Home » » Ujio wa muigizaji Lucy uwe chachu kwa maendeleo ya sanaa nchini

Ujio wa muigizaji Lucy uwe chachu kwa maendeleo ya sanaa nchini



Na. Immaculate Makilika- MAELEZO
Mkurugenzi wa Idara ya habari (MAELEZO) Bw. Hassan Abbas amesema kuwa ujio wa msanii wa maigizo kutoka nchini Marekani Bi. Toussaint Duchess maarufu kama Mama Lucy uwe changamoto kwa wadau wa sanaa nchini.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo  Mheshimiwa Nape Nnauye aliyekuwa mgeni rasmi  kwenye  uzinduzi wa igizo la   msanii Lucy linaloitwa Mama Lucy anakwenda Afrika (Mrs. Lucy goes to Africa)  mwishoni mwa wiki Jijini Dar es salaam.
Mkurugenzi Abbas alisema kuwa ni vyema  wadau wa sanaa wakatumia ujio huo kama changamoto itakayowasaidia kujifunza na kuwa  wabunifu zaidi katika kazi zao za sanaa.
“Ujio wa muigizaji Lucy ni changamoto kwa wadau wa sanaa nchini, ni fursa ya kujifunza kwa wasanii hususani katika eneo la sanaa za jukwaani, vile vile ni fursa kwa vijana wa kitanzania ambao wanatarajia kufanya kazi  za sanaa” alisisitiza Bw. Abbas
Aliendelea kwa kusema kuwa Serikali inatoa pongezi kwa kituo cha televisheni cha Azam na wasanii mbalimbali wakiwemo Suzan Lewis (Natasha) na Yvone Cherry (Monalisa) ambao wameshiriki  kwa ubunifu wa kumleta msanii huyo nchini pamoja na maboresho mengine yanayofanywa na kituo hicho cha televisheni cha Azam.
Aidha, aliongeza kuwa  akiwa Msemaji wa Serikali, anatarajia kushirikiana  na wadau wa sanaa  nchini kupitia mikakati mbalimbali itakayoandaliwa ili kuunga mkono juhudi aliyoanza Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli katika kujali na kusimamia kazi za sanaa na wasanii ili waweze kunufaika na kazi zao.
Kituo cha televisheni cha Azam kinatarajiwa kuonesha igizo hilo la msanii huyo kutoka nchini Marekani liloandaliwa kwa kushirikiana na wasanii mbalimbali kutoka nchini wakiwemo Suzan Lewis (Natasha) na Yvone Cherry (Monalisa) pamoja na filamu mbalimbali zitakazofanywa na msanii huyo.

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa