Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com
Home » » Watumishi wa Umma watakiwa kushiriki zoezi la usafi disemba 9‏

Watumishi wa Umma watakiwa kushiriki zoezi la usafi disemba 9‏

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Na Shamimu Nyaki-Maelezo

Serikali imewaagiza watumishi wa umma kushiriki zoezi la usafi wa  nchi  litakalofanyika tarehe 9 disemba mwaka huu katika maeneo yao wanaoishi.

Agizo hilo limetolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Bw Assah Mwambene alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari leo jijin Dar es salaam na kusema kwamba Watumishi wa Umma  wanatakiwa wabaki nyumbani na kufanya usafi katika maeneo yao na  yale watakayo pangiwa na viongozi wa mitaa wanayoishi.

“Kila mwananchi ahakikishe eneo lake ni safi”Alisema Mwambene.

Mkurugenzi ameongeza kuwa Watumishi wa Umma hawataenda kazini badala yake  watabaki  nyumbani na kufanya usafi kwa kushirikiana na wananchi kusafisha maeneo yanayozunguka mitaa wanayoishi ikiwemo hospitali,kuzibua mitaro iliyoziba pamoja na kuzoa taka zilizolundikana sehemu ambazo sio rasmi.

Ameongeza kuwa muongozo kuhusu namna zoezi la usafi litakavyotekelezwa umeshatolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI  kwa Uongozi wa Mikoa hadi Mitaa na kilichobaki ni utekelezaji tuu wa agizo hilo kwa kila mwananchi sehemu anayoishi,anayofanyia shughuli nyingine za kila siku kuhakikisha anafanya usafi.

Aidha Mkurugenzi amewataka viongozi wa kila eneo kutengeneza utaratibu mzuri ambao utafanikisha zoezi la usafi  kufanikiwa kwa kuhakikisha wanasimamia kwa ukamilifu na kuwahimiza wananchi kuwa na tabia ya kusafisha maeneo wanaoishi kwa kuwa ni wajibu wao kufanya hivyo.

Hata hivyo tarehe tisa disemba kila mwaka huwa ni siku ya kusherehekea Uhuru wa Tanganyika uliopatikana miaka hamsini na nne iliyopita lakini kwa mwaka huu itaadhimishwa kwa kufanya usafi nchi nzima.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa