Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Serikali
imesimamisha shughuli za Mfuko wa Wakfu wa Kuendeleza Zao la Korosho
ili kupisha uchunguzi wa matumizi ya fedha za mfuko huo.
Hatua
hiyo imechukuliwa baada ya Mfuko huo kushindwa kutekeleza majukumu yake
kikamilifu pamoja na kuwepo kwa malalamiko ya muda mrefu kuhusu
utendaji wa mfuko huo.
Uamuzi
huo umechukuliwa leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa Kilimo, Mifugo
na Uvuvi, Dkt. Charles Tizeba alipokuwa akizungumza na waandishi wa
habari juu ya mafanikio na changamoto ya zao hilo.
Dkt.
Tizeba alisema kuwa lengo la uanzishwaji wa mfuko huo lililoafikiwa na
Serikali pamoja na wadau wa korosho limekuwa halifanani na utekelezaji
wake kwani maendeleo yote yanayoonekana kwenye zao hilo hayatokani na
uwepo wa mfuko bali yanatokana na nguvu ya Serikali.
“Baada
ya kutafakari utendaji wa mfuko huo tumegundua kuwa mfuko umeshindwa
kutimiza malengo yaliyodhamiriwa, umeshindwa kusimamia na kutekeleza
maelekezo mbalimbali yanayotolewa na Bodi ya Korosho hivyo tumeamua
kusitisha shughuli za mfuko huo na kuanzia leo shughuli hizo
zitatekelezwa na Bodi ya Korosho mpaka hapo tutakapotoa maelekezo
mengine.”alisema Waziri huyo.
Waziri
aliongeza sababu nyingine za kusitishwa kwa Mfuko huo ni kujihusisha na
vitendo vinavyohujumu wakulima wa zao hilo hasa wakati wa ununuzi wa
pembejeo pamoja na kununua viuatilifu vilivyo chini ya kiwango kwa bei
kubwa, matumizi mabaya ya fedha kinyume cha Sheria na Kanuni za mfuko
pamoja na kushindwa kutekeleza agizo la Serikali kwa kuweka fedha kwenye
amana za muda maalumu katika Benki mbalimbali badala ya kupeleka Benki
Kuu.
Aidha,
Dkt. Tizeba alimtaka Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania
anapowasilisha fedha zilizokusanywa na watu wanaosafirisha korosho nje
ya nchi kuwasiliana kwanza na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho ili
kufahamu usimamizi na utaratibu wa fedha hizo.
Kwa
upande mwingine, Dkt. Tizeba ameizuia Menejimenti ya mfuko huo kufanya
muamala wowote wa fedha za mfuko mpaka hapo maelekezo ya hatima yao
yatakapotolewa na badala yake miamala yote itafanyika kwa utaratibu
utakaopangwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo pamoja na Katibu Mkuu wa
Wizara ya Fedha na Mipango.
Ameiagiza
Bodi ya Korosho kusimamia kwa haraka jukumu la upatikanaji wa pembejeo
na viuatilifu kwa sababu msimu wa zao hilo umekaribia.
0 comments:
Post a Comment