(Picha/Habari na Benedict Liwenga-WHUSM)
Wadau wanaojishughulisha na masuala ya Sanaa nchini
wamehamishwa kujitokeza kwa wingi katika kusaidia maendeleo ya Sanaa kwa
kudhamini na kufadhili mashindano ya urembo bila kubagua.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Kaimu
Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Sanaa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo, Bw. Francis Songoro wakati alipokuwa akiwasilisha hotuba ya Naibu
Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Anastazia Wambura ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi
katika Mashindano ya Miss Tanzania Indian Ocean 2016 yaliyofanyika katika Ukumbi
wa MRC uliopo Mikocheni jijini hapa.
Akiwasilisha hotuba hiyo, Songoro amesema kwamba kazi
inayofanywa na wadau wa sanaa ni hatua ya utekelezaji wa Sera ya Taifa ya
Utamaduni ambayo inasisitiza jamii na wakuzaji sanaa kuendeleza ubunifu katika
kazi za kiutamaduni.
Ameeleza kuwa, Serikali kupitia Wizara yake inathamini na
kuunga mkono juhudi zinazofanywa na wadau hao hasa katika kukuza na
kuviendeleza vipaji vya vijana nchini, hivyo amewapongeza wadau hao kwa moyo
wao wa kujitoa na kuwataka kuendeleza kwa vitendo Sera ya Taifa ya Utamaduni ya
mwaka 1997 katika Sura ya 9 kifungu cha 9:5:8 ambacho kinasisitiza na kuhimiza
watu binafsi pamoja na Mashirika kuwekeza rasilimali katika sekta ya utamaduni.
‘’Maonyesho haya ni ishara tosha kuwa sanaa ni kazi, ajira,
biashara na burudani, hivyo kipekee nawapongeza sana’’, alisema Songoro.
Aliongeza kuwa, Warembo ambao wameshiriki katika mashindano
hayo wanautangaza utalii wa ndani na nje ya nchi na kwa kufanya hivyo
wanaiwakilisha vyema Tanzania Duniani katika mashindano ya Miss World na pia
kukuza uchumi wa nchi.
Aidha, amewataka warembo ambao hawakubahatika kuibuka
washindi katika mashindano hayo kutokata tamaa, bali waitumie fursa hiyo
hususani ya elimu waliyoipata wakiwa kambini kwa kuisadia jamii inayowazunguka
na kuwa wanawake wa mfano wa kuigwa katika kujitambua na kujiamini.
‘’Mtambue kwamba, siyo wote mtakaoibuka washindi na kuendelea
mbele katika mashindano haya, niwaombe wale ambao hamtashinda msivunjike moyo,
bali mkaitumie elimu mliyoipata na yale ambayo mmejifunza mkiwa kambini kwa
kuisaidia jamii inayowazunguka na muwe wanawake wa mfano wa kuigwa’’, alisema
Songoro.
Katika mashindano hayo, Mshindi wa Kwanza aliyeibuka na
kunyakua taji hilo ni Jackline Kimambo ambaye alipatikana kati ya tano bora na kuvikwa taji la Miss Tanzania Indian Ocean
2016 na Mshindi wa pili ni Regina Ndimbo huku wengine waliobaki kwenye tano
bora wamepata fursa ya kuingia katika mashindano ya Miss Kinondoni.
Shindano hilo lilihusisha jumla ya washiriki wapatao 20
ambapo mmoja kati yao ndiyo aliyeibuka mshindi na lilidhaminiwa na wadau
mbalimbali wakiwemo Mikocheni Resort Centre, Mlimani TV, Channel Ten, Darling,
Helmic, Tanzania Breast Cancer Foundation, Magic FM, Jozi Lounge, Kiss Printers
pamoja na NTS.
0 comments:
Post a Comment