Na
Frank Shija
MAELEZO
Dar
es Salaam
WATANZANIA wameaswa kujenga
utamaduni wa kulipa kodi na kudai risiti pindi wanapofanya biasha au kununua
bidhaa ili kuisaidia Serikali kukusanya mapato kwa ajili ya kuendelea kutoa
huduma za kijamii.
Wito huo umetolewa jana
Jijini Dar es Salaam na Afisa Mwandamizi wa Idara ya Huduma na Elimu kwa Mlipa
Kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bibi. Rose Mahendeka alipokuwa
akitoa elimu kwa waumini wa Kanisa la Ufufuo na Uzima kuhusu umuhimu wa kulipa
kodi.
Rose alisema kuwa shughuli
za Serikali katika nchi yeyote duniani, ikiwemo Tanzania zinagharamiwa na fedha
zinazotokana na kodi pamoja na tozo mbalimbali.
“Katika maandiko
matakatifu imeandikwa; Ya Kaisari mpeni Kaisari, vya Mungu mpeni Mungu, hivyo
ni vyema tukajenga utamaduni wa kulipa kodi na kudai risiti kwa ajili ya maendeleo
ya nchi yetu”. Alisema Rose.
Alisema umuhimu wa
kudai risiti kuwa ni pamoja mwananchi
kutambua kiasi cha kodi anayochangia Serikali yake, kutambua kodi halisi
inayotakiwa kulipwa na ushahidi wa ununuzi wa bidhaa na uhalali wa umiliki wake.
Aliongeza kuwa
kutodai risiti ni kwenda kinyume na matakwa ya sheria ya mlipa kodi ambapo
adhabu yake ni faini ya pointi za fedha
2 hadi 100 ambazo ni sawa na shilingi 30,000 mpaka 1,500,000/=.
Kwa upande wake Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Dkt. Amon Mpanju aliupongeza uongozi
wa Kanisa hilo kwa kuona haja ya waumini wake kupatiwa elimu ya mlipa kodi.
Aidha aliwaka waumini
wa kanisa hilo kulipa kodi na kufanya kazi kwa bidii ili kufikia malengo ya
kuwa na Tanzania mpya kama ambavyo baba wa Kanisa hilo Askofu Josephat Gwajima
amekuwa akisisitiza.
Askofu Mkuu wa Kanisa
la Ufufuo na Uzima Dkt. Josephat Gwajima amewahimiza waumini wake kuishika na
kuitumia elimu waliyopata kutoka kwa mwakilishi wa TRA ambapo aliwataka waumini
hao kujenga utamaduni wa kudai risiti kila anapofanya malipo ili kusaidia
ukusanyaji wa mapato ya Serikali.
MWISHO.
0 comments:
Post a Comment