Wizara
ya Maliasili na Utalii kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania -TFS
imechangia miche ya miti 3,000 katika Kampeni ya Upandaji Miti Jijini
Dar es Salaam iliyozinduliwa leo na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza
na vyombo vya habari Jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Mtendaji Mkuu wa
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Prof. Dos Santos Silayo alisema
hatua hiyo ni kuunga Mkono Kampeni ya Mkuu wa Mkoa huo, Paul Makonda
ambayo imetambuliwa kwa jina la "Mti Wangu" kwa ajili ya kupendezesha na
kuhifadhi Mazingira ya Jiji hilo.
"Sisi
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania tuna jukumu la kuanzisha na
kusimamia misitu na rasilimali zake nchini, katika kumuunga Mkono Mkuu
wa Mkoa wa Dar es Salaam kwenye upandaji wa miti, tumetoa miche ya miti
3,000 katika uzinduzi wa kampeni hiyo, na miche mingine 5,000 tutaitoa
kwa ajili ya kupandwa wakati wa masika, tunaomba wananchi wajitokeze kwa
wingi na kutuunga mkono katika kampeni hizi za upandaji wa miti"
alisema prof. Dos Santos.
Awali
akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Mama Salma Kikwete,
Kijitonyama Jijini Dar es Salaam ambapo pia alikabidhi miche mingine ya
miti 600 kwa ajili ya shule hiyo, Kaimu Mtendaji Mkuu huyo aliwaasa
wanafunzi hao kuwa mstari wa mbele katika kupenda mazingira, kupanda
miti na kuitunza. Pia aliiasa jamii kwa ujumla kuacha mara moja
uharibifu wa misitu kwakuwa ni kinyume cha sheria.
Naye
Naibu Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira na Muungano,
Luhaga Mpina akizungumza na waandishi wa habari katika tukio hilo,
alisema asilimia 61 ya nchi inakaribia kuwa jangwa kutokana na uharibifu
wa mazingira unaosababishwa na ukataji wa miti kwa ajili nishati ya
mkaa na rasilimali nyingine za misitu."Takriban hekta laki 3.72 za msitu kwa mwaka zinaharibiwa hapa nchini jambo linalopelekea asilimia 61 ya ardhi kuwa hatarini kuwa jangwa hivyo Serikali imeamua kuchukua hatua za makusudi kunusuru hali hiyo" alisema.
Akizungumzia hatua hizo za Serikali alisema umeandaliwa mpango wa miaka mitano wa kitaifa wa upandaji miti ambapo kila Wilaya nchini imepangiwa kupanda miti milioni 2 kwa mwaka.
Mpina alisema kuwa baadhi ya viongozi wa vijiji na halmashauri wamekua wakifanya kazi kwa mazoea kwa kutoa taarifa za uongo kuhusu kazi za upandaji wa miti katika maeneo yao, hivyo kuahidi kutembelea kila Mkoa na Wilaya kuona kama kweli miti inayotolewa na Serikali inapandwa ipasavyo.
"Sitokubali kuona Ilani ya uchaguzi ikichakachuliwa na baadhi ya viongozi wasio waadilifu, tutafuatilia kila Wilaya na Mkoa kuona kama agizo hilo linatekelezwa" alisema Mpina.
Aliongeza kuwa mpango mwingine ya Serikali ni kupeleka nishati ya gesi kwenye kaya zaidi ya milioni 30 nchini ili ziondokane na matumizi ya mkaa kunusuru misitu na mazingira. Alisema kuwa mpango huo utazishirikisha Wizara mbalimbali ikiwemo Nishati na Madini.
Alitoa wito kwa wananchi kushirikiana na Serikali katika zoezi la upandaji wa miti kutunza mazingira na kuepuka uharibifu wa misitu.
MWISHO
Hamza Temba
Wizara ya Maliasili na Utalii
0713635204

0 comments:
Post a Comment