Home » » Dumisheni Michezo kuongeza ufanisi katika kazi; Katibu Mkuu Kiongozi.

Dumisheni Michezo kuongeza ufanisi katika kazi; Katibu Mkuu Kiongozi.

Na Shamimu Nyaki WHUSM.
Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi amewataka Watumishi wa Umma kushiriki katika Michezo mbalimbali ili kuwa na afya imara itakayosaidia ufanisi katika kutekeleza kazi zao.
Balozi Kijazi ametoa rai hiyo leo Jijini Dar es Salaam katika hotuba yake iliyosomwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais  Utumishi  Dk.Lawrence  Ndombaro katika  Bonanza  la  Michezo la  ufunguzi wa mashindano  ya thelatini  na nne yanayojulikana kama  SHIMIWI  lililofanyika katika Uwanja wa Uhuru wa Jijini  humo.
“Michezo inasaidia mwili kuwa na afya njema na kuondoa msongo wa mawazo pamoja na kuleta nguvu na akili katika mwili vinavyosaidia  katika utendaji bora wa Mtumishi kwa maendeleo ya Taifa”.Alisema Balozi Kijazi.
Aidha Katibu  Mkuu  Kiongozi  Balozi  Kijazi  amewataka  Viongozi wa Serikali na Taasisi  zake kutenga muda kwa Watumishi  wanamichezo  wa kufanya mazoezi  pamoja na kuwapatia  vifaa vya michezo ili waweze kufanikiwa  katika mashindano  hayo.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni,Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel amewapongeza Watumishi wake kwa kushiriki Bonanza hilo na kuahidi kuwapa muda mzuri wa maandalizi ili wafanye vizuri katika mashindano hayo.
Akifafanua maandalizi ya timu ya Wizara ya Habari,Utamaduni, Sanaa na Michezo Mwenyekiti wa timu hiyo Bw. John Manyika ameahidi ushindi kwa timu yake kwani wanaendelea kijiandaa vizuri katika mazoezi.
Mashindano ya SHIMIWI yanatarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu mjini Dodoma kuanzia tarehe 14 ikiwa ni kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kmbarage Nyerere.
Bonanza hilo lilimalizika kwa timu ya Jiji la Dar es Salaam kutwaa Kikombe kwa kuwa na wanamichezo wengi ikifuatiwa na Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi.
MWISHO
 

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa