Askofu Msaidizi wa wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Eusebius Nzigilwa.
WANANDOA wakongwe wanaoaminika kuwa na ndoa zenye umri mkubwa kuliko
zote ndani ya Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, wanatarajia
kutunukiwa tuzo maalumu, Jumapili wiki hii katika tukio linalotarajia
kukutanisha mamia ya wanandoa.
Tuzo hizo zitakazotolewa na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu hilo,
Eusebius Nzigilwa, zitakabidhiwa kwa wanafamilia watatu wanaoaminika
kuwa ndoa zao ni kongwe kuliko nyingine, katika hafla ya wanandoa
maarufu kama Kliniki ya Ndoa, itakayofanyika Msimbazi Centre katika
ukumbi wa Maranta.
Mmoja wa viongozi wanaoratibu tuzo hizo, Nolascus Mpota alisema
katika tukio hilo lililoandaliwa na familia ya wanamaridhiano na
kusimamiwa na Idara ya Kichungaji na Utume wa Familia ya Kanisa
Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, wanandoa hao watapewa tuzo, kama
moja ya kumbukumbu ya maadhimisho ya Mwaka wa Huruma ya Mungu.
“Tumepata uthibitisho wa ndoa yenye umri wa miaka 61, kutoka Parokia
ya Chang’ombe na ile ya miaka 57 kutoka Parokia ya Oysterbay. Hata
hivyo, tunasubiri uthibitisho wa ndoa yenye umri wa miaka 67 ambapo kwa
sasa wanandoa hawa wakongwe wako Mahenge, walikokwenda wiki mbili tu
zilizopita wakitokea Segerea walikokuwa wakiishi, na tunaamini huenda
ndio ikawa ndoa kongwe kuliko nyingine zote jijini Dar es Salaam,”
alisema Mpota.
Hata hivyo, alisema ikiwa wapo wanandoa waliodumu kwa miaka mingi
zaidi ya wale waliokwishajitokeza, watawapokea na kujinyakulia tuzo hizo
ambazo hakuzitaja ili kutoa nafasi ya kutangazwa siku hiyo.
Alisema katika kliniki hiyo, Nzigilwa atatoa baraka maalumu kwa
wanandoa hao na wote watakaoshiriki na itahudhuriwa na viongozi
mbalimbali wa dini, na kutatolewa mada na wataalamu wabobevu katika
masuala ya ndoa na malezi ya familia.
Alisema lengo kuu ni kuwakumbusha wanandoa juu ya umuhimu wa kutunza
na kuheshimu maisha ya ndoa na kutambua baraka na huruma ya Mungu
inavyowasaidia wanandoa na wanafamilia katika maisha yao “Ni siku ya
kutoka “out” na mwenzako wa ndoa, kula na kunywa na wanandoa wengine,
hivyo tunawakaribisha wanandoa.
Watakaopenda kushiriki wajiandikishe mapema Msimbazi Centre ofisi ya
mapokezi na kulipa ada ya kiingilio ya Sh 25,000 kwa kila mtu,” alisema
Mpota.
Chanzo Gazeti La Habari Leo
0 comments:
Post a Comment