Na Eleuteri Mangi,
MAELEZO
Watafiti wa masuala
mbalimbali ya kijamii nchini wametakiwa kuhakikisha wanafanya tafiti ambazo
zitawasaidia watu wenye ulemavu kupata vifaa saidizi ili waweze kumudu
kuendesha maisha yao ya kila siku.
Hayo yamebainishwa na
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Watu wenye Walemavu
Dkt. Abdallah Possi alipokuwa akizindua taarifa mpya ya utafiti inayobainisha
hali halisi ya ulemevu na uzee nchini jijini Dar es salaam.
“Serikali inafarijika
inapoona watu wanafanya utafiti ili kuwasaidia watu wenye ulemavu waweze kupata
vifaa saidizi na ni kitu gani kifanyike ili NGOs ziweze kujikwamua kiuchumi na
kuwasaidia wenye mahitaji” alisema Dkt. Possi.
Kuhusu suala la
unyanyapaa kwa watu wenye ulemavu, Dkt. Possi amesema kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu
hapo tayari kuona wananchi wananyanyapaliwa huku akisisitiza kuwa watu wote ni
sawa na ofisi hiyo ina “zero tolerance” kwa watu wanaowanyayapaa mlemavu.
Katika masuala ya
kisheria kwa watu wenye ulemavu, Dkt. Possi amesema kuwa inapotokea mlemavu au
mzee amefanyiwa kosa taarifa itolewe mara moja ili hatua za kisheria
zichukuliwe dhidi ya waliofanya makosa hayo na haki iweze kutendeka.
Naibu Waziri Dkt.
Possi pia amezitaka Asasi zinazoshughulika na watu walemavu wafanye kazi kwa
pamoja ili kuwasaidia walengwa ambao ni walemavu, watoto na wazee na kuwataka
kutumia fursa waliyonayo ya kupata msaada kisheria bure kutoka kwenye taasisi
za sheria ikiwemo Chama cha Mawakili (Tanganyika Law Society), TAMWA pamoja
na taasisi nyingine za kisheria wakati
masuala ya jianai amewataka wayapeleke kwenye polisi kwa hatua zaidi za
kisheria huku akisisitiza kumshirikisha inapobidi kufanya hivyo.
Akitoa maelezo ya utafiti
huo wakati wa uzinduzi, Mtafiti kutoka Taasisi ya Afya Ifakara (IHI) Bakar
Fakih amesema kuwa utafiti huo umewashirikisha watafiti rika mbalimbali
wakiwemo wazee na watu wenye ulemavu na kubainisha kuwa bado kuna imani potofu
kwenye jamii juu ya wazee na watu wenye ulemavu.
Utafiti huo
unaoongozwa na kaulimbiu “Ulemavu na uzee sio laana” umebainisha kuwa watu
wenye ulemavu na wazee nchini wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo
kupata elimu, huduma za afya, unayanyasaji wa kingono na kuvunjika kwa ndoa,
kutokujaliwa na familia pamoja na kutengwa kwa watu wenye ualbino kutokana na
mila potofu.
Kwa upande wake
mtafiti rika Blandina Isaya amesema kuwa walemavu waachwe wafanye maamuzi
yanayohusu maisha yao ikiwemo masuala ya ndoa wawe huru kuchagua wenza wao
badala ya kuchaguliwa na familia zao kwa kuwa wanahaki kama watu wengine wasio
na ulemavu.
Katika kuhakikisha
familia zinakuwa imara kiuchumi, Blandina amesema kuwa familia zenye watu wenye
ulemavu na wazee wapewe elimu ya ujasiriamali ili waweze kuwa na uwezo wa
kuendesha maisha yao kwa kulea familia ipasavyo na kuomba Seriklai za mtaa ziwe
na takwimu za wazee na watu wenye ulemavu.
Mwisho.
0 comments:
Post a Comment