Picha na Ally Daud- Maelezo
Na: Immaculate Makilika- MAELEZO
Dar es Salaam
BARA la Afrika limetakiwa
kuimarisha Utawala wa Sheria kupitia vyombo vya dola ikiwemo mahakama na
polisi ili kuisaidia mfumo huo kutetea maslahi ya wanyonge.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es
Salaam na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Balozi Augustine Mahiga wakati alipokuwa akifunga Mkutano wa siku
mbili wa Kimataifa kuhusu Utawala wa Sheria na Utawala bora.
“Lazima Afrika iimarishe vyombo
vyake vinavyosimamia Utawala wa sheria na Utawala bora kama Polisi na
Mahakama pamoja na kuwa na msimamo wa Bara katika kuzungumzia masuala
mbalimbali” alisema Balozi Mahiga
Balozi Maiga alisisitiza kuwa
rushwa imekua adui mkubwa katika Utawala wa Sheria, hivyo ni lazima
suala hilo lipatiwe ufumbuzi ili haki iweze kutendeka kwa watu wote.
Aidha, Balozi Maiga amemshukuru
Balozi wa Italia nchini Mhe. Luigi Scott kwa kufanikisha mkutano huo
pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya Sheria
(IDLO) Bibi. Irene Khani kwa uamuzi wa wake wa kuichagua Tanzania kuwa
mwenyeji wa mkutano huo.
“Mkutano huu ni wa kihistoria
utasaidia kuleta mageuzi katika Taasisi ama Vyombo vinavyosimamia
masuala ya Sera na Sheria ambayo yatachochea maendeleo mazuri katika
nchi za Afrika” alisema Balozi Mahiga.
Mkutano huo unaomalizika leo
ulikua na kauli mbiu isemayo “Kufikia agenda ya 2030 na agenda ya 2063:
Utawala wa Sheria kwa Maendeleo Endelevu ya Afrika”, umehusisha wadau
mbalimbali wakiwemo Mawaziri, kutoka nchi mbalimbali za Afrika, Mabalozi
kutoka ndani na nje ya Afrika pamoja na wawakilishi wa Mashirika ya
kutetea Haki za Binadamu ulimwenguni.
0 comments:
Post a Comment