kuwataka Watanzania waendelee kuchukua tahadhari kutokana na ardhi kushiba maji.
Familia zakosa makazi Z'bar
Katika hatua nyingine, mvua kubwa inayoendelea kunyesha Zanzibar, imesababisha watu 2,117 kukosa makazi na kupewa hifadhi katika Shule ya Sekondari Mwanakwerekwe C, baada ya nyumba zao kuathirika na mvua hizo.
Hadi sasa, mvua hizo ambazo zimeanza kunyesha alfajiri ya Mei 3, mwaka huu, zimeathiri nyumba 354 ambapo taarifa ya utafiti kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa, unasema mvua hiyo imefikia milimita 172.2.
Kiwango hicho ni kikubwa kutokea Zanzibar ikilinganishwa na kilichowahi kuripotiwa Mei 7,1972 ambacho kilifikia milimita 114.
Akiwasilisha taarifa ya awali kuhusu tathmini ya athari za mvua kwenye Kikao cha Kamati ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar chini ya Mwenyekiti wake, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, Katibu wa kamati hiyo, Dkt. Khalid Mohammed Salum, alisema watu watatu wamefariki dunia.
Alisema mbali ya mvua hizo kusababisha vifo, pia kumekuwa
na mashimo makubwa kwenye baadhi ya maeneo pamoja na kukatika kwa barabara.
Aliyataja maeneo yaliyoathirika na mvua hizo kuwa ni Nyerere, Magomeni, Jang’ombe, Karakana, Sebleni, Mwanakwerekwe, Sogea, Welezo, Kisauni, Tomondo, Mombasa, Kinuni.
Maeneo mengine ni Mtopepo, Chumbuni, Kwahani, Mpendae, Pangawe, Bububu na Kwaalinato, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na uongozi wa Mkoa Mjini Magharibi, Wilaya zake, Majimbo na Shehia husika, ilichukuwa hatua mbalimbali za kujaribu kukabiliana na maafa hayo.
Aliongeza kuwa, baadhi ya hatua zilizochukuliwa na Serikali ni pamoja na kufanya tathmini ya kina ili kujua idadi kamili ya watu walioathirika na mvua hizo.
"Serikali imelazimika kuzihamisha familia zilizokosa makazi kwa kuwaweka katika kambi maalumu kwenye Sekondari ya Mwanakwerekwe C na kuwapatia huduma za kibinaadamu pamoja na ubani kwa kila familia," alisema.
0 comments:
Post a Comment