Na Daudi Manongi-MAELEZO
Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda Biashara na Uwekezaji Prof Adolph Mkenda
amesema kuwa serikali imeondoa tozo ya uhakiki wa viwango vya ubora na usajili
katika kuanzisha viwanda vidogovidogo
katika shirika la viwango Tanzania Tanzania(TBS) ambao sasa unafanyika bure.
Prof Mkenda ameyasema hayo alipokuwa akitoa mada
katika uzinduzi wa Jukwaa la kuwezesha wanawake na akaunti ya mkopo ya MALAIKA
ambayo imeanzishwa katika benki ya Wanawake Tanzania.
Aidha amesema ameagiza kwa wilaya na vijiji
kuanzisha viwanda kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wanaunga mkono jitihada za
serikali ya awamu ya Tano na kuinua uchumi wa nchi yetu.
“Bidhaa za kilimo kwa sasa zinapewa dhamana na
hivyo basi nawaimiza wanawake waanzE kuanzisha viwanda vidogovidogo kwani
uanzishwaji wake ni bure.”Alisema Prof Mkenda.
Pia alisema kuwa kipato cha kati nchini
kinaongezeka siku hadi siku na kuwataka wanawake kutolima kwa mazoea na
kuwataka wafanye biashara kwa faida kwa kutumia teknolojia sahihi ili kuongeza
uzalishaji.
Katika upande mwingine aliwataka wanawake kutokata
tamaa katika kujiinua kiuchumi kwani Serikali ya awamu ya tano iko makini na
inaweka mazingira mazuri kwa wanawake kama kuondoa tozo zisizokuwa za lazima ili
kuvutia wawekezaji wa viwanda vidogo vidogo.
Katika uzinduzi huo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
muungano wa Tanzania Bi Samia Suluhu Hassan alizindua jukwaa hilo na akaunti ya
mikopo ya wanawake ya MALAIKA kupitia benki ya wanawake ambayo akaunti hiyo
itakuwa na mikopo yenye riba nafuu ya asilimia 5 kwa muda wa miezi sita,mafunzo
yanatolewa bure,hamna haja ya kuleta mchanganuo wa mahesabu na hakuna hitaji la
dhamana yenye lengo la kuwakwamua wanawake kiuchumi.

0 comments:
Post a Comment