Home » » Tanzania na Iran kuanzisha wiki ya Utamaduni.

Tanzania na Iran kuanzisha wiki ya Utamaduni.

Na Raymond Mushumbusi WHUSM.

Serikali ya Tanzania na Iran zakubaliana kuanzishwa kwa wiki ya Utamaduni itakayowezesha kujifunza namna ya kuukuza ,kuulinda na kuendeleza sekta hiyo.

Makubaliano hayo yamebainishwa leo Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye alipokutana na Naibu Waziri wa Utamaduni kutoka Iran  Mhe. Abuzar Ebrahimi Turkaman kujadili masuala ya ushirikiano katika sekta ya Utamaduni kati ya Tanzania na Iran.

Waziri Nnauye alisema kuwa amekubaliana na wazo la kuanzishwa  kwa wiki ya Utamaduni kati ya Tanzania na Iran  ni fursa pekee ya kujifunza kutoka kwao namna ya kuukuza, kuulinda na kuuendeleza utamaduni wa mtanzania.

“Utamaduni ni silaha ya upendo na nimefurahia wazo la kuanzisha wiki ya Utamaduni na tuko tayari kujifunza kutoka kwenu na hakika tumelipokea na tunaamini fursa hii italeta mafanikio makubwa katika sekta hii”, alisema Mhe. Nnauye.

Kwa upande wa Naibu Waziri wa Utamaduni Iran Mhe. Abuzar Ebrahimi Turkaman aliihakikishia Serikali ya Tanzania kuwa wataendelea kushirikiana katika masuala ya Utamaduni na kuendelea kujifunza kutoka kwa watanzania namna bora ya kuuenzi,kuuendeleza na kuutunza Utamaduni.

Naibu Waziri huyo wa Iran aliendelea kusema serikali yake iko tayari kushirikiana na Tanzania katika uandaaji wa Filamu na kubadilishana uzoefu katika masuala ya filamu kati ya nchi hizo mbili.

Hata hivyo Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Nnauye alipata mwaliko kutoka kwa  Naibu Waziri wa Utamaduni Iran Mhe. Turkaman kwenda nchini Iran kujionea vivutio vya Utamaduni.

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa