Na Jacquiline Mrisho- MAELEZO
Wizara
ya Maji na Umwagiliaji imepewa mafunzo na Kampuni ya TRUNZ kutoka
Uswisi juu ya mitambo inayosafisha maji yenye chumvi na madini
yasiyotakiwa katika maji ili kusaidia ongezeko la upatikanaji wa maji
safi na salama nchini.
Mafunzo
hayo yametolewa leo Jijini Dar es Salaam na Mtaalamu wa Teknolojia
kutoka katika Kampuni hiyo, Ronny Graul ambaye ameelezea na kuonyesha
jinsi mitambo hiyo inavyosafisha maji yenye chumvi au madini
yasiyotakiwa hadi kuwa safi na salama kwa ajili ya matumizi ya binadamu.
“Mitambo
hii inatumia nguvu ya jua na umeme kidogo sana lakini inafanya kazi
kubwa ya kusafisha maji yenye chumvi na madini ambayo hayahitajiki
katika maji yakiwemo madini ya floride, chuma,zinki, shaba pamoja na
naitreti na kuyaacha maji yakiwa safi na salama katika viwango
vinavyohitajika na Shirika la Afya Duniani (WHO)”,alisema Graul.
Mtaalamu
huyo ameongeza kuwa mitambo hiyo inapatikana kiurahisi na ina uwezo
mkubwa wa kusafisha maji hasa kwa maeneo yenye visima vya maji yenye
chumvi pamoja na madini yasiyotakiwa ambapo kwa Tanzania maeneo
yaliyokithiri kwa kuwa na maji yenye chumvi nyingi ni Mtwara,Singida,
Dar es Salaam na Pwani.
Naye
Mkurugenzi Msaidizi Maji Mjini wa wizara hiyo, Muhandisi Mary Mbowe
alisema kuwa lengo la Wizara kuomba mafunzo hayo ni kufahamu namna gani
mitambo hiyo inavyofanya kazi ili kama itakidhi vigezo iweze kununuliwa
na kupelekwa katika maeneo sugu yenye maji ya chumvi hivyo, kusaidia
Watanzania wengi kupata maji safi na salama.
Kwa
upande wa Mkurugenzi Msaidizi wa Ubora wa Maji Philip Chacha pamoja na
wataalamu wengine wa ubora wa maji kutoka wizarani hapo wamesema kuwa
wamejidhihirisha kwa ubora wa mitambo hiyo na jinsi ilivyo na uwezo
mkubwa wa kusafisha maji kwa kwa muda mfupi hivyo, itaweza kuokoa maisha
ya Watanzania hasa waishio vijijini kwani wataepuka magonjwa
yanayosababishwa na maji yasiyo safi na salama.
Mitambo
hiyo imeundwa na mitambo miwili inayofanya kazi kwa pamoja ambapo
mtambo wa kwanza unajulikana kwa jina la AQUIFIER 200 unaotumika kuondoa
chumvi na madini yasiyotakiwa katika maji na mtambo wa pili unaitwa
SURVIVOR 300 ambao unachuja maji na kuyaacha yakiwa safi na salama kwa
kunywa bila kuchemsha wala kutia dawa ya kusafishia.

0 comments:
Post a Comment