Na Fatma Salum (MAELEZO)
Serikali
kupitia Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) imesema hivi karibuni itaanza
msako mkali wa kuwatafuta na kuwakamata wauzaji wa dawa zinazokatazwa
pamoja na vipodozi vikali ambao wanajitangaza kupitia mitandao
mbalimbali ya kijamii.
Hayo
yamesemwa na Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Umma kutoka TFDA Bi.
Gaudensia Simwanza wakati wa mahojiano na mwandishi wa habari hii kuhusu
kuibuka kwa watu wanaotangaza biashara ya dawa na vipodozi ambavyo
Serikali imevipiga marufuku.
Akitaja
bidhaa hizo Bi. Simwanza alisema ni pamoja na dawa za kuongeza ukubwa wa
viungo vya mwili, kupunguza uzito wa mwili na vipodozi vyenye kemikali
za kuchubua ngozi bidhaa ambazo zinasababisha madhara makubwa kwa
binadamu ikiwemo ugonjwa wa Saratani.
“Kumezuka
wafanyabiashara holela wanaotumia mitandao ya kijamii kama vile
Instagram, Facebook, Whatsup Groups na kwengineko kutangaza biashara ya
dawa na vipodozi vyenye kemikali hatari ambavyo vimepigwa marufuku na
TFDA hivyo wanaohusika wajiandae, hivi karibuni tutaanza
kuwashughulikia.” Alisema Simwanza.
Alibainisha
kuwa bidhaa hizo nyingi hazijathibitishwa na kupewa kibali na TFDA
hivyo wauzaji wanakiuka Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi Sura ya 219
inayowataka wafanyabiashara wote wa bidhaa hizo kuzisajili kabla
hazijaenda kwa mtumiaji na kutofanya hivyo ni kwenda kinyume na Sheria.
Alieleza
kuwa TFDA kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi wameandaa mkakati
madhubuti wa kuhakikisha wanawabaini na kuwakamata wafanyabiashara wote
wanaouza dawa na vipodozi hivyo kupitia mitandao na kuwachukulia hatua
ikiwemo kuwafikisha mahakamani au kuwatoza faini.
“Wengi wa
wafanyabiashara hao hawaweki anuani za maeneo wanayopatikana na hawana
maduka rasmi bali huweka namba za simu za mkononi lakini kwa kutumia
vyombo vya dola tutawabaini tu na kuwatia mbaroni.” Alisisitiza
Simwanza.
Kwa
upande wake Meneja Mawasiliano wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)
Bw. Innocent Mungy amewatahadharisha watumiaji wa huduma za mawasiliano
hasa matangazo ya biashara kuwa makini na matangazo hayo kwani baadhi
ya wafanyabiashara hizo wanaweza kuwa ni watu wenye nia mbaya.
Hivi
karibuni kumeibuka wimbi la wafanyabiashara wa dawa mbalimbali pamoja na
vipodozi ambao wanajitangaza kupitia mitandao ya kijamii na kuna baadhi
ya watu wananunua bidhaa hizo bila ya kuhakikisha usalama wake jambo
ambalo ni hatari kwa afya zao.
0 comments:
Post a Comment