Na: Lilian Lundo - MAELEZO
Serikali
kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imejizatiti kuondoa
tabaka la wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu kwa vijana na watu
wazima kwa kujenga uwiano sawa wa utoaji wa elimu kwa watu wote.
Hayo
yamesemwa na Kaimu Kamishna wa Elimu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na
Teknolojia Bw. Nicholaus Bureta ambaye alimuwakilisha Mgeni Rasmi,
Katibu Mkuu wa wizara hiyo katika Maadhimisho ya Siku ya Kisomo Duniani,
yaliyofanyika leo, katika viwanja vya Makumbusho ya Taifa Jijini Dar es
Salaam.
“Wizara
imejipanga vizuri, na lengo kubwa la wizara ni kuhakikisha tunakuwa na
mtanzania aliye elimika na aliye na stadi, maarifa na uwezo wa kutumia
elimu aliyoipata,” alifafanua Bureta.
Vile
vile Bw. Bureta amesema kwa sasa wizara ipo kwenye mpango wa kukuza
stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) ambao unaanzia chini kwa
wanafunzi wa awali mpaka shule za msingi.
Katika
mpango huo walimu wamekuwa wakipata mafunzo mbalimbali ya namna ya
kumuwezesha mwanafunzi kujua Kusoma Kuandika na Kuhesabu katika ngazi ya
elimu ya awali.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi Msaidizi Elimu ya Watu Wazima na Elimu Nje ya
Mfumo Rasmi, Basilina Levira amesema kwamba kwa mujibu wa sensa ya mwaka
2012, asilimia 78 ya vijana na watu wazima ndio waliokuwa wakijua
kusoma na kuandika.
Akaongeza
kuwa mwaka 2015 idadi hiyo ya wanaojua kusoma na kuandika ilishuka na
kufikia asilimia 77 ambapo ilipelekea wizara hiyo kutoka na mikakati
inayokusudia kuondoa kabisa tabaka la watu wasiojua kusoma na kuandika
nchini.
Aidha,
Basilina amesema kuwa Serikali ilipitisha sheria ya vyumba vya madarasa
ya shule zote nchini kutumika kufundishia vijana na watu wazima ambao
hawajui kusoma na kuandika muda wa jioni baada ya wanafunzi wa kawaida
wanapomaliza masomo yao.
Amefafanua
kwa kusema kuwa, wizara imeandaa programu ambayo iko kwenye mfumo wa
Televisheni na picha za video (DVD) yenye masomo 65 ya kujifunza kusoma,
kuandika na kuhesabu, ambapo kwa kutumia program hiyo mwanafunzi
anaweza kujua kusoma, kuandika na kuhesabu kwa muda wa miezi 4 mpaka 6.
Mafunzo
hayo kwa njia ya Televisheni na Picha za Video tayari yameanza kutumika
kwa wilaya za Ilemela, Dodoma Manispaa, Songea Manispaa, Bagamoyo,
Mkuranga, Temeke, Ilala na Kinondoni, ambapo asilimia 65
ya vijana na watu wazima wasiojua kusoma na kuandika wamejitokeza
kujiunga na Elimu hiyo huku idadi kubwa ikiwa ni ya wanawake.
Siku
ya Kisomo Duniani huadhimishwa Duniani kote kila ifikapo Septemba 08 ya
kila ya mwaka, ambapo mwaka huu 2016 maadhimisho hayo yametimiza miaka
50 tangu yalipoanza kuadhimishwa mwaka 1966.
.........................Mwisho...................
0 comments:
Post a Comment