Na Beatrice Lyimo-MAELEZO
29/07/2016
Dar es salaam
Watumishi
wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
wamechangia kiasi cha Tsh. Milioni 100 ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha
umma kuhusu zoezi la upatikanaji wa madawati katika shule za msingi na
Sekondari nchini.
Akikabidhi
mchango huo kwa Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa kwa niaba ya watumishi
wa wizara hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki Balozi Augustine
Mahiga amesema kuwa watumishi hao wametoa fedha hizo kwa shule ya
msingi Chamazi ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais la upatikanaji wa
madawati katika shule za msingi na sekondari nchini.
Balozi
Mahiga amesema Wizara yake iliwahamasisha watumishi wake walio makao
makuu na wale walio kwenye balozi mbalimbali nje ya nchi kuchangia zoezi
hilo la upatikanaji wa madawati.
“Ili
kufanisha upatikanaji wa fedha hizi Wizara yangu iliwahamasisha
watumishi wake wote walio Makao makuu na wale walio katika balozi zetu
duniani kote, wito
huu uliitikiwa kwa ari na hamasa kubwa na kufanikisha kukusanya kiasi
cha Shilingi 100,176,825.52 za kitanzania”alisisitiza Balozi Mahiga
Waziri
Mahiga aliongeza kuwa mara baada ya kukusanya fedha hizo watumishi wa
Wizara hiyo waliamua kumpatia aliyekuwa Mtumishi wa Wizara ambaye sasa
ameteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Manyoni kiasi cha shilingi Milioni 15
kwa ajili ya ununuzi wa madawati katika Wilaya yake.
Aidha, amesema kiasi fedha zilizobaki zaidi ya shilingi milioni 85 zilikabidhiwa kwa Waziri Mkuu wa Tanzania, Mhe Kassim Majaliwa kwa ajili ya mchango wa utengenezaji wa madawati ya shule ya Msingi Chamazi iliyoko Wilaya ya Temeke Jijini Dar es Salaam.
Waziri
Mahiga aliongeza kuwa mbali na wizara yake kuwa na majukumu mbalimbali
bado inalo jukumu la kuhakikisha inaitangaza Tanzania ili kuvutia
wawekezaji na kukuza uchumi wa nchi, na kuongeza kuwa elimu bora ni
msingi imara katika kufanikisha hilo.
0 comments:
Post a Comment