Home »
» Erick Mashauri aelezea jinsi VAT inavyoathiri biashara utalii, aiomba serikali kupitia tena ongezeko hilo
Erick Mashauri aelezea jinsi VAT inavyoathiri biashara utalii, aiomba serikali kupitia tena ongezeko hilo
Kufuatia serikali kupitisha muswada wa ongezeko la VAT kwa watalii ambao wanakuja nchini kwa ajili ya kutembelea vivutio mbalimbali, MO Blog imepata nafasi ya kufanya mahojiano na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Travel Partner, Erick Mashauri ili kujua ni kwa kiasi gani ongezeko hilo limeathiri biashara kwa makampuni yanayopeleka watalii mbugani na kwa sekta ya utalii kwa ujumla.
Mashauri alisema kuwa ongezeko la VAT kwa watalii limeathiri kwa kiasi kikubwa biashara zao kwani serikali ilifanya maamuzi ya haraka bila kuangalia athari ambazo zingejitokeza baada ya kupitisha muswada na haikuwashirikisha wao kama wadau wa karibu ambao wanafanya biashara ya kuwahudumia watalii wawapo nchini.
"Ongezeko la VAT ambalo serikali ilifanya limevuruga biashara ya utalii, ilisahau kama wageni hawa huwa wanafanya booking mwezi mmoja kabla ya safari, tukashangaa serikali inapeleka muswada haraka haraka bungeni na kuupitisha bila kuangali athari ambazo zitajitokeza,
"Baada ya kuongeza VAT ilibidi makampuni ya utalii yarudishe pesa kwa watalii na wengine wametaka kupelekana hata mahakamani kwani tayari wameshaingia mikataba alafu anakuja unaanza kumwambia tena inabidi alipie VAT, jambo ambalo nchi kama Kenya tayari wameitoa kwani waliona jinsi inavyoathiri utalii lakini hapa kwetu ndiyo tunaileta," alisema Mashauri.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Travel Partner, Erick Mashauri akizungumza kuhusu ongezeko la VAT limevyoathiri biashara ya utalii kwa makampuni yanayowahudumia watalii wawapo nchini. (Picha zote zimepigwa na Rabi Hume, MO BLOG)
Mashauri alitumia fursa hiyo kuiomba serikali kupitia tena muswada huo na kuangali jinsi gani ongezeko la VAT linakavyoathiri biashara ya utalii nchini na ikiwezekana iitoe ili watalii wengi waje nchini na serikali iweze kupata pesa nyingi tofauti na sasa ambapo imeongeza VAT ambayo inachangia watalii kupungua.
"Serikali inasema bora waje watalii wachache lakini wanaolipa VAT, wakija watalii wa VIP au wa kawaida wote wanatoa pesa sawa na kwanza watalii wa VIP ambao wanawataka wao hata hoteli wanazotumia wakiwa hifadhi kama Serengeti sio za watanzania, zinamilikiwa na watu wa nje,
"Nafikiri serikali ipitie tena VAT na tozo inayofanywa na TANAPA kwani zote ni pesa za serikali, iangalie jinsi gani gharama hizo zinatuathiri, hakuna haja ya kuweka gharama kubwa hawa watu hawaondoki na hizo hifadhi, waweke gharama za kawaida ili watalii waje wengi zaidi," alisema Mashauri.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Travel Partner, Erick Mashauri ameiomba serikali kupitia tena muswada wa VAT ili ikiwezekana itolewe kwani ongezeko hilo linaweza kusababisha idadi ya watalii wanaokuja nchini kupungua kwa kiasi kikubwa.
Aidha Mashauri aliishauri serikali kufanya mabadiliko ya matangazo ambayo imekuwa ikiyatumia kujitangaza kimataifa ya kutumia viwanja vya michezo kuwa njia hiyo haiwezi kusaidia kwa kiasi kikubwa kama inavyotarajia na badala yake itumie vyombo vya usafiri.
"Wanaokwenda mpirani wengi hawapendi utalii, njia rahisi ni kuingia mikataba na makampuni ya mabasi na treni, wakitangaza wale hapa tutawakimbia watalii, wanaingia mikataba mara moja na tangazo linakaa mwaka mzima, hebu fikiria mfano Uingereza kuna mabasi zaidi ya 300, kama tangazo kila siku likionwa na watu milioni moja tu kwa mwaka tutapata watalii wengi," alisema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Travel Partner, Erick Mashauri akielezea jinsi watalii wanavyonyang'anywa vinyago wanavyo nunua nchini na kuiomba serikali iliangalie jambo hilo na kuwaruhusu watalii kuondoka na vinyago hivyo kwani wao ndiyo wateja wakubwa wa biashara hiyo.
Pia Mashauri aliiomba serikali kuweka utaratibu wa watalii ambao wanakuja nchini kuruhusiwa kuondoka na vinyago ambavyo wamekuwa wakinunua nchini kwani hizo ndizo zawadi ambazo wanaweza kuzipata nchini na kuwapelekea ndugu zao katika nchi ambazo wametoka.
"Kuna tatizo kubwa la watalii kunyang'anywa vinyago wakifika uwanja wa ndege, hivi wanadhani hawa watalii zawadi gani wanaweza kuipata nchini tofauti na vinyago maana vingine ata kwao vipo, lakini watalii wakifika uwanja wa ndege wafanyakazi wa pale wanavichukua eti hawana kibali cha kuondoka navyo,
"Watalii wanakuwa wanaona nchi yetu hakuna mfumo wa kufanya kazi pamoja maana anayeuza vinyago amepewa leseni ya kuuza na mteja wa hivyo vinyago ni nani kama sio watalii, nadhani iliangalie jambo hilo kwakweli limekuwa likiwakera sana watalii pindi wanapokuwa wanarejea nchi walizotokea," alisema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Travel Partner, Erick Mashauri akizungumza na waandishi wa habari ambao walimtembelea ofisini kwake mwishoni mwa wiki iliyopita.
Kuhusu Erick Mashauri amekuwa mmoja wa washindi wa tuzo za Top 100 kupitia kampuni yake ya Travel Partner ikishika nafasi ya 30 kati ya kampuni 100, amekuwa akifanya biashara ya kupeleka watalii katika hifadhi mbalimbali tangu mwaka 2007 na kupitia kampuni yake ametoa ajira rasmi kwa watanzania wasiopungua 90.
Na Rabi Hume, MO BLOG
0 comments:
Post a Comment