Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Na Beatrice Lyimo-MAELEZO
Kufanikiwa
kwa juhudi za Kutokomeza ugonjwa wa Malaria kutaufanya ulimwengu kuwa
mahali pazuri na salama pa kuishi kwa kizazi hiki na vizazi vijavyo na
kuwawezesha mamilioni ya watu kufikia malengo yao kimaisha.
Hivi
karibuni Tanzania imeungana na nchi nyingine Ulimwenguni kuadhimisha
siku ya Malaria duniani ambapo ni maalumu kwa ajili ya kuhamasisha umma
kuhusu umuhimu wa kuendeleza mapambano dhidi ya ugonjwa huo katika
jamii.
Takwimu
kutoka Shirika la Afya ulimwenguni WHO za mwaka 2002 zinaonyesha kuwa
kila mwaka watu kati ya milioni 300 hadi 500 duniani wanapata ugonjwa wa
malaria, kati yao watu milioni moja na nusu hufariki kutokana na
ugonjwa huo.
Kulingana
na takwimu hizo katika bara la Afrika watoto wadogo wenye umri chini ya
miaka mitano ndiyo wanaathirika zaidi na ugonjwa wa malaria ambapo kila
mwaka watoto milioni tano wanakufa kwa ugonjwa huo barani Afrika.
Kwa
mujibu wa WHO idadi vifo vinavyotokana na ugonjwa wa malaria hadi
kufikia mwaka 2013 vilipungua kwa takriban asilimia 20 tu duniani kote
katika muongo mmoja uliopita ambapo theluthi moja ya nchi 108 ambazo
malaria ilikuwa imeenea zilitarajiwa kutokomeza ugonjwa huo katika
kipindi cha miaka 10.
Kufuatia
ufanisi mkubwa uliopatikana chini ya malengo ya maendeleo ya milenia,
ni muhimu kuuendeleza ufanisi huu na kuutokomeza kabisa ugonjwa wa
malaria chini ya malengo ya maendeleo endelevu.
Kauli
mbiu hiyo inaenda sambamba na lengo la kuwa na ulimwengu usio na
malaria lilijumuishwa katika mkakati wa kiufundi wa kimataifa kwa ajili
ya malaria 2016 hadi 2030, ulioidhinishwa Mei mwaka uliopita na baraza
kuu la Afya duniani. Mkakati huo unalenga kupunguza kwa kiwango kikubwa
maambukizi ya malaria ulimwenguni katika kipindi cha miaka 15 ijayo.
Kwa
mujibu wa ripoti kuhusu malaria ya shirika la afya duniani (WHO) mwaka
2015, visa vya maambukizi ya malaria na vifo kutokana na ugonjwa huo
vilipungua tangu mwaka 2000. Ufanisi huenda ulipatikana kupitia utanuzi
wa vifaa na nyenzo za kuzuia na kutibu malaria, kama vile neti za mbu
zilizonyunyiziwa dawa, kupima malaria na utoaji wa dawa ya kuzuia
ugonjwa huo.
Takwimu
kutoka wizara ya afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia ,Wazee na wastoto
zinaonesha kuwa kila mwaka watanzania wapatao milioni 18 wanaugua
ugonjwa wa malaria hali ambayo inalifanya taifa kupoteza mapato mengi
ambapo inakadiriwa kila mwaka zaidi ya sh. milioni 350 zinapotea kwa
ajili ya malaria.
Malaria
ni ugonjwa wa kuambukizana unaoletwa na chembe chembe zinazoitwa
plasmodium.Chembe chembe hizi huingia ndani ya mwili wa binadamu baada
ya kuumwa na mbu wa kike kwa jina Anopheles.
Aidha
Mbu mwenye chembe chembe za plasmodium anapomuuma mtu humuingizia
baadhi ya mate yenye viini vya kuambukizana kwenye kidonda hivyo
kusambaza Malaria.
Viini hivyo husafiri hadi kwenye maini ambapo hukaa hadi vifikie ukomavu na kusababisha
homa inayoandamana na maumivu katika viungo vya mwili, kutokwa na
jasho, kutetemeka, kutapika na kupapatika kama mtu aliye na kifafa.
Katika kuhakikisha kuwa tatizo hilo linapatiwa ufumbuzi WAZIRI mwenye dhamana ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu anawataka watanzania kuunga mkono juhudi za Serikali kuutokomeza ugonjwa huo ambao umekuwa chanzo cha vifo vya watu wengi nchini.
Waziri Ummy anasema Serikali
imeendelea kutekeleza Mpango Mkakati wa Kudhibiti Malaria 2014 –2020
kwa kushirikiana na afua mbalimbali za kuzuia na kudhibiti ugonjwa wa
malaria nchini hivyo kupitia afua hizo kiwango cha maambukizi ya malaria
kimeshuka kutoka asilimia 18 mwaka 2008 hadi 9.2 mwaka 2011/12.
Anasema
kuwa mwaka 2014/15 Serikali ilisambaza dozi 12,911,100 za dawa mseto ya
kutibu malaria na vitendanishi vyenye jumla ya vipimo 28,130,736 vya
kupima malaria (mRDT), katika vituo ili kuthibitisha uwepo wa vimelea
kabla ya matibabu.
Anaongeza
kuwa vyandarua vipatavyo 500,000 viligawiwa katika shule za msingi na
Sekondari za Mikoa ya Lindi, Mtwara na shule 24 za mkoa wa Ruvuma
kupitia Programu ya Wanafunzi Shuleni pamoja na kunyunyizia dawa za
ukoko ndani ya nyumba katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa na katika nyumba
400,000 za wananchi.
Anaeleza
kuwa kuanzia mwaka 2015/16, Serikali imeanza kutekeleza mpango wa
kuangamiza viluwiluwi vya mbu kwa kutumia viuadudu vya kibailojia katika
kata za Jiji la Dar es Salaam pamoja na miji sita iliyofanyiwa
maandalizi ya Mpango huo ikiwemo Miji ya Kibaha, Mwanza, Musoma, Bukoba,
Shinyanga na Geita.
“Msisitizo
mkubwa wa Wizara yangu ni kwamba wananchi na wadau wote waone umuhimu
na kutoa kipaumbele katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Malaria kwa
kuhakikisha matumizi sahihi ya mikakati iliyopo katika kuuthibiti
ugonjwa huu”anasitiza Waziri Ummy.
Anasema
iwapo mikakati hiyo itatekelezwa ipasavyo ni dhahiri kuwa maambukizi
yataendelea kupungua kwa kiasi kikubwa na hatimaye kumaliza kabisa.
Kwa upande
wa Tanzania Visiwani Waziri wa Afya wa Zanzibari Mahmoud Thabit Kombo
alisema kuwa Zanzibar inaadhimisha siku hii kwa kujivunia mafanikio
makubwa yaliyopatikana katika kupambana na ugonjwa wa malaria.
Mhe.
Kombo anasema kuwa Katika maadhimisho ya mwaka huu wa 2016, Wizara yake
imepanga kutoa elimu kwa jamii juu ya njia mbali mbali za kijikinga na
malaria pamoja na maradhi mengine ya kuambukiza. Anasema malaria bado ni
tatizo kwa upande wa Zanzibar na katika mikoa yote ikiwemo Wilaya ya
Magharibi A na B, Wilaya ya Kati na Micheweni Pemba.
Anatoa
wito kwa wananchi kuendelea kutumia vyandarua vilivyotiwa dawa,
kusafisha mazingira tunayoishi ili kuondosha mazalio, kufunika maji
ndani ya mahodhi, mapipa na sehemu nyengine ili kujikinga na ugonjwa huo
na kuzuia fursa ya mbu kuzaliana.
“Ninatoa
wito kwamba mtu yeyote ndani ya familia anapojihisi kuwa ana homa ni
vema akaenda kituo cha afya kilichoko karibu nae ili kuchunguzwa kama
ana homa ya malaria, mtu asitumie dawa kwa kuhisi dalili za malaria bila
kufanyiwa uchunguzi”, anasisitiza Mhe.Kombo.
Kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwahutubia wananchi wakati wa maadhimisho Siku ya Malaria anasema kuwa Serikali inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali inayolenga kuboresha kinga dhidi ya ugonjwa huo na kuwahakikishia wananchi kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha tiba sahihi inapatikana kwa watu wote.
Bw.
Juma Hassan mkazi wa Buguruni mmoja wa waathirika wa Malaria nchini
anasema kuwa mazingira ya Tanzania yamekuwa ni mazalio ya mbu hali
inayochangia kueneza ugonjwa wa malaria ambao unamaliza maelfu ya watu
kila mwaka.
Anasema
ugonjwa wa malaria hauwezi kumalizika katika mazingira rafiki kwa
mazalio ya mbu, ametolea mfano baadhi ya maeneo nchini watu wamechimba
mabwawa ya kufugia samaki ambayo hayana samaki badala yale yamekuwa
mazalia ya mbu.
“Iwapo
katika mabwawa hayo kungekuwa na samaki, wangekula vimelea vya mbu na
kuzuia mbu kuzaliana pia usafi wa mazingira ungefanyika kikamilifu
mazalio ya mbu yangepungua na hatimaye malaria ingebakia historia’’,
alisisitiza.
0 comments:
Post a Comment