Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli (CCM) na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa (Chadema).
Wagombea hao, Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli (CCM) na Waziri
Mkuu wa zamani, Edward Lowassa (Chadema), walifanya hivyo kama sharti
la kutimiza sheria na kanuni kabla ya kurejesha fomu za kuomba kuteuliwa
kugombea nafasi hiyo.
Dk. Magufuli na Lowassa anayewania nafasi hiyo chini ya kivuli cha
Umoja wa Katiba ya Wananchi kupitia Chadema, kwa nyakati tofauti,
walifika mahakamani hapo jana wakiwa wameambatana na wafuasi wao
wachache kwa ajili ya kula kiapo hicho.
DK. MAGUFULI
Kwa upande wake, Dk. Magufuli na mgombea mwenza wake wa urais,
Samia Suluhu Hassan, walisaini fomu 40 za wadhamini waliowatafuta katika
mikoa 10 ikiwamo minane ya Tanzania Bara na miwili ya Tanzania
Visiwani.
Mgombea huyo wa CCM aliwasili katika viwanja vya mahakama hiyo saa
5:30 asubuhi akiwa ameongozana na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho
Tanzania Bara, Rajabu Luhwavi, maofisa wachache wa chama pamoja na
maofisa usalama.
Baada ya kuingia ndani, Dk. Magufuli alikwenda moja kwa moja mbele
ya Jaji Sekieti Kihio, kwa ajili ya kula kiapo na kusaini fomu zake
pamoja na za mgombea mwenza wake.
ALICHOZUNGUMZA
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kusaini fomu hizo, Dk.
Magufuli alisema kuna kanuni na sheria zinazotakiwa kufuatwa kwa mtu
anapotaka kushika madaraka ya kuongoza nchi na lazima zifuatwe.
|"Mambo mengine tusubiri tutakapopitishwa tunaomba mtuombee ..." alisema Dk. Magufuli.
LOWASSA
Lowassa aliingia saa 7:00 mchana akitanguliwa muda mfupi na mgombea
mwenza wake, Juma Duni Haji, Naibu Katibu Mkuu Chadema Bara, Salum
Mwalimu, wanasheria wa Chadema, Mabere Marando na Peter Kibatala,
aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Khamisi Mgeja na
aliyekuwa Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Makongoro Mahanga.
Mgombea huyo ambaye anapeperusha bendera ya Ukawa unaoundwa na
Chadema, Cuf, NCCR-Mageuzi na NLD, baada ya kuingia ndani, alikwenda
katika ofisi ya Jaji Kihio na kula kiapo pamoja na kusaini fomu za
wadhamini za mikoa 10 kati yake minane ya Tanzania Bara na miwili ya
Tanzania Visiwani.
ALICHOZUNGUMZA
Lowassa alisema hana kitu cha kuzungumza kwa kuwa bado wakati wake hadi pale atakapopitishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec).
MSAJILI WA MAHAKAMA ANENA
Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya wagombea hao
wawili kumaliza kula kiapo, Msajili Mkuu wa Mahakama Kuu Tanzania, John
Kahyoza, alisema Sheria ya Uchaguzi Namba 31, kifungu kidogo (1) cha
Kanuni za Uchaguzi wa Rais na Bunge ya mwaka 2015, inawataka wagombea
urais kula kiapo mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania ama Mahakama
ya Rufaa.
Alisema mgombea wa CCM alisaini fomu 40 za wadhamini aliopata
katika mikoa 10 ikiwamo miwili ya Zanzibar, huku mgombea wa Chadema
akisaini fomu sita za wadhamini kati ya 40 alizokwenda nazo.
Akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu, Kibatala alisema mgombea
wa Chadema alisaini fomu sita badala ya 40 kama alivyofanya mwenzake wa
CCM, kwa kuwa sheria inatamka mgombea kusaini fomu za wadhamini
aliowapata mikoani kati ya nne hadi sita.
Alisema anashangaa kusikia mgombea wa CCM amesaini fomu 40 na
kwamba hata marais waliopita walisaini idadi ya fomu nne za wadhamini.
KAMPENI ZA CCM
CCM imesema baada ya kesho kutwa kuzindua kampeni zake jijini Dar
es Salaam, itafanya kampeni katika maeneo yote ya nchi, huku ikifanya
mikutano 1,000 sawa na wastani wa mikutamo 15 kwa siku moja.
Kauli hiyo ya CCM ilitolewa na Luhwavi huku akiongeza kuwa
maandalizi yote kwa ajili ya mgombea wa chama hicho kufanya kampeni
yamekamilika.
Kuhusu namna chama kilivyojipanga kufanya kampeni katika mikoa ama
maeneo yenye idadi ya wapigakura wengi, Luhwavi alisema watahakikisha
wanawafikia watu wote ili wapate ujumbe wa kile wanachokisema.
KAMPENI ZA UKAWA
Wakati CCM wakitoa ratiba ya uzinduzi wa kampeni, Chadema chini ya
mwamvuli wa Ukawa, bado hawajasema watazindulia wapi na lini kampeni
zake.
Kampeni za uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani mwaka huu,
zitaanza Agosti 22, mwaka huu na zifanyika kwa siku 63 na upigaji kura
utafanyika Oktoba 25, mwaka huu.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment