Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Katibu wa Nec wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye.
Saa72 kabla ya kuanza mbio za uteuzi wa mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), vikao vya ndani vimeanza rasmi mjini hapa.
Jana vikao vya ndani vilianza kwa ajili ya maandalizi ya vikao vya Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) vinavyotarajia kuanza Ijumaa ijayo.
Viongozi kadhaa wa ngazi za juu wa chama hicho wakiwamo wajumbe wa sekretarieti walionekana katika ofisi ya makao makuu ya CCM maarufu kama ‘White House’ majira ya asubuhi na kuendelea hadi jioni.
Ajenda ambazo zinaandaliwa kwa ajili ya kujadiliwa na vikao hivyo ni kuandaa ratiba ya mchakato wa kuchukua fomu na kuzirejesha kwa ajili ya urais, udiwani na ubunge.
Ratiba hiyo pia itaonyesha ratiba za kura ya maoni na uteuzi wa wagombea wake kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.
Pia vikao hivyo vitajadili ilani ya uchaguzi ya chama hicho kisha kuipitisha kwa ajili ya uchaguzi huo.
Ingawa hadi sasa chama hicho hakijaeleza lolote kuhusu ukomo wa adhabu waliyopewa makada wake sita kutokana na tuhuma za kuanza kampeni za urais mapema kinyume cha kanuni na taratibu za chama hicho, kuna uwezekano wa kutolewa maamuzi hukusu hatma yao. Makada hao walifungiwa kwa miezi 12 kutogombea nafasi yoyote ndani ya chama.
Pia, makada hao waliwekwa chini ya uangalizi wa kutorudia kosa hilo.
Adhabu hiyo ilianza Februari 18, mwaka jana na ilitarajia kumalizika Februari 18, mwaka huu. Hata hivyo, Februari 28, mwaka huu CC ilipokutana, ilisema kuwa adhabu hiyo inaendelea.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Katibu wa Nec wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema hadi sasa makada hao wanaendelea kuchunguzwa na kwamba chama hakijaamua lini adhabu yao itafikia ukomo.
Waliofungiwa ni mawaziri wakuu wastaafu, Edward Lowassa na Frederick Sumaye; Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe; Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira; Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Nape Mei 16, mwaka huu, vikao hivyo vya awali vinafanya kazi ya kuandaa kikao cha CC na NEC.
Nape alisema vikao hivyo vingeanza jana hadi Mei 21, mwaka huu ambavyo vingefanyika Dar es salaam na vingine Dodoma vikiwamo vikao vya sekretarieti.
Alisema vikao hivyo vinaandaa na kuthibitisha ajenda ambazo zitajadiliwa na moja ya ajenda ambazo zitajadiliwa ni hali ya kisiasa nchini.
Baada ya vikao hivyo vitafuatiwa na kikao cha CC kitakachofanyika Mei 22, mkoani Dodoma na kuongozwa na Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Rais Jakaya Kikwete na Mei 23 na 24 kitafanyika kikao cha NEC.
Alisema vikao hivyo vya CCM vinatarajiwa pia kujadili ratiba ya mchakato wa uteuzi wa wagombea katika nafasi mbalimbali ndani ya chama.
Akizungumza na NIPASHE mjini hapa jana, Nape alithibitisha kuanza kwa vikao hivyo vya ndani jana, lakini alisema havitakuwa na taarifa yoyote kwa kuwa ni vya ndani.
“Niliwaambieni siku ile vikao vya kuanzia tarehe 18 Mei hadi Mei 21, achaneni navyo maana hatutatoa briefing (taarifa) yoyote maana haviwahusu, niliwaambia vitaanza tarehe hizo, lakini sikusema ni vikao gani?,” alisema Nape.
NIPASHE ilifika katika viwanja vya White House CCM Makao Makuu na kuona wajumbe mbalimbali wa sekretarieti akiwamo Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na Nape.
CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment