Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com
Home » » SEKTA YA KILIMO YAZIDI KUAJIRI WANAWAKE NA VIJANA NCHINI

SEKTA YA KILIMO YAZIDI KUAJIRI WANAWAKE NA VIJANA NCHINI


Na Beatrice Lyimo-MAELEZO
Dar es Salaam


SERIKALI imesema sekta ya kilimo inaendelea kuwa sekta muhimu katika uchumi wa Tanzania kwa asilimia 25% ya pato la taifa na kuajiri asilimia 75% ya watanzania  wakiwemo wanawake na vijana.

Hayo yamesemwa leo na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano katika Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Richard Kasuga wakati wa uzinduzi wa mchezo wa redio uitwao KUMEKUCHA unaotarajia kuonyesha mchango wa wanawake na vijana katika kutokomeza tatizo la uhaba wa chakula nchini.

Kasuga  amesema kuwa igizo hilo la mchezo wa redio, litaakisi umuhimu wa ushirikishwaji wa wanawake na vijana katika kukuza sekta ya kilimo na kutoa ujumbe kwa vijana kuona umuhimu wa kilimo hasa kilimo cha biashara.

“Sheria na tamaduni zilizopo zinakwaza juhudi za mwanamke kupata fursa za kiuchumi kwa sababu hawana haki ya kumiliki ardhi au vifaa vya kilimo, vyanzo endelevu vya maji, ukosefu wa mikopo ambayo wanahitaji ili kufanikisha juhudi zao”alisema Kasuga.

Kwa upande wake mwakilishi kutoka shirika la msaada la Marekani (USAID) Randy Chester alisema kuwa mchezo wa KUMEKUCHA umeandaliwa na taasisi ya Africa Lead kwa kushirikiana na Media for Development International (MFDI) na kufadhiliwa na USAID kwa lengo la kupunguza uhaba wa vyakula vyenye virutubisho hapa Tanzania.

Mchezo wa KUMEKUCHA ni mchezo wa redio wa kila wiki ambao unaangazia maisha, vikwazo na fursa za wakulima Tanzania na utaanza kurushwa hewani kuanzia Julai 25, 2016 kupitia Redio Free Afrika, Redio Abood FM, Redio Ebony FM na Redio Bomba FM.

MWISHO
 
 

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa