Baadhi ya Waandishi wa Habari wakifuatilia mada wakati wa
Semina kuhusu mabadiliko ya tabianchi na Afya iliyofanyika leo 3 Mei, 2016
Jijini Dar es Salaam.
|
(Picha zote na Benedict Liwenga)
Na
Benedict Liwenga-MAELEZO.
Wanahabari nchini
wametakiwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto katika kuelimisha na kuhamasisha jamii kuhusiana na mabadiliko ya hali
ya hewa na afya.
Akiongea kwa niaba ya
Mkurugenzi wa Huduma za Kinga Bi. Neema Rusibamayila wa Wizara hiyo, Dkt. Azma
Simba wa Kitengo cha Epidemolojia amesema kuwa suala la kuielimisha jamii lina umuhimu
ndo maana kuna haja ya Wizara kushirikiana kwa pamoja katika kutekeleza suala
hilo.
Ameeleza kuwa
Shughuli za kibinadamu zinachangia kwa kiasi cha asilimia 95 katika kuzalisha
na kuongeza kiasi cha gesi joto katika kwenye anga hewa ambapo amezitaja baadhi
ya shughuli hizo zikiwemo za uzalishaji viwandani, uzalishaji nishati, kilimo,ufugaji,
ukataji miti, uchomaji misitu, usafirishaji, pamoja taka.
Akitaja athari za mabadiliko
ya tabianchi, Dkt. Azma ameeleza kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa joto juu ya
wastani, ukame, mafuriko, vimbunga, kubadilika kwa mgawanyo na muda mvua
kunyesha pamoja na kuongezeka kwa kina cha bahari.
‘’Sisi sote ni mashahidi
wa mabadiliko ya hali hewa yalivyokuwa tishio katika afya ya binadamu. Mabadiliko
hayo yameendelea kuleta athari mbalimbali kwa jamii, mazingira na afya ikiwemo
upatikanaji wa maji safi na salama, hewa safi, uhakika wa upatikanaji wa chakula
na makazi salama’’, alisema Dkt. Azma.
Ameongeza kuwa athari
hizo zimepeleke uwepo wa magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ya kuambikiza ikiwemo
malaria, kuhara, kipindupindu, homa ya bonde la Ufa, denge, utapiamlo, magonjwa
ya mfumo wa upumaji na magonjwa ya mfumo wa fahamu.
‘’Jamii ina fursa ya
kuboresha afya yake na vizazi vijavyo endapo itaamua kubadilisha mfumo wa
maisha unaochangia uzalishaji na ongezeko wa jotogesi unaoharibu (ozone) yaani
tabaka hewa’’, aliongeza Dkt. Azma.
Kwa upande wake Msimamizi
wa Mradi wa Global Framework For Climate Services toka Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Geofrey Mchau amesema kuwa halli
ya hewa na tabianchi vinaweza kubadilika kiuhalisia (Naturally) au binadamu
wenyewe ambapo amefafanua kuwa lengo la semina hiyo ni kuoingeza wigo wa
matumizi wa taarifa ya hali ya hewa katika sekta mbalimbali ikiwemo afya pamoja
kuwajengea uwezo Wataalam katika ngazi ya Wizara kimkoa pamoja na Wilaya.
‘’Tukizipata taarifa
zinazohusiana na masuala ya hali ya hewa toka Mamlaka ya Hali ya Hewa
tunazitafsiri na tunazitumia kwa manufaa ya jamii’’, alisema Dkt. Mchau.
Naye Afisa Habari
toka Hospitali ya Taifa Muhimbili Bwana Saidi Makola ameeleza kuwa tafiti
zinazoendelea zinaonyesha kuwa kuna ongezeko la magonjwa yatonayo na mfumo wa
hewa na hayo yanatokana na mabailiko ya tabianchi, hivyo uwepo wa semina hiyo
kwa Wanahabari utasaadia kutambua masuala mbalimbali na kuwajengea uwezo katika
kuelimisha jamii.
Aidha, Afisa Habari
toka Wizarani hapo, Bi. Catherine Sungura amewaasa Wanahabari kuzingatia katika
kutafuta taarifa mbalimbali ili kuweza kuelimisha jamii kuhusiana na masuala
mbalimbali yanayohusu afya.
Semina hiyo imehusisha
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ikiwemo Ofisi ya
Makamu wa Rais, Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania
(TMA).
0 comments:
Post a Comment