Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Na Jonas Kamaleki.
Wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inakusudia kutoa taarifa ya wanawake wanaofariki
Dunia kutokana na matatizo ya uzazi kila baada ya miezi mitatu ili kukabiliana
na tatizo la vifo vya wanawake nchini.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto, Ummy Mwalimu leo jijini Dar es Salaam wakati akifungua Mkutano wa Viongozi
Wanawake katika masuala ya Afya.
“Nimeamua kuhakikisha wanawake
wanapiga hatua na kuthaminiwa katika jamii, na nimeamua kuanza kutoa ripoti ya
robo mwaka kwa kila Halmashauri kuhusu taarifa ya wanawake wanaofariki kutokana
na matatizo ya uzazi,” alisema Ummy Mwalimu.
Ameeleza kuwa, katika uteuzi
atakaoufanya kwenye bodi zilizo chini ya Wizara yake, atahakikisha asilimia 30
ya wajumbe wa bodi hizo ni wanawake. Baadhi ya Bodi zilizo chini ya Wizara yake
ni pamoja MSD, TFDA na Bodi ya Wafamasia.
Aidha, Mhe. Ummy amemshukuru Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa
kutekeleza sera ya elimu bure ambapo amesema wazazi watalazimika kuwapeleka
watoto wa kike shuleni kwa wingi kuliko ilivyokuwa awali.
Katika kutilia mkazo suala la elimu
kwa wasichana, Waziri Ummy amasema watoto wa kike hawana budi kujitambua na
kuzingatia masomo ambayo ndiyo yatawafanya waweze kuchagulika au kuteuliwa
kushika nyadhifa kubwa za uongozi. “Hamsini kwa Hamsini bila elimu ni siasa tu”
alisisitiza Mhe. Waziri.
Mhe. Ummy amewataka wanawake
kujituma katika kufanya kazi ili kuibadilisha jamii. Hapa akaja na kauli mbiu
kuwa “Mwanamke akitenda, jamii itatenda, Tanzania Itasonga mbele’’.
Kwa upande wake Mwenyekiti
Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS), Bibi Fatuma Mrisho
amewasisitiza watoto wa kike kuthamini masomo na kuepuka ndoa za utotoni.
Amesema kuwa mtoto anapokuwa shuleni anaepuka Ukimwi kwa asilimia saba. Hivyo
amesema ni lazima wasichana kupenda shule na kuacha kurubuniwa na wavulana.
Huu ni mkutano wa utangulizi
kabla ya mkutano Mkubwa wa karne kuhusu Afya, Haki na Ustawi wa Wasichana na
wanawake ambao wajumbe zaidi ya 5,000 wakiwemo viongozi wa Dunia, Wasomi, Watunga
sera, Wanaharakati, Watu wa habari, dini, Vyama vya kijamii na Wawakilishi wa
sekta binafsi watashiriki.
0 comments:
Post a Comment